Umemejua unavyoboresha, afya, elimu Bagamoyo
- Umemejua waongeza ufaulu na idadi ya wanafunzi shuleni.
- Innovation Africa, Bayport wapania kuboresha maisha ya wananchi vijijini.
- Wadau washauri usawa uzingatiwe katika utoaji wa huduma za jamii.
Dar es Salaam. Kutoka mbali ukiwa unaikabili shule ya sekondari Moreto wakati wa mchana utaliona paa la shule hiyo likitoa miale mikali ya mwanga.
Lakini ukisogea karibu utagundua wazi ni miale ya paneli za sola zilizofungwa juu ya paa la shule hiyo.
Shule ya Moreto ambayo ni ya bweni iko kwenye kijiji cha Mindutulieni wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani; ni miongoni mwa shule za sekondari ambazo hazijaunganishwa na gridi ya taifa ya umeme. Lakini imefanikiwa kupata umemejua na kwa sehemu kubwa kuondokana na tatizo la wanafunzi kukaa gizani.
Kazi kubwa ya umemejua shuleni hapo ni kuwaangazia wanafunzi kwenye mabweni na wakati wakijisomea masomo ya jioni baada ya kukamilisha vipindi vya darasani.
Kabla ya wanafunzi wa Moreto kupata umemejua, wanafunzi walikuwa wanasomea nje wakitumia mwangaza wa mwezi na katika vipindi ambapo mwezi haonekani iliwalazimu kukaa gizani na kusubiri mapambazuko ya jua.
Ukosefu wa umeme uliathiri maendeleo ya wanafunzi katika shule hiyo hasa katika mitihani ya kidato cha nne. Mathalani mwaka 2016 wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne walikuwa 60 lakini ni 32 tu kati ya hao walifaulu.
Lakini mwaka uliofuata wa 2017, wanafunzi wa Moreto walikuwa na kila sababu ya kusoma kwa bidii, baada ya kampuni ya Innovation Africa (iA) kutoa msaada wa kuwafungia sola paneli ambayo inatumika kusambaza umemejua kwenye mabweni na madarasani.
Umuhimu wa umemejua shuleni hapo ulianza kujitokeza mwaka huo huo wa 2017 ambapo idadi ya wanafunzi wanaohudhuria vipindi darasani na kufaulu mitihani imeanza kuongezeka.
Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka jana wanafunzi 33 kati ya 67 walifaulu. Licha ya kutopata mafanikio makubwa kielimu, Moreto imeonyesha muelekeo mzuri wa kuboresha huduma za kijamii ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
“Ili kuongeza idadi ya wanafunzi, Innovation Africa imeipatia jamii ya Moreto vifaa muhimu ili kuvunja mnyonyoro wa umaskini- upatikanaji wa umemejua na mwanga,” inaeleza taarifa ya utekelezaji wa mradi wa iA uliofadhiliwa na Debra Pell,raia wa Israel.
Uwepo wa umemejua shuleni ni kichocheo cha wanafunzi kuhudhuria masomo. Picha|Innovation Africa
iA yenye makao yake Marekani imejikita kutumia teknolojia rahisi ya nishati ya jua kuboresha maisha ya watu wanaoishi vijijini, imefanikiwa kuunganisha umemejua kwenye shule 16 na vituo vya afya viwili katika wilaya za Bagamoyo na Chalinze.
Katika kuhakikisha inakuwa sehemu ya kuboresha huduma za jamii, iA imeingia kwenye makubaliano na taasisi ya Fedha ya Bayport Management Limited kutekeleza mradi wa kuwasogezea karibu huduma ya maji safi na umeme kwa watanzania waishio vijijini.
Katika makubaliano hayo, Bayport imekubali kubeba jukumu la kusafirisha wataalamu na vifaa katika maeneo ya miradi ambapo iA itajikita zaidi kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi ya sola kuwaongezea nishati ya umeme mbadala wakati wakisubiri gridi ya umeme wa Taifa kupita katika maeneo yao.
“Ushirikiano kati ya kampuni hizo mbili utasaidia kuboresha afya na elimu, na matokeo chanya kwa maisha ya watu wa Tanzania kupitia matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua na maji,” inaeleza taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano cha Bayport.
Tayari wamefanikiwa kufunga paneli za umemejua katika kituo cha afya cha Bumbuta na pampu ya kusambaza maji safi katika kijiji cha Iyoli mkoani Dodoma.
“Ushirikiano huu na iA unakubalika kwetu sote,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Bayport, Stuart Stone. “Mashirika yetu yanatumia teknolojia na ubunifu kuwapa watu wanaoibukia kwenye soko la vifaa ili kuboresha maisha yao na kujenga mstakabali mzuri.”
Zinazohusiana:
- Lucy, katuni aliyejizatiti kupunguza mimba za utotoni Morogoro.
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya taifa.
Mpaka sasa watu zaidi ya 200 kutoka katika nchi za Uganda, Malawi, Tanzania, Ethiopia, Afrika Kusini, the Democratic Republic of Congo, Senegal na Cameroon wamefaidika na teknolojia ya umemejua inayowezeshwa na iA.
“Msaada wa Bayport unatuwezesha sisi kutoa suluhu kwa vijiji vya pembezoni mwa Tanzania, na kuwawezesha wanajamii kujikwamua wenyewe kwenye umaskini uliopitiliza kwa kuwapa njia mbadala,” anasema Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Innovation Africa, Sivan Ya’ari.
Mambo ya msingi ya kuzingatia
Wachambuzi wa masuala ya elimu wanabainisha kuwa kuna mahusiano kati ya uwepo wa huduma za jamii shuleni kama umeme na uelewa wa masomo na ufaulu wa wanafunzi, ambapo ameishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau kuongeza juhudi za kuboresha huduma za kijamii hasa kwa wanafunzi.
Meneja Programu wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla anasema kukosekana kwa usawa wa huduma za kijamii katika sekta ya elimu kunaathiri ujifunzaji wa wanafunzi darasani na hata maendeleo ya eneo husika.
“Kukosekana kwa usawa kwenye mfumo wa elimu kunajidhihirisha katika matokeo ya kujifunza, rasilimali na huduma zinazopatikana shuleni,” anasema Mgalla.
Anasema athari za mfumo huo usiozingatia usawa zinadhihirisha dhahiri kwamba maeneo ambayo yana huduma nzuri yamepiga hatua katika maendeleo ambapo kiwango cha umasikini kiko chini ukilinganisha na maeneo ambayo huduma hazipatikani; jamii zake bado ziko kwenye lindi la umasikini. Licha ya umemejua kuwa suluhuhisho la tatizo la umeme katika shule na vituo vya afya lakini ufanisi wake hupungua wakati wa mvua na baridi nyingi ukilinganisha na umeme wa gridi ya taifa ambao unapatikana wakati wote.
Ili kutatua changamoto ya kukatika kwa umemejua, watumiaji wanashauriwa kutengeneza mfumo wa kuhifadhi umeme katika kipindi ambapo jua linakuwa limepungua.
Wanafunzi wa shule ya msingi Makurunge wilayani Bagamoyo wanapata umemejua. Picha|Innovation Africa.