Usafirishaji mazao ya misitu ya kupandwa sasa kuwa usiku na mchana

April 2, 2019 8:08 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa utaratibu wa usafirishaji wa mazao hayo saa 24 ili kuchochea ukuaji wa uchumi. 
  • Serikali ilitunga sheria ya kuzuia mazao ya misitu namba 98 ya mwaka 2000 kutokana na uhaba wa watumishi na ugumu wa ukaguzi nyakati za usiku. 

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa utaratibu maalum kwa ajili ya kufungua mlango wa usafirishaji usiku na mchana mazao ya misitu ya kupandwa ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi. 

Kigwangalla aliyekuwa akitoa ufafanuzi wa usafirishaji wa mazao ya misitu leo (Aprili 2, 2019) bungeni amesema mtazamo wake ni kuona watu wanafanya kazi usiku na mchana katika maeneo mbalimbali ya shughuli za maendeleo.

“Suala hili tumeshaanza kulifanyia kazi hata kabla ya kupokea swali kutoka kwa Mhe Chumi (Mbunge wa Mafinga Mjini) na tuko katika hatua za mwisho mwisho kuweka utaratibu kwa ajili ya kufungua usafirishaji usiku wa mbao za kupandwa,” amesema Kigwangalla.

Amesema yeye siyo muumini wa kuzuia watu wasifanyaje kazi usiku ikizingatiwa kuwa mabasi na malori hayasafiri usiku na mbao hazisafiri usiku, jambo linachelewesha ukuaji wa uchumi. 

Kutokana na hali hiyo, tayari amewaagiza wataalam wa wizara kutoa ushauri wa namna utaratibu huo utakavyotekelezwa ili kudhibiti uhalifu na watu waruhusiwe kusafirisha mazao ya misitu nyakati za usiku. 

“Kwa hivyo mtazamo wangu ili kutia chachu ya ukuaji wa uchumi watu lazima wafanye kazi mchana na usiku na ndiyo maana nimetoa agizo ndani ya wizara kwamba walete ushauri wa kitaalam wa namna ambavyo tunaweka controls (vizuizi) ili kudhibiti uhalifu na mambo mengine lakini watu waruhusiwe kusafirisha mazao yao usiku,” amesema. 

Ufafanuzi huo ulitokana na swali la Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi aliyetaka kujua kama Serikali iko tayari kubadilisha sheria na kanuni ili kuruhusu usafirishaji wa mazao ya misitu usiku na mchana yaani saa 24. 


Zinazohusiana: 


Awali akitoa maelezo ya mchakato wa usafirishaji wa mazao ya misitu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema utaratibu unaondaliwa utahusu vibali maalum vitakavyotolewa kwa watu kusafirisha mazao hayo ya kupandwa ikiwemo milunda na siyo mazao pori ili kulinda maliasili.

“Hivyo wizara itaanza kutoa vibali maalum kwa wasafirishaji wa mazao ya misitu ya kupandwa kusafirishwa kwa masaa 24,” amesema Kanyasu. 

Akitolea mfano wa vibali hivyo, Mwaka 2018 kupitia tangazo la Serikali 478, Serikali imetoa kibali cha kusafirisha usiku nguzo za umeme kwa saa 24 ili kuharakisha usambazaji wa umeme vijijini.

Mbao ni miongoni mwa mazao ya misitu ya kupandwa ambazo hutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi. Picha| Mtandao.

Kanyasu amesema kutokana na ugumu wa ukaguzi nyakati za usiku, Serikali ilitunga sheria ya kuzuia mazao ya misitu nyakati za usiku. Sababu nyingine iliyopelekea kuzuia usafirishaji wa mazao ya misitu nyakati za usiku ni pamoja na uhaba wa watumishi, udangajifu na ubadhirifu, hali ambayo hivi sasa imeshughulikiwa. 

“Sheria ya kuzuia mazao ya misitu namba 98 ya mwaka 2000 iliwekwa kutokana na changamoto za usafirishaji haramu wa mazao ya misitu ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni vigumu kudhibiti uhalifu huo nyakati za usiku,” amesema Kanyasu. 

Ukaguzi wa kina wa mazao ya misitu hufanyika katika kituo cha mwanzo wa safari na vituo vya ukaguzi vilivyoko barabarani kwa kukagua nyaraka mbalimbali ikiwemo kibali cha usafirishaji na kuangalia aina ya mazao, jamii ya miti na kiasi kinachosafirishwa.

Hatua kama hiyo imeanza kuchukuliwa na mkoa wa Dar es Salaam kwa kufunga taa na kamera za usalama ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao usiku na mchana ili kuongeza mapato ya kodi na ukuaji wa uchumi. 

Enable Notifications OK No thanks