Ununuzi, uvaaji wa nguo uliopitiliza wachangia athari mabadiliko ya tabianchi

December 23, 2021 2:21 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Unachangia kuongeza uzalishaji viwandani na hewa ukaa.
  • Watu washauriwa kupunguza manunuzi ya nguo yaliyopitiliza.
  • Pia sekta ya mavazi yashauriwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.
  • Sekta hiyo inatoa asilimia kati ya 2 hadi 8 ya hewa chafuzi duniani.

Dar es Salaam. Wakati viongozi wa duniani wakiendelea kuumiza vichwa kutafuta suluhu ya kudumu ya athari za mabadiliko ya tabianchi, sekta ya ubunifu wa mitindo ya mavazi imetangaza kutoa elimu kwa wazalishaji na wavaaji  ili kupunguza matumizi ya nguo yaliyopitiliza kuokoa tabianchi. 

Huenda hatua hiyo ikasaidia kupunguza uzalishaji na ununuzi wa nguo kupitiliza ambao unachangia katika madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira Duniani (UNEP), sekta ya mitindo ya mavazi ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika janga la tabianchi na ekolojia na linatoa asilimia kati ya 2 hadi 8 ya hewa chafuzi.

Kampuni 160 zimekubali kubadili mbinu ya mawasiliano kuanzia kwa wazalishaji hadi wavaaji ili kwenda sambamba na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Hatua hiyo imefikiwa Novemba 8, 2021 baada ya mashauriano yaliyoitishwa na Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) yaliyofanyika katika  mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi (COP26) huko Glasgow, Scotland.

Pia makubaliano hayo yanazingatia ahadi kuu iliyotolewa na sekta ya mitindo ya mavazi kupitia chata ya sekta ya mitindo ya mavazi kwa hatua dhidi ya tabianchi  ya mwaka 2018 ambayo imefanyiwa  marekabisho.

Baadhi ya makubaliano hayo ni kutoa elimu kwa watu kupunguza matumizi ya nguo yaliyopitiliza na kuzivaa walizonazo mara kwa mara kabla ya kununua nyingine. 

Hatua hiyo itaenda sambamba na wazalishaji kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira na kupunguza utoaji wa hewa ukaa. 

Sekta ya mitindo ya mavazi ikitumiwa vizuri inaweza kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Picha| Monchi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mitindo ya mavazi ya Futerra, Lucy Shea amesema nyanja ya mitindo ya mavazi ni moja ya sekta ambazo zina nguvu sana katika matangazo ya biashara na kusaka masoko, jambo linalochangia kuchochea mabadiliko tabianchi.

“Kama wapasha habari kutoka kona zote za sekta hii, tunapaswa kuwa pamoja na kutumia nguvu yetu kwa uwajibikaji zaidi ili kushawishi mabadiliko ya mienendo na tabia ambazo ni muhimu kushughulikia janga la sasa la kibinadamu la tabianchi. 

“Hii ni fursa ya sekta ya mitindo ya mavazi kuwa sehemu ya jawabu, kutumia uwezo wake wa matangazo kuumba maadili mapya na matarajio mapya,” amsisitiza Shea.

Uzalishaji wa nguo umeongezeka maradufu katika miaka ya 15 ya mwanzo ya karne ya 21 huku kiwango cha urudiaji wa nguo kabla ya kutupwa kimepungua kwa asilimia 36, imeeleza UNEP.

Utafiti uliofanywa kwa niaba ya UNEP juu ya mzunguko wa nguo moja umeonesha kuwa kiwango kidogo cha urudiaji wa nguo kimechangia asilimia 24 ya hewa chafuzi kutoka sekta hiyo ya nguo na kwamba kuongeza muda wa kuvaa nguo kabla ya kuitupa kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafuzi.

Hiyo inamaanisha kuwa uzalishaji utapungua kwa kuwa mahitaij ya nguo mpya yatapungua, vivyo hivyo uzalishaji.

UNEP inasema iwapo mwelekeo wa sasa wa uzalishaji na uvaaji wa nguo utaendelea, kuna uwezekano mkubwa wa kutofikia lengo la kupunguza utoaji wa hewa chafuzi katika sekta hiyo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

“Kushughulikia suala la matumizi au uvaaji wa nguo ni sehemu kuu ya kupunguza athari za tabianchi kuanzia kiwango cha bidhaa mpya za nguo zinazonunuliwa hadi kiwango cha hewa ya ukaa inayozalishwa sambamba na jinsi ya kutumia bidhaa hizo. 

“Lazima tushirikiane kuwapanga wadau wote pamoja wa sekta hii ya mitindo ya mavazi ili kufikia lengo la kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi kwa mujibu wa mkataba wa Paris,” amesema Steven Stone, Naibu Mkurugenzi idara ya Uchumi UNEP.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW