Umemejua wapunguza maumivu kwa wafanyabiashara Morogoro
- Sasa biashara zinafanyika saa 24, tofauti na awali.
- Umeimarisha usalama, na kuongeza idadi ya wafanyabiashara sokoni hapo.
Morogoro. Licha ya kuwa ni Saa 1.39 usiku, biashara katika soko la Nguzo Mbili lililopo pembezoni mwa barabara kuu ya Morogoro-Dodoma zinaendelea kama kawaida kama ilivyo mchana.
Katika soko hilo lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, kuna wanaouza vyakula kama ndizi, viazi, mahindi mabichi, mboga mboga, matunda, na mama lishe. Ng’ambo ya pili ya barabara vijana wanaofanya shughuli za ukuli wanaendelea kupakia mizigo kwenye malori yaliyoegesha kando ya barabara.
Iwapo ungepita hapa miaka mitatu iliyopita yaani kuanzia 2020 kurudi nyuma huenda ungekutana na hali ya tofauti kidogo, sehemu kubwa ya wafanyabiashara wangekuwa wameshafunga shughuli zao au la ungekuta wachache kati yao wakiwa wanajiandaa kufunga.
Hali hiyo ilichangiwa zaidi na giza lililokuwa linatawala mahali hapo kutokana na kukosekana kwa nishati ya mwanga.
Tochi za simu au taa za kuchaji mara kadhaa hazikufua dafu, kwa mujibu wa wenyeji wa eneo hilo na hivyo kuwalazimisha wafanyabiashara hao kufunga shughuli zao mapema.
Kukwepa vihatarishi, kwao ilikuwa ni afadhali kukosa wateja wa usiku kuliko kuuza na kisha kupoteza fedha kwa kuibiwa na wezi waliokuwa wanahifadhiwa na giza lililokuwepo.
Hivi sasa mambo ni tofauti. Pembezoni mwa barabara hii kumefungwa zaidi ya taa 20 zinazotumia umemejua, kwenye umbali unaokaribia nusu kilomita katika eneo hili zinazotoa mwanga unaowezesha kufanyika kwa shughuli zote hizi nyakati za usiku.
Taa zaleta nuru mpya kwa wafanyabiashara
Kuwepo kwa taa hizo kunalifanya soko la Nguzo Mbili kuwa miongoni mwa masoko yanayotoa huduma kwa saa 24 mkoani Morogoro.
“Zamani tulikuwa tunakodi taa, sasa hivi hatukodi. Hata wenye taa nadhani wanalalamika kwa sababu tumeletewa umeme wa bure…hiyo Sh 30,000 niliyokuwa nalipa kukodia taa kwa mwezi naweza kuifanyia shughuli nyingine,” anasema Sauda Nasibu, maarufu kama mama Swairat.
Mfanyabiashara huyo wa nyanya na chakula sokoni hapo kwa zaidi ya miaka 10, anasema taa hizo zimeleta “nuru mpya” maishani mwake.
Awali wafanyabiashara ambao hawakutaka kufunga biashara zao baada ya saa kumi na mbili jioni walilazimika kukodi taa kwa Sh500 hadi 1,000 kwa siku au kununua taa kwa Sh3,000 walizokuwa wanaweka betri za Sh 1,500 kila siku jambo lililokuwa linatoboa mifuko yao zaidi.
Mwenyekiti wa soko hilo Athumani Iddi ameiambia Nukta Habari kuwa uwepo wa taa hizo umewaongezea wateja kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa huo na kuwawezesha kujiendeleza kiuchumi.
“Watu wanakuja kutoka sehemu mbalimbali kwa sababu ya mataa…Tumepata faida kubwa tunajenga sawa, na pia watoto wanasoma kama kawaida kutokana na kwamba watu tunafanya kazi muda mrefu sana,” anasema Iddi.
Taa hizo za umemejua ni matokeo ya miradi mbalimbali inaofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Elico Foundation ikilenga kusambaza nishati umeme katika maeneo ambayo hajafikiwa na gridi ya Taifa kwa dhumuni la kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo hayo na kuchechemua uchumi wa nchi.
Pamoja na umemejua barabarani, Elico Foundation wamewawezesha wakazi wengine wa vijijini pampu za umemejua kumwagilia mazao na kunywesha mifugo.
Kutokana na umemejua hivi sasa Utingo waliopo katika soko la Nguzo Mbili wanaweza kushusha mizigo muda wowote ndani ya masaa24.Picha|Esau Ng’umbi.
Usalama waimarika
Pamoja na taa hizo kuwezesha shughuli za biashara kufanyika kwa saa 24, wafanyabiashara wanafurahia zaidi usalama wao na mali zao uliochagizwa na uwepo wa mwanga katika eneo kubwa la soko hilo ambapo awali vilikuwa vinatendeka vitendo vya wizi na uporaji kutokana na giza.
“Zamani watu walikuwa wanakabwa hata ukiwa na kihela chako unawaza utakificha wapi wasikione…ukitoka hapa saa tatu ukifika nyumbani salama unasema ‘alhamdulilah’ ila sasa hivi hata saa sita unarudi nyumbani salama,” anasema Sauda.
Licha ya kutokuwa na idadi rasmi, Mwenyekiti wa Soko hilo Athumani Iddi amebainisha kuwa kuimarika kwa usalama kumechochea idadi ya wafanyabiashara kuongezeka, wengi wao wakiwa ni wanawake.
Hali hiyo iliyodumu kwa miezi miwili katika soko la Nguzo mbili ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wa baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam ambao hufurahia fursa kedekede zilizoletwa na taa za barabarani zinaoangaza kwa saa 24.
Kutokana na taa hizo, wafanyabiashara wengi wajiji hilo hujikuta wakifanya biashara kwa muda mrefu kutokana na wingi wa watu na usalama uliopo jambo ambalo linawaonngezea kipato.
Ripoti ya upatikanaji na matumizi ya nishati Tanzania ya mwaka 2019/2020 inaonyesha kuwa asilimia 30.4 au 3 kati ya 10 ya kaya nchini Tanzania wanatumia nishati ya umemejua kama chanzo cha nishati majumbani.
Bidhaa maarufu zinazopatikana katika soko la Nguzo bili ni pamoja na Nyanya na vitunguu ambavyo hupatikana katika misimu yote mwaka mzima zikitoka maeneo mbalimbali nchini.Picha |Esau Ng’umbi.
Kizuizi kilichobakia
Pamoja na kuwa na faida ya mwanga unaowawezesha kufanya shughuli zao kwa saa 24, bado wafanyabiashara wa nguzo mbili wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu mibovu ya soko.
Tofauti na masoko mengine ambayo huwa na meza maalumu zilizojengwa kwa zege, wafanyabiashara wa soko la Nguzo Mbili hupanga bidhaa zao chini, ambapo hutandika magunia au maturubai kuzuia unyevu unyevu na mafuriko ya maji yanayopita eneo hilo.
Wengi wao vibanda vyao vimeshikiliwa na mbao nyembamba huku mabati yakionekana chakavu kutokana na kutokufanyiwa ukarabati muda mrefu. Kwa sasa changamoto kubwa zaidi, kwa mujibu wa wafanyabiashara wa soko hilo, ni ukosefu wa choo ambapo kuna matundu mawili tu ya choo yanayotumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 300 hali inayotishia usalama wa afya zao.
“Ushuru unachukuliwa lakini bado hawatuboreshei, tumejenga banda na mabati yanazidi kuisha…choo hawatujengei, mimaji ikija inatuvamia, tunaiomba Serikali watuwekee vifusi pia watujengee soko,” amesema Mwenyekiti Iddi.
Hata hivyo, haijawa bayani ni lini changamoto hizo zitakoma baada ya juhudi za Nukta Habari kusaka maofisa wanaohusika kufua dafu. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba hakupatikana kwa wakati kuelezea changamoto hizo.
Soma zaidi:Umemejua unavyowakwamua wanawake kiuchumi Tanzania
‘Umemejua ni nguzo ukuaji wa uchumi’
Mdau wa nishati jadidifu na Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii kipunguni Selemani Bishagazi, ameiambia Nukta Habari kuwa nishati jadidifu ikiwemo umeme jua husaidia kukuza kipato cha wanafanyabiashara huku ikiwaepusha kutopoteza wateja.
“Hakuna kitu kibaya kama unahudumia mteja alafu umeme ukakatika ghafla hiyo inakufanya unapoteza wateja…ina maana bishara yako inakuwa haina uhakika,” amesema Bishagazi.
Aidha, amewashauri baadhi ya wafanyabiashara wanaosita sita kujiingiza katika matumizi ya nishati jadidifu ikiwemo umemejua kuanza matumizi yake mapema kwani yatawapunguzia gharama za uendeshaji.
Mkurugenzi huyo pia anasema kama Taifa endapo tutahamasisha matumizi wa jadidifu tunaweza kujihakikishaii kukua kwa uchumi unaotokana na kodi za wafanyabiashara hao.