Utafiti: Nusu ya walimu wanatumia viboko, vitisho kuwaadhibu wanafunzi wa awali Tanzania
- Adhabu hizo hazipendekezwi kutumika kwa watoto wa shule awali.
- Hiyo inatokana na walimu kukosa mafunzo maalumu kwa ajili ya kufundisha madarasa ya awali.
- Wadau washauri Serikali kuongeza walimu wenye maadili na uelewa wa watoto hao.
Dar es Salaam. Ripoti mpya za taasisi ya HakiElimu zinaonyesha mwenendo mzuri wa elimu ya awali Tanzania kutokana na utekelezaji wa sera elimu bure huku zikibainisha kuwa nusu ya walimu katika ngazi hiyo wanatumia viboko na vitisho kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na nidhamu.
Ripoti hizo mbili za tafiti za “namna bora ya kujumuisha dhana ya ulinzi wa mtoto katika elimu ya awali” na “mazingira ya kujifunza na kufundishia ya elimu ya awali Tanzania kwa mwaka 2019” zimezinduliwa leo (Mei 28, 2020) na taasisi hiyo.
Matokeo ya tafiti hizo mbili yanaonyesha kuwa uandikishaji wa watoto kwenye madarasa ya awali umefanikiwa sana katika maeneo mbalimbali nchini.
Mathalani katika wilaya ambako tafiti zilifanyika ikiwemo ya Mvomero mkoani Morogoro, wastani wa uandikishaji ukilinganisha na matarajio ni zaidi ya asilimia 100 na hii inatokana na utekelezaji wa sera ya Serikali ya utoaji wa elimu bila malipo.
Hata hivyo, changamoto kubwa iliyopo ni walimu kutumia njia zisizofaa kuwajengea wanafunzi hao nidhamu hasa matumizi ya viboko.
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dk John Kalage akitoa muhtasari wa tafiti hizo amesema takribani asilimia 50 ya walimu walioshiriki katika tafiti hizo wanatoa adhabu kali kama za viboko na vitisho ili kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu.
“Lakini mbinu hizi hazipendekezwi kutumika kwa watoto wa shule awali,” amesema Dk Kalage.
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 909 darasa la saba
- Elimu bure yasababisha uandikishaji madarasa ya awali kushuka
Tafiti hizo zimebaini kuwa changamoto hiyo na nyingine za elimu ya awali kuwa walimu wanaofundisha madarasa hayo wana uelewa mdogo wa mbinu za kufundishia madarasa ya awali.
Mathalani, katika shule zote zilizohusika kwenye utafiti hakukuwa na walimu wenye mafunzo maalumu kwa ajili ya kufundisha madarasa ya awali.
“Hii inamaanisha kuwa katika shule hizo walimu waliokuwa wakifundisha madarasa ya awali hawakuwa na sifa stahili ya kufundisha madarasa hayo,” amesema Dk Kalage.
Pia takribani asilimia 52.6 ya walimu wa madarasa ya awali walioshiriki utafiti huu, hawana uelewa sahihi wa maana ya elimu ya awali na mahitaji yake.
Hali hiyo imesababisha ufundishaji na malezi ya watoto wa awali shuleni kufanana kwa kushabihiana na na ile ya watoto wa shule ya msingi ikiwemo walimu kutumia viboko kwa wanafunzi.
Tafiti hizo pia zimebaini changamoto ya ushirikiano mdogo kati ya wazazi/walezi na walimu katika kuhakikisha mtoto anapata malezi na elimu stahili vinavyoendana na umri na mahitaji yake.
“Ushirikiano hafifu kati ya wazazi na walezi umesababisha watoto kukosa mahitaji ya msingi kama lishe shuleni na kukumbwa na matukio ya unyanyasaji kutokana na ulinzi hafifu,” amesisitiza Dk Kalage.
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2008 na Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 zinatoa haki kwa kila mtoto kupata elimu bora ikiwemo elimu ya awali ambayo ni ya lazima.
Elimu ya awali ndiyo msingi wa watoto kujifunza katika ngazi zingine za elimu. Picha|HakiElimu.
Wadau wa elimu watoa suluhisho
Mmoja wa Watafiti wa tafiti hizo Dk Jacquiline Amani amesema kuna haja ya kuhamasisha na kuongeza mafunzo na ajira kwa walimu wa elimu ya awali ili kuziba pengo kubwa la mahitaji ya walimu lililopo.
“Elimu ya awali ni taaluma kama taaluma zingine. Isichukuliwe kiurahisi. Baadhi ya changamoto tulizoziona ni pamoja na weledi wa walimu katika kufundisha. Walimu wapewe mafunzo na kujengewa uwezo,” amesema Dk Amani.
Pia Serikali imeshauriwa kuwajengea uwezo walimu waliopo ili wawe na uelewa wa kutosha juu ya dhana ya elimu ya awali na mahitaji yake.
Mhadhiri kutoka Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Duce), Dk Maregesi Machumu amesema elimu ya awali ina umuhimu mkubwa kwa mtoto kwa sababu inamuandaa kimaadili na kimalezi kwa ajili ya ngazi zinazofuata hivyo uwekezaji wa mazingira mazuri ya kufundishia na kusomea.
“Shule zijenge mazingira mazuri ya kusomea ya kuwapokea wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum huku miundombinu ikiboreshwa kulingana na hali zao ili kuwawezesha kusoma vizuri,” amesema Dk Machumu.
Aidha, kuna haja pia ya kuhamasisha ushirikiano mkubwa zaidi baina ya wazazi na jamii pamoja na walimu ili kufanikisha makuzi na malezi ya watoto wakiwa shuleni.
“Kuna utashi wa wazazi kuwaachia malezi ya watoto wao watu wengine na hawako tayari kulipa. Tupanue uwezo wetu wa kuzungumzia malezi ya watoto wetu wanapokuwa nyumbani na shuleni,” amesema mchambuzi wa masuala ya elimu Jenerali Ulimwengu katika uzinduzi huo.
Hata hivyo, viongozi wa juu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) hawakupatikana mara moja kuzungumzia suala hili la elimu ya awali hasusan uchapaji wa viboko kwa watoto hao wadogo.