Utaweza kupanda gari inayojiendesha yenyewe?
- Gari hizi zimeanza kufanya kazi nchini Marekani.
- Zimetengenezwa na kampuni ya usafirishaji ya Cruise.
- Zinatumia umeme na hazihitaji dereva.
Dar es Salaam. Kwa wanaotumia programu tumishi (apps) za usafiri kama Uber, Bolt na Linkee, wanafahamu kuwa kutumia huduma ya usafiri, unaingia kwenye app na kuweka jina la eneo unaloenda na kisha App itakuunganisha na dereva atakayekufuata ulipo na kukupeleka uendako.
Hata hivyo, teknolojia nayo imezidi kuendelea kwani huenda siku za usoni tusiwe na ulazima wa kuwa na dereva wa kutuendesha kwenye gari.
Hivi karibuni, kampuni ya usafirishaji wa abiria ya nchini Marekani inayotumia magari yasiyo na dereva, Cruise imeanza kufanyia majaribio magari yake ambayo yanasafirisha abiria bila kuwa na dereva.
Hivi ndivyo yanavyofanya kazi
Ukiwa na App ya Cruise kwenye simu yako, utaagiza usafiri kama unavyofanya kwenye Bolt na Uber.
Kwenye simu yako, utaona umbali wa gari na umefanyiwa mahesabu kwa dakika. Kadri gari inavyosogea, umbali nao utaendelea kupungua. Mfano, kama gari ipo umbali wa dakika tano, ikianza kuja kukufuata dakika zitakuwa zikipungua kutoka tano, nne, tatu, mbili na hadi gari kukufikia.
Baada ya gari kuwasili, utapokea arifa (notification) kwenye simu yako ya kutoa loki ya mlango wa gari. Ukibonyeza arifa hiyo, utaweza kufungua mlango wa gari na kuingia.
Gari hiyo inatumia akili bandia (artificial Intelligence) hivyo itakuambia kufunga mlango na kukupatia maelekezo mengine.
Baada ya hapo, gari itakupeleka hadi unapotaka kwenda kwa kujiendesha yenyewe.
Nini zaidi?
Kwa sasa gari za Cruise zinafanyiwa majaribio nchini Marekani kwenye mji wa San Franciso na zipo zaidi ya gari tano kwenye mji huo zikiwa zimepewa majina kama Scampi, Crepe, Disco, Tostada na Matcha.
Mpango wa Cruise ni kusogeza zaidi huduma hiyo kwenye miji mingine pamoja na nchi nyingine.
Gari hizo zinatumia nishati ya umeme ikiwa ni malenggo ya kupunguza matumizi ya pertoli na dizeli yanayozalisha hewa ya ukaa.
Iwapo barabarani, gari ya Cruise inatumia zaidi ya sensa 40 na hivyo kuweza kung’amua watumiaji wengine wa barabara ikiwemo watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.
Cruise inatumia sensa zinazofanya kazi kwa nyuzi 360 kuona mbali na kwa mawanda mapana.
Waliotumia magari hayo watoa ya moyoni
Baadhi ya wadau waliofanikiwa kufanya majaribio ya gari hizo ni mtengeneza maudhui, Karen X Cheng. Kwenye video yake aliyoiweka kwenye mtandao wa Instagram amesema, yeye binafsi hawezi kuendesha gari licha ya kuwa na leseni ya kuendesha gari.
Amesema hofu ya kuendesha gari imemkwamisha kwa namna mbalimbali na hiyo imekuwa sababu ya yeye kutegemea zaidi usafiri wa umma na wa kuchangia (ride share).
“Yamekuwa malengo yangu ya chini chini nisiendeshe gari tena na nimekuwa nikiisubiria siku ambayo magari yanayojiendesha yenyewe yatakuja. Nilipoona Cruise wameruhusu watu kutumia magari yao sikusubiri,” ameandika Cheng.
Utabiri wake ni kuwa, ifikapo miaka ambayo watoto wake wamekua, watu kuendesha magari itakuwa ni habari ya zamani na watu watakuwa wakishangaa kuwa zamani watu walikuwa wakiendesha magari.
Latest
