UN: Nusu ya watu duniani watakuwa katika hatari ya mafuriko, vimbunga ifikapo 2030
Mwanamke akiangalia kijiji chake nchini Indonesia kilichoharikiwa na tsunami mwaka 2004. Picha|OCHA/Anthony Burke.
- Inakadiriwa kuwa asilimia 50 ya watu wote duniani katika maeneo hayo.
- Ni kutokana kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi.
- UN yahimiza ushirikiano na ufadhili kukabiliana na majanga hayo.
Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umeonya kuwa kufikia mwaka wa 2030, inakadiriwa kuwa asilimia 50 ya watu wote duniani wataishi katika maeneo ya pwani ambayo yanakabiliwa na mafuriko, vimbunga na tsunami.
Onyo hilo linakuja wakati mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi ukiendelea Glasgow, Scotland ambao wadau na viongozi wa serikali wanatafuta suluhu ya tatizo hilo.
Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi zote, mashirika ya kimataifa, na mashirika ya kiraia, kuongeza uelewa wa tishio hilo hatari, na kubadilishana mbinu za ubunifu za kupunguza hatari zake.
“Tunaweza kuendeleza hatua zilizofikiwa kuanzia kwa elimu bora hadi kwa jamii zilizoathiriwa na tsunami kote ulimwenguni, hadi kujumuishwa kwa mpango wa Tsunami katika muongo wa Umoja wa Mataifa wa sayansi ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu,” amesema Guterres katika maadhimisho ya siku ya tsunami duniani Novemba 5, 2021.
Kwa mantiki hiyo amesema ni “lazima tupunguze ongezeko la joto duniani hadi kusalia katika nyuzi joto 1.5 juu ya wastani wa kabla ya mapinduzi ya viwanda na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kujenga mnepo wa jamii za pwani.”
Katika ujumbe wake umeongeza kuwa ukuaji wa haraka wa miji na utalii unaokua katika maeneo yanayokumbwa na Tsunami, pia unawaweka watu wengi zaidi katika hatari.
Guterres amesema sayansi, ushirikiano wa kimataifa, kujitayarisha na hatua za mapema lazima ziwe kiini cha juhudi zote za kuweka watu na jamii salama zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko.
“Kuongeza msaada kwa nchi zinazoendelea na kuboresha utambuzi na mfumo wa tahadhari za mapema ni muhimu. Katika kukabiliana na kuongezeka kwa migogoro migumu ya kimataifa, tunahitaji kujiandaa vyema,” amesisitiza.
Uharibifu nchini Japan baada ya Tsunami. Picha| Ewerthon Tobace.
Tsunami ni matukio ya nadra lakini yanaweza kuangamiza kwa kiasi kikubwa. Katika miaka 100 iliyopita, matukio 58 yamekatili maisha ya watu zaidi ya 260,000, au wastani wa watu 4,600 kwa kila janga idadi ikiwa ni zaidi ya majanga mengine yoyote hatari ya asili.
Idadi kubwa zaidi ya vifo ilitokea katika tsunami ya bahari ya Hindi ya Desemba 2004, ambayo ilisababisha vifo vya takriban watu 227,000 katika nchi 14 huku Indonesia, Sri Lanka, India na Thailand ndizo zilizoathirika zaidi.
Wiki tatu tu baada ya maafa, jumuiya ya kimataifa ilikutana Kobe, Japan, na kupitisha mfumo wa utekelezaji wa miaka 10 wa Hyogo, ambao ni makubaliano ya kwanza ya kina ya kimataifa kuhusu kupunguza hatari ya maafa.
Pia waliunda mkakati wa tahadhari na kupunguza tsunami katika bahari ya Hindi, ambao unatumia vituo vya ufuatiliaji wa hali ya hewa na usawa wa kina cha bahari ili kutuma taarifa kwa vituo vya kitaifa vya taarifa kuhusu tsunami.
Baada ya mfumo wa utekelezaji wa Hyogo kumalizika, mwaka 2014, ulimwengu ulipitisha mkakati wa Sendai wa kupunguza hatari za majanga wa mwaka 2015-2030, ukielezea malengo saba ya wazi na vipaumbele vinne vya kuzuia na kupunguza hatari za majanga.
Latest
