Unayotakiwa kuzingatia unapotumia ‘apps’ za bajeti mtandaoni
- Unatakiwa kuwa makini wakati wa kuweka taarifa zako hasa za benki kwenye programu hizo.
- Taarifa zako zitaonekana kwa mtu aliyetengeneza au anayesimamia programu husika.
- Hata hivyo, ni programu muhimu kukusaidia kutumia vizuri fedha zako.
Dar es Salaam. Maendeleo ya teknolojia yanaendelea kusambaa katika sekta mbalimbali ili kuboresha maisha na kuifanya dunia kuwa sehemu muhimu ya kuishi.
Kati ya teknolojia ambazo zimetengenezwa kurahisisha maisha ya watu ni pamoja na programu tumishi (Apps) za kupanga bajeti binafsi au taasisi kwa ajili ya matumizi sahihi ya mapato na kufikia malengo husika.
Kama wewe siyo mdau wa programu hizo, basi unaweza kutembelea duka la programu linalohusiana na simu janja yako na kuangalia programu kama “track money” ambayo inaangazia mlolongo wa matumizi ya fedha, “Money Manager”, “Wallet” na “Buxget”.
Licha ya apps hizo kurahisisha utendaji kazi na upangaji bajeti, bado mapokezi ya teknolojia yanatofautiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine. Baadhi ya watu wanahofia usalama wa taarifa zao wanapotumia teknolojia.
Je apps za bajeti binafsi ni salama kuzitumia? Ni mambo gani ya msingi unatakiwa kuzingatia kabla ya kutumia?
Mtaalam wa programu za kompyuta, Emmanuel Evance ambaye anatumia programu ya “Wallet”, amesema programu hiyo inamsaidia kumkumbusha vitu anavyotakiwa kulipia pamoja na matumizi yake binafsi.
Evance amesema kupitia “wallet” anaweza kuweka jumla ya mapato yake, na kuweka vipaumbele vya matumizi na programu hiyo itamkumbusha endapo atasahau.
“Unaweza ukaweka mapato yako na kuweka vipaumbele vyako kama bili na matumizi unayotarajia kuyafanya. Programu hiyo itakukumbusha na kukueleza pale utapozidisha matumizi hayo ama kukawia kulipa bili zako” amesema Evance.
Pamoja na hayo, baadhi ya programu zinamtaka mtu kuweka taarifa zake za benki. Jambo ambalo linazua utata juu ya usalama wa taarifa hizo hasa ikizingatiwa kuwa hujui ni nani anayeshikilia taarifa zako.
Evance amesema, yeye anatumia mfumo wa programu hiyo ambao haujalipiwa hivyo, “uwezo” wa kuweka taarifa za benki hawezi kuitumia kwani upo kwenye mfumo uliolipiwa ambao uko salama zaidi.
Unaweza ukaweka mapato yako na kuweka vipaumbele vyako kama bili na matumizi unayotarajia kuyafanya. Picha| Mtandao.
Amesema mtumiaji anatakiwa kuzitumia programu hizo za bajeti kama anavyotumia mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram kwa sababu taarifa zozote unazoziweka zinaonekana na kampuni au mtu aliyetengeneza programu hiyo.
“Taarifa yoyote unayoweka kwenye hizo apps ujue pia zinaonekana na kampuni husika. Hakuna tahadhari yoyote ya kiusalama lakini taarifa zako zinaonekana, usifikiri unazo peke yako,” amesema.
Hata hivyo, wakati wengine wakikubaliana na mwenendo wa teknolojia, bado wapo vijana ambao wanapendelea mifumo ya zamani ya kupangilia bajeti zao kwa kutumia akili.
Mdau kutoka kampuni inayohusika na kuunganisha wafanyakazi na sehemu za kufanyia kazi ya Worknasi, Edgar Mwampinge amesema yeye hana mambo mengi na hivyo hahitaji kutumia programu kumkumbusha wajibu wake wa kuwa na matumizi sahihi ya kipato anachopata.
“Pesa zangu zote najua nazifanyia nini. Iwe ni kulipa kodi ama hata kulipia gharama za umeme na maji. Ninajua ni lini zinahitajika na wapi nazipata,” amesema.
Zinazohusiana
- Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Zaidi Mwampinge amesema huenda ni kweli programu hizo zina umuhimu lakini kwa yeye bado hajawa na mambo mengi kiasi cha kuhitaji kukumbushwa.
Naye Peter Mashauri, mfanyabiashara mwenye wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, amesema ana kawaida ya kupanga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha hatumii pesa vibaya, jambo ambalo linaweza kusababisha biashara yake kutetereka.
“Bila bajeti unaweza ukajikuta umekula hata pesa ya mtaji. Inatakiwa nipange kama ninepata Sh1 milioni moja, Sh10,000i inaenda wapi na buku (1,000) inaenda wapi,” amesema Mashauri.
Umuhimu wa jambo hilo (bajeti) huenda ndiyo chachu ya wanasayansi na wadau wa teknolojia kuunda programu hizo ambazo zinapatikana kwenye maduka ya mtandaoni ya programu ya kiwemo Play store na App store.