Unavyoweza kuitumia simu yako kama rimoti
- Ni teknolojia ya “infrared” inayofanya kazi na baadhi ya simu.
- Husaidia kubadilisha chaneli za televisheni, viyoyozi na redio.
- Inatumika katika simu za Android.
Dar es Salaam. Kuyaelewa mawanda ya matumizi ya simu janja huenda ikachukua miongo na miongo. Wakati wengine wanazitumia kwa ajili ya mawasiliano, picha, burudani na uhifadhi, matumizi ya simu janja yanazidi kuwa mapana kila kukicha.
Kutoka kifaa cha mawasiliano ya mkononi, skrini ya kutazamia filamu na spika za kusikiliza redio, baadhi ya simu janja pia zina uwezo wa kufanya kazi ya rimoti kwa ajili ya vifaa vyako vya kielektroniki.
Huenda usione haja ya kugombania rimoti au usitaabike kutafuta rimoti ya televisheni pale mtoto anapoificha na badala yake, simu yako ikakusaidia kubadilisha chaneli za televisheni.
Haiishii kwenye televisheni tu. Inaenda kwenye ving’amuzi, viyoyozi, redio na vifaa vinavyotumia teknolojia ya mawimbi ya “Infrared (IR)”.
Teknolojia ya IR huambatana na baadhi ya simu zinazotumia mfumo endeshi wa Android ambapo sehemu yenye mfumo huo huwa kwenye eneo la juu la simu.
Kwa baadhi ya simu, IR huwa kwenye sehemu ya nyuma karibu na kamera. Picha| Dignited.
Licha ya kuwa baadhi ya kampuni ikiwemo Samsung imeachana na teknolojia hiyo, bado kampuni za kutengeneza simu hasa za nchini China zimeendelea na teknolojia ya IR.
Tovuti ya masuala ya simu, Android Authority, imezitaja baadhi ya simu ambazo kwa mwaka 2021, ndiyo zimeshikilia teknolojia ya IR kwa ueledi zaidi.
Simu hizo ni pamoja na Vivo X70 Pro Plus, Huawei P40 Pro na P40 Pro Plus, Poco F3 na F3 GT, Xiaomi Mi 11, Xiaomi 11T na Poco X3 Pro pamoja na X3 GT.
Simu nyingine ni Redmi Note 10 na 10 Pro na Poco M3.
Unaweza kutumia rimotihiyo kwenye televisheni, viyoyozi na king’amuzi. Picha| Droid Life.
Utajuaje kama simu yako ina uwezo wa kufanya kazi ya rimoti?
Simu ambazo zinaweza kufanya kazi kama rimoti ni zile zilizotengenezwa na teknolojia ya IR lakini zipo ambazo huuzwa tofauti na simu ambazo zinaweza kuchomekwa kwenye sehemu ya kuchajia simu au sehemu ya kuchomekea “earphones” na kufanya kazi kama rimoti.
Kwa simu ambazo zina IR, nyingi huwa na “app” ya rimoti inayoambatana na simu. Lakini baadhi hazina app hiyo hivyo, endapo utaona sehemu ya IR kwenye sehemu ya juu ya simu yako, unaweza kupakua app ya “universal remotecontrol” kutoka duka la app, Play Store.
Kwa watumiaji wa simu zinazotumia mfumo endeshi wa IOS, kampuni hiyo haijaweka teknolojia ya IR katika simu zake hivyo huenda suluhu iliyopo ni kununua IR kivyake na kisha kufurahia rimoti yako.
Latest



