Unesco: Ukosefu wa kanuni za usimamizi chanzo cha uongo kuaminika mitandaoni

February 25, 2023 11:44 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay akifungua mkutano kuhusu Intaneti kwa Kuaminiana huko Paris Ufaransa. Picha | 

UNESCO/Christelle ALIX.


  • Yasema uongo unasambaa kwa kasi kuliko ukweli.

  • Yaandaa kanuni na mwongozo wa kimataifa kusimamia suala hilo. 

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) Audrey Azoulay amesema kuzidi kushamiri kwa mpaka kati ya ukweli na uongo na kukataliwa kwa taarifa za ukweli za kisayansi kumechangiwa na kukosekana kwa kanuni za udhibiti na usimamizi.

Azoulay aliyekuwa akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu intaneti kwa ajili ya kuaminiana Ufaransa jana Februari 24, 2022 amesema ni kwa kuchukua hatua madhubuti ndiyo inawezekana kutoa hakikisho kwamba maendeleo ya teknolojia hayakwamishi haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na demokrasia.

Bosi huyo amesema habari zinasalia kuwa bidhaa ya umma na ibakie hivyo na ni lazima kufanya kazi kwa pamoja kufanikisha.

Mkutano huu unakuwa ndiyo mashauriano ya ngazi ya juu zaidi yaliyozinduliwa na Unesco kusongesha miongozo ya mwanzo kabisa ya kanuni za mitandao ya kijamii ili kuboresha kuaminika kwa taarifa na haki za binadamu mitandaoni.

Wadau ni pamoja na serikali, wasimamiaji huru wa kanuni, kampuni za kidijitali, wanazuoni na mashirika ya kiraia ambapo miongozo hiyo inatarajiwa kuzinduliwa na Unesco Septemba 2023.

“Uongo unasambaa kwa kasi kubwa kuliko ukweli. Na kwa sababu fulani maelezo ya ukweli hayana mvuto,” amesema Maria Ressa, mwandishi wa habari na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kutoka Ufilipino.

Amesema kuw uongo hasa ule uliochanganywa na hofu, hasira, chuki na ukabila ukichagiza ‘Sisi dhidi ya Wao’ unasambaa kwa kasi duniani.

“Ni sawa kutupa njiti ya kibiriti iwakayo kwenye kuni,” amesema Ressa.

Amesisitiza kuwa iwapo dunia itaendelea kuvumilia mienendo ya mitandao ya kijamii inayozawadia watu uongo, basi vizazi vijavyo vitarithi dunia ambamo ukweli hautakuwa na thamani kwani bila ukweli hakuna kuaminiana na bila kuaminiana hakuna uhalisia wa pamoja.


Zinazohusiana:


Washiriki walipata ujumbe wa video kutoka kwa Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil ambaye alitumia fursa hiyo kukumbushia mashambulizi ya hatari dhidi ya taasisi za kidemokrasia nchini mwake Januari 8 mwaka huu.

“Kilichotokea siku ile ni hitimisho la kampeni ya siku nyingi iliyotumia uongo na taarifa za uongo kama silaha. Kwa kiasi kikubwa kampeni hii inalelewa, inapangwa na kusambazwa kupitia majukwaa ya kidijitali na apu za kutuma ujumbe mfupi. Hii ndiyo mbinu inayotumika kuchochea matendo ya ghasia duniani kote, lazima ikome,” amesema Rais Lula da Silva.

Maandalizi ya kanuni hizo

Mkurugenzi Mkuu wa Unesco ameeleza hatua za maandalizi ya kanuni hizo akisema takribani nchi 55 zinaandaa lakini lazima zizingatie mwelekeo wa kimataifa na haki za binadamu.

“Iwapo hatua hizo zinaandaliwa na kila nchi kivyake, kila nchi ikiwa imejitenga kuna hatari ya kushindwa. Uvurugaji wa taarifa ni tatizo pekee kwa hiyo tafakuri zetu zifanyike katika ngazi ya kimataifa,” amesisitiza bosi huyo na kuongeza kuwa,

“Ni muhimu kuwa na mtazamo wa mwongozo wa pamoja ya jinsi ya kusimamia nyanja ya dijitali. Teknolojia haiwezi kutumiwa vibaya kukandamiza watu, kuwanyanyasa au kufunga mtandao wa intaneti.”

Bi. Azoulay amesihi nchi zote kuungana na juhudi za Unesco kufanyia marekebisho mtandao wa intaneti ili uwe ni mbinu halisi ya huduma kwa umma ikisaidia kuweka hakikisho la uhuru wa kujieleza; haki ambayo inajumuisha haki ya kusaka na kupata taarifa.

Washiriki wa mkutano huo ni 4,300 na ni wa kwanza kufanyika kimataifa.

Enable Notifications OK No thanks