Umuhimu wa kuwa mkweli kwa mwenzi wako

November 13, 2021 9:05 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukweli utakuepusha na mifarakano.
  • Pia utaepuka madeni na kumwacha mpenzi wako katika hali ya mawazo.
  • Inashauriwa kuwa makini na mtu ambaye unaamua kufunguka kwake.

Dar es Salaam. Kama ni mawe, wanaume tumetupiwa sana. Baadhi ya wanawake hutushutumu kutokuwa na uwazi kwenye mahusiano. 

“Meme” za mtandaoni huko zinatuonyesha wanaume kama viumbe walaghai tusio na ukweli hata punje. 

Hata hivyo, huenda ni vile wanaume hatuna sifa ya uongeaji sana lakini huenda hata sisi tumekutana na wanawake ambao hawakuwa wawazi kwetu lakini tukafunika kombe.

Uongo unaweza kuharibu “chaka” zuri

Vipi? Haujaelewa maana ya chaka? Alikiba kwenye wimbo wake wa “Utu” ameimba kuwa “niliforce kujificha kule kumbe chaka langu ni hapa sasa napewa amani mapenzi yasiyo na mipaka.” 

Baada ya kuelewa maana ya chaka, tuendelee. 

Katika mahusiano, watu hushindwa kuwa wawazi kwa sababu mbalimbali. Gazeti la afya ya wanawake la Women’s Health limetaja baadhi ya sababu kuwa ni kiburi, kumuepusha umpendaye na maumivu na kuepusha ugomvi.

Hata hivyo, tovuti hiyo imeeleza, iwe kwa sababu yotote ile mtu akaamua kumdanganya mwenziwe, ipo siku itasababisha  mahusiano hayo kuharibika.

Waswahili wa kale hawakuwa mbumbumbu kusema “ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga”.

Ukweli utakuweka huru. Picha| Huffpost.

Umuhimu wa uwazi katika mahusiano

Sitaki kuamini ya kuwa kuna mtu ambaye anapenda kuongopewa. Hata wewe unayeongopa leo, ikifika siku ukajua kuwa umeongopewa tena na umpendaye, bila shaka hautofurahia.

Katika mahusiano, uwazi unaweza kuyajenga na hata kuyabomoa mahusiano yenu. Hivyo kwa kila chaguo unalolifanya, fikiria kama upo tayari kuwa na mtu kwa sababu ya uongo uliomwambia au kumpa mtu uhuru wa kuchagua kubaki baada ya kuwa mkweli.

Uwazi humpunguzia mwenzi wako “stress”

Licha ya sababu yako ya kudanganya, kwa mtu ambaye anakufahamu vizuri, lazima atabaki na wasi wasi. Mbali na kujiuliza mwaswali ya kuwa “kwanini amenidanganya”, mwenzi wako anaweza kubaki na maulizo ya kuumiza kichwa.

Kusema ukweli, kutathibitisha dhamira yako juu yake na hata kama akiumia, atakuheshimu kwa kumwambia ukweli.

Fahamu kuwa, wakati mwingine mwenzi wako anaweza kuwa anakuuliza kitu kukutega tu huku ukweli wote tayari anao.


Soma zaidi


Unajenga mawasiliano yenye afya

Kusema ukweli kwenye mahusiano yako kutajenga mawasiliano mazuri baina yako na mwenzio.

Tovuti ya masuala ya ndoa, Marriage.com inaeleza kuwa ukweli utafanya urahisi kwenye kutatua ugomvi baina yako na mwenzi wako na pia tabia ya kuwa muwazi inajenga ukaribu baina yako na mwenzi wako.

Ukweli unajenga heshima

Umewahi kuona filamu na binti akisema “He would never do that” baada ya kupewa umbea kuhusu mpenziwe?

Hicho ni kiashiria cha heshima ambayo mpenzi wako anaweza kuwa nayo juu yako. Heshima hiyo inajengwa na imani yake juu yako na kumwagiliwa na ukosefu wa mashaka juu yako kwani anakuwa anakuamini.

Inaweza isiishie kwenye filamu na ikawe kwenye maisha yako.

Wapowanaodanganya kuhusu wao ili wapate anachokitaka kutoka kwako. Picha| SheKnows.

Kukubalika kwa jinsi ulivyo

Kwa wale waliotongoza wapenzi wako wakijimwambafai kama watu wenye pesa wanaweza kuelewa wapi ninaelekea.

Unapokuwa muwazi juu ya hali ya uchumi wako, maisha yako mtu kama akichagua kukupenda, atakupenda kama ulivyo. 

Niliwahi kukaa na mwanamama mmoja ambaye ni mke wa ndugu yangu na alikuwa akiniambia, “yaani mimi ndugu yako hata akiniambia mke wangu leo sina hela, ninamuamini. Tutapika mboga za majani tule. Ni kwa sababu tangu mwanzo aliniambia hali yake,” 

Kukosa uwazi hasa katika masuala ya uchumi wako, kutakuongezea msongo wa mawazo na hata kukubakisha na madeni kwa rafiki na jamaa zako.

Kwanini ufike huko?

Hata hivyo, maelezo hayo hayamaanishi uwe kitabu kilicho wazi kwamba kila mtu anaweza kukusoma.

Katika dunia ambayo pesa imekuwa kipaumbele katika mahusiano, huenda ukadhibiti kujianika kwani inaweza kukuletea fedheha endapo utamfungukia mtu ambaye siyo sahihi.

Unapoamua kuwa muwazi, hakikisha unakuwa muwazi kwa mtu ambaye moyo wako una amani naye.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW