Uongozi, mashabiki Simba washtushwa kutekwa Mo Dewji

October 11, 2018 5:30 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema uongozi na mashabiki wa timu hiyo wamehudhunishwa na tukio la kutekwa  kwa bilionea huyo.
  • Timu hiyo na familia wameamua kuwa suala la kutekwa kwa mwekezaji wao sasa litazungumzwa na vyombo vya dola pekee.
  • Ni tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia tajiri mdogo zaidi Afrika ambaye ana utajiri unafikia Dola za Marekani 1.5 bilioni. 

Dar es Salaam. Msemaji wa Klabu ya mpira wa miguu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa uongozi na mashabiki wa timu hiyo wameshtuka na kuhudhunishwa na tukio la kutekwa kwa bilionea Mo Dewji na kwamba hadi sasa bado hajapatikana.

Manara amewaambia wanahabari leo kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo na familia wameamua kuwa suala la kutekwa kwa mwekezaji wao sasa litazungumzwa na vyombo vya dola pekee.

“Vyombo vya dola pekee hususan polisi ndiyo watakaotoa taarifa zote zinazohusu tukio hilo la Mo,” amesema.

Manara, aliyefika katika hoteli ya Collesseum alipotekewa Mo kuzungumza na wanahabari, amesema uongozi wa Simba na familia wanawaomba mashabiki na Watanzania kufanya dua ili mfanyabiashara huyo apatikane akiwa hai na salama na watekaji watiwe mbaroni.

“Hadi sasa bado hajapatikana na taarifa kuwa kapatikana Coco Beach ni uzushi mtupu. Kama kuna mtu ana taarifa za kupatikana kwake awasiliane na polisi na siyo kuzusha kwenye mtandao,” amesema.

Manara amesema Mo alikuwa kwenye kikao Cha Bodi ya Wakurugenzi hadi jana usiku akiwa mwenye furaha hivyo taarifa za kutekwa kwake zimewashtua.


Zinazohusiana: 


Jarida maarufu la masuala ya fedha na utajiri duniani la Forbes, linamtaja Mo mwenye umri wa miaka 43 kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia tajiri mdogo zaidi Afrika ambaye ana utajiri unafikia Dola za Marekani 1.5 bilioni (zaidi ya Sh3.42 trilioni)

Mbali ya kuwa mfanyabiashara maarufu Afrika, amewahi kuwa mbunge wa Singida Mjini kwa miaka 10 hadi alipoamua kuachana na siasa za uwakilishi mwaka 2015.

Mo pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira wa miguu ya Simba ambapo anamiliki asilimia 49 ya hisa za timu hiyo. 

Uwekezaji wa Mo katika klabu ya Simba umechangia mabadiliko mbalimbali ya kiutendaji na uchumi wa timu hiyo ambapo imefanikiwa kuwa katika orodha ya klabu bora Afrika huku ikitoa ushindani mkali kwa timu za Ligi Kuu Bara.

Kwa mujibu wa gazeti la michezo la Mwanaspoti, uwekezaji wa Dewji umesaidia motisha na bajeti ya mishahara ya Simba kupanda mara mbili zaidi ya iliyokuwepo hapo awali 

Bajeti ya mishahara kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza na vijana, benchi la ufundi pamoja na watumishi wa timu hiyo ilikuwa inakadiriwa kuwa Sh120 milioni kwa mwezi. Hata hivyo, kwa sasa bajeti ya mishahara ya Simba ni inafikia Sh250 milioni kwa mwezi, ambapo kwa mwaka ni takribani Sh3 bilioni.

Mafanikio ya Mo ndani ya Simba yameonekana pia katika usimamiaji wa tamasha la klabu hiyo la Simba Day mwaka huu, ambapo lilisheheni mambo mengi ambayo yaliwavutia mashabiki wa timu hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini. 

Enable Notifications OK No thanks