Utakayokutana nayo ukinunua simu mpya ya Motorola
- Ni simu inayogharimu takriban Sh2.3 milioni.
- Ni simu zenye camera, betri na skrini nzuri zinazoshindana simu kama Samsung na iPhone.
- Kama Samsung note 10 plus isingekuwepo, huenda Motorola angekuwa ni simu kubwa kuliko zote zilizopo sokoni.
Dar es Salaam. Ni kweli kampuni ya kutengeneza simu na vifaa vya kielektroniki ya Motorola imekuwa ikitengeneza simu nzuri ambazo zina ushindani mkubwa sokoni dhidi ya zile zenye majina makubwa kama iPhone, Samsung, Huawei na Oneplus.
Huenda mkito mkubwa wa ulimwengu wa simu janja kwa kampuni hiyo ulisikika baada ya kuzindua simu janja ya mkunjo ya Motorola Razr ya mwaka 2019 iliyozinduliwa ikiwa na gharama zaidi ya Sh3.4 milioni.
Muendelezo wa maajabu ya kampuni hiyo unaendelea baada ya kuitangaza simu yake mpya ya Motorola Edge Plus ambayo inajitambulisha kama simu yenye kasi ya 5G inayopiga kikumbo simu zingine zote zenye kutumia teknolojia hiyo.
Je yaliyomo yamo?
Motorola Edge Plus ambayo kwa muonekano inafanana na simu za toleo la edge za kampuni ya Samsung, inatarajiwa kuzinduliwa Mei 14, 2020 ikiwa ni kwa mujibu wa wadau wa teknolojia wa ZDnet.
Simu hiyo ambayo kwa mujibu wa mafundi wake itakuwa kubwa kuliko simu janja zilizopo sokoni na itachukua sifa hiyo kwani ukubwa wake ni inchi 6.7 ambao ni zaidi ya iphone 11 pro yenye ukubwa wa inchi 5.8, Samsung S10 plus yenye ukubwa wa inchi 6.4.
Hata hivyo, huenda Motorola walisahau ukubwa wa toleo la Oppo Reno ambayo ina ukubwa wa inch 6.7 mbali na Samsung note 10 plus yenye inchi 6.8.
Motorola Edge plus inaendeleza mashindano ya kamera za simu ikiwa na kamera tatu nyuma zenye muundo wa aina yake.
Kamera kubwa zaidi ina uwezo megapikseli 108 huku ikisemekana kung’amua hata kipele kilichojificha kwenye ngozi yako.
Kamera yake yenye upana wa “telephoto” inapiga picha kwa uwezo wa megapikselil nane ambayo bado haifui dafu kwa kamera ya Samsung Galaxy S20 Ultra 5G yenye megapikseli 48 na Samsung Note 10 plus yenye megapikseli 12.
Motorola inaungana na simu zingine zenye kupeperusha bendera ya ubora wa betri zikiwemo LG Thin Q, Samsung Galaxy S20 na One plus 8 pro ambazo zote betri yake ina uwezo wa 5,000mAh.
Kampuni hiyo imesema simu hiyo ikichajiwa ina uwezo kutumia kwa siku mbili mfululizo bila kujali matumizi yake.
Zinazohusiana
- Sifa za simu mpya ya Apple itakayozinduliwa Aprili 24
- Motorola Razr:Simu inayogharimu zaidi ya Sh3.4 milioni
Zaidi, mchuano baina ya simu za LG na Motorola kwenye ubora wa spika na sauti umefika kileleni baada ya Motorola kuamua kuweka alama yake kwenye Edge plus yake.
“Spika mbili zenye nguvu za mfumo wa sterio zinatoa sauti kubwa kuwahi kutokea kwa umaridhawa. Furahia bezi (bass) na voko safi hata ukiongeza sauti hadi mwisho,” imesomeka sehemu ya maelezo ya simu hiyo kwenye tovuti ya Motorola.
Simu hiyo inayotumia mfumo endeshi wa Android, inajidai kwa kuwa na kadi ya uhifadhi ya ndani (RAM) yenye ukubwa wa GB12 huku uhifadhi wa nje ya kumbukumbu ukiwa ni wa GB256.
Tofauti na simu za Apple na Samsung, simu hii haina madaraja yanayotofautishwa na uwezo wa uhifadhi kwani bei yake ni moja tu nayo ni Sh2.3 milioni bei ambayo bado haiifikia Motorola Razr 2019.
Uko tayari kutoboa mfuko wako kununua simu hii ili kufaidika na uzuri wake?
Latest