Uchafuzi mto Ngerengere unavyotishia uhai wake, viumbe hai Tanzania

Morogoro. Katika moja ya mito inayopita katikati mwa mji wa Morogoro, takataka mbalimbali zinaonekana pembezoni wa mto huo huku kukiwa na vijito vidogo vidogo vinavyotiririsha maji machafu ndani yake kutoka viwandani na majumbani.
Sehemu nyingine za mto huo unaojulikana kama Ngerengere zina taka ngumu ambazo si rahisi kusafirishwa na maji kiasi cha kunasa kwenye kingo zake.
Ngerengere ni moja ya rasilimali muhimu ya maji nchini Tanzania hasa kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani.
Mto huu ni chanzo cha maji katika bwawa la Mindu unaotegemewa na wakazi wa Manispaa ya Morogoro, ambao maji hayo kwa shughuli mbalimbali za majumbani, kilimo, mifugo, na viwanda.
Utegemezi wa Mto Ngerengere hauishii kwa wakazi wa Morogoro pekee.
Mto huu ni miongoni mwa mito mitano inayomwaga maji Mto Ruvu ambao ni chanzo muhimu cha maji safi na salama kwa zaidi ya robo tatu ama asilimia 79 ya wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo, uhai wa Mto Ngerengere upo hatarini kupotea na kuathiri viumbe hai wa majini, kutokana na uchafu unaotoka majumbani, viwandani, pamoja na shughuli za kilimo na ufugaji karibu na mto huo.

Miongoni mwa taka zinatupwa katika mto huo zinajumuisha taka ngumu na nyepesi na utiririshaji wa maji machafu yakiwemo yenye kemikali kuelekea mtoni.
Athari za uchafuzi wa mto Ngerengere zimekuwa zikionekana kwa nyakati tofauti kwa watumiaji wa maji ya mto huo wakiwemo wa wakazi wa Manispaa ya Morogoro ambako mto huo umekatiza.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa cha Kipera uliopo kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro wanasema hupata matatizo ya kiafya ambayo hutokea baada ya kutumia maji ya mto Ngerengere.
Katarina Mchiwa, mkazi wa mtaa wa Kipera anasema huyatumia maji ya mto huo unaopita mtaani hapo kwa ajili ya kupikia, kunywa, kuoga na kufulia.
Kwa nyakati tofauti baada ya kuyatumia hukutana na athari za kiafya kama kuwashwa ngozi pamoja na kuhara wanapotumia maji ya mto huo.
“Maradhi ya kuharisha hayatupiti mbali kutokana na maji tunayokunywa, nikienda kwenye vikao na wenzangu huwa nawaambia hebu niangalieni mwili wangu una mapele kwa sababu ya maji, ukioga tu lazima uone mwili unawasha ni lazima upake mafuta ndo kidogo hali inatulia,” anasema Katarina.

Wakazi wa Kipera wakichota maji ya Mto Ngerengere kwa ajili ya matumizi ya majumbani kama kufulia na kupikia. Picha l Esau Ng’umbi
Wakazi wa Kipera hutegemea kwa sehemu kubwa maji ya Mto Ngerengere kutokana na mtaa wao kukosa miundombinu ya maji ya bomba, jambo linalowafanya kutembea umbali mrefu au kutumia pikipiki kwa wenye uwezo kufuata maji katika mitaa ya jirani.
Serikali ya mtaa wa Kipera inaeleza kuwa athari za uchafuzi wa mto huo hutokea zaidi wakati wa kiangazi wakati kiwango cha maji kikiwa chini.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kipera Bakari Athumani alitueleza kuwa huwa wanagundua uchafuzi kirahisi kutokana na maji hayo kubadilika rangi na kutoa mapovu.
“Kutokana na kuwa hatuna miundombonu ya maji safi mto huo ndo tunautegemea kama chanzo cha maji ya matumizi madogo madogo kama, kufulia nguo, kuosha vyombo,” ameeleza Mwenyekiti Athumani.

Bago Dile, mkazi wa Kinguruwila mkoani Morogoro anayejishughulisha na kufyatua matofali kwa kutumia maji ya mto Ngerengere ameiambia Nukta habari kuwa miongoni mwa changamoto anayoipata kutokana na uchafuzi wa maji hayo ni kupata fangasi za mikono na miguu kutokana na kugusa maji hayo kila siku.
Licha ya athari hizi za kiafya, Bago na wenzake wanalazimika kuendelea kutumia maji ya mto huo ikiwemo kunywa kwa kuwa hawana njia mbadala ya kupata maji kukidhi mahitaji yao. kazi zao.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linabainisha kuwa mwaka 2022 zaidi ya watu bilioni 1.7 duniani kote walitumia chanzo cha maji ya kunywa kilichochafuliwa na kinyesi.
Kwa mujibu wa WHO uchafuzi wa vijidudu kwenye maji ya kunywa unaosababishwa na kinyesi ndiyo hatari kubwa zaidi kwa usalama wa maji ya kunywa duniani.
WHO inaonya uwezekano wa kutokea kwa athari kubwa za kiafya kutokana na kutirishwa kwa kemikali hasa za viwandani kwenye vyanzo vya maji kwa sababu matokeo yake huonekana baada ya muda mrefu.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inakataza shughuli za kibinadamu umbali wa mita sitini kando ya vyanzo vya maji ikiwemo mito.
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro Rufiji, Abel Sembeka ametueleza hivi karibuni kuwa shughuli za kibinadamu, ndio chanzo cha uchafuzi wa Mto Ngerengere.

Mbali na shughuli za kibinadamu, kwa mujibu wa Sembeka baadhi ya viwanda mkoani humo vinatitirisha maji yenye kemikali katika mto huo jambo ambalo si tu linaweza kuhatarisha uhai wa mto Ngerengere bali hata afya za watumiaji.
“Kuna changamoto pia ya uchafuzi wa Mto Ngerengere ikiwa ni pamoja na vowanda ambavyo viko ndani ya manispaa ya morogoro siwezi kuvitaja kwa majina lakini baadhi yake vinazalisha maji taka lakini hayo maji taka yanaishia kwenye mto Ngerengere na hawayatibu kwa utaratibu unaotakiwa,” amesema Sembeka.
Sembeka ameongeza kuwa kutofanyika kwa ukarabati wa mabwawa ya kutibu maji machafu yanayotoka katika baadhi ya viwanda vilivyopo Manispaa ya Morogoro, huchangia uchafuzi wa mto huo.
Aidha, Sembeka ameeleza kuwa kwa sasa kuna jitihada za ukarabati wa mabwawa hayon kwa kushirikiana na wadau ikiwemo asasi za kiraia na wamiliki wa viwanda wenyewe.
“Tunapozungumza mda huu, Manispaa ya Morogoro wako wanamalizia kupima yale maeneo na kumkabidhi Mwaruwassa ili ashirikiane na wadau wa viwanda kuanza kukarabati mabwawa hayo, sisi kama wadau wa mazingira tunamani kazi hiyo ianze kabla mvua hazijaanza kunyesha..

Mabwawa ya kuhifadhi maji yanayotoka viwandani yakiwa yamejaa maji ambayo hayajatibiwa. Picha l Esau Ng’umbi
Viwanda vilishakubali na mpango wa muda mrefu ni kuwa, viwanda vipya vitakavyokuja vitaunganishwa na hayo mabwawa na yatakuwa yanafuatiliwa kwa ukaribu sana,” amesema Sembeka.
Baadhi ya wamiliki wa viwanda tuliozungumza nao wanakiri kuwa baadhi yao hutiririsha maji mtoni japo wanajivua kuwa wao hawahusiki na uchafuzi huo na wamekuwa wakitafuta njia ya kuboresha mabwawa.
Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha 21 Century kilichopo Morogoro Clemence Munisi alitueleza kwa njia ya simu kwamba kiwanda chao hakihusiki na kutiririsha maji yenye kemikali ndani ya Mto Ngerengere kwa kuwa huyatibu maji yao kabla ya kutiririshwa.
“Sisi tunatibu maji yetu vizuri, na kuyaachia wakati yana vipimo kabisa, na pale yanapoingilia mtu yoyote anaweza kwenda akacheki pale akaona, lakini yanayotoka sehemu nyingine hayatibiwi, tunaona yana harufu,” amesema Munisi.
Ili kuboresha zaidi udhibiti wa kemikali za viwandani, anasema wao wana nia ya kuyakarabati mabwawa hayo ila wanakosa ushirikiano kutoka kwa taasisi zinazohusika, jambo linalokwamisha mchakato huo.
Sera ya Taifa ya Maji na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009 inazuia uchafuzi wa maji na inazipa mamlaka Bodi za Maji za Bonde zilizopo nchini Tanzania kuchukua hatua dhidi ya watu wanaohatarisha rasilimali hiyo.
Mto Ngerengere kama ilivyo mito mingine iliyopo mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam unasimamiwa na Bodi ya Bonde la Wami Ruvu.
Mhandisi Lusajo Edwin, Afisa Kidakio cha Ngerengere kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu ameiambia Nukta Habari kuwa wanafahamu uchafuzi wa maji ya mto huo kutoka viwandani.
Edwin anasema wanachukua hatua kulinda Mto Ngerengere kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo NEMC katika kusimamia vigezo vya utoaji wa leseni za utiririshaji maji, kufanya doria za mara kwa mara mtoni na kukagua ubora wa maji yanayotiririshwa kutoka viwandani na shughuli nyingine.
Kwa mujibu wa Wizara Ya Maji, Tanzania inakadiriwa kuwa na rasilimali maji inayofikia mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka, ambapo kati ya hizo zaidi ya mita za ujazo bilioni 105 ni kutoka rasilimali za maji za juu ya ardhi ikiwemo bahari, maziwa, pamoja na mito.
Hata hivyo, uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji unaoendelea huenda vikatishia uwepo wa rasilimali hiyo muhimu kwa uhai wa binadamu na viumbe hai wengine.

Shughuli za kibinadamu zikiendelea pembezoni mwa mito midogo inayotiririsha maji kwenye mto Ruvu mkoani Morogoro. Picha l Esau Ng’umbi
Wadau wa utunzaji wa rasilimali maji wanashauri kuwa mamlaka na wadau wengine wanatakiwa kushirikiana katika utunzaji wa rasilimali maji ili kuiepusha Tanzania na uhaba mkubwa wa maji siku zijazo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kiraia la Shahidi wa Maji, Abel Dugange alitueleza kuwa ili kulinda vyanzo vya maji ukiwemo Mto Ngerengere hutoa elimu kwa wananchi na kufanya utafiti kujua ubora wa maji.
“Tunaitengeneza jamii ambayo inaweza kufuatilia rasilimali maji zao, lakini atusemi lazima iwe na sayansi ya maji, kuna vile viashiria vya kawaida kuwa mbona haya maji yapo tofauti, sasa sisi tunawaambia mahali sahihi kwa kuuliza haya maswali ni hapa,” amesema Dugange.
Shahidi wa Maji ni miongoni mwa mashirika vinara katika kuhamasisha utunzaji wa maji nchini yakiwemo maeneo yanayokabiliwa na matatizo makubwa ya uharibifu na migogoro ya matumizi ya rasilimali hiyo kama Kilombero na Kilosa.

Latest



