‘Tuma na ya kutolea’ ya Tigo Pesa: Ni ubunifu, ahueni ama yale yale?

March 25, 2021 5:55 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Uchambuzi wa awali uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa huduma hiyo mpya inapunguza hatari ya kutuma zaidi kiwango cha “ya kutolea” ama kutuma kiasi pungufu na kinachotakiwa.
  • Huduma hiyo haijabadisha gharama nyingine za kufanya miamala.

Dar es Salaam. Ilianza taratibu kwa baadhi ya watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi kuwasihi wanaowatumia fedha kuwa watume na gharama za kutolea kupitia msemo mashuhuri wa “tuma na ya kutolea”.

Hata hivyo, haikuchukua muda msemo huo wa tuma na ya kutolea kubamba mitandaoni na kuwafanya baadhi kuanza kuwatania mabinti wanaowaambia wenza wao kutuma kiasi cha fedha na cha kutolea kupitia simu za mkononi kwa huusisha na picha ama video za watu wanaofanya kazi ngumu.

Sasa msemo huo umekuwa ni fursa ya kibiashara baada ya kampuni ya huduma za simu ya Tigo hivi karibuni kuanzisha chaguo maalum la kumtumia mtu fedha kupitia Tigo Pesa kinachojumuisha kiwango cha kutolea. “Tuma na ya kutolea” ni sehemu ya gharama za kufanikisha muamala.



Sehemu ya machaguo ya kutuma fedha kupitia huduma ya Tigo Pesa. Picha|Nukta. 

Chaguo hilo lilipo kwenye uwanja wa machaguo maarufu kama ‘menu’ ya Tigo Pesa ni moja ya machaguo ya sehemu ya huduma za kipengele cha kutuma fedha. Hata hivyo, hulazimishwi na kutuma na ya kutolea.

Mabadiliko hayo ya menu ya Tigo Pesa bado hayajaanza kujitokeza katika programu rununu (app) ya Tigo Pesa labda kwa watu waliopata maboresho yake.

Ni ubunifu, ahueni ama yale yale? 

Uchambuzi zaidi uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) unabainisha kuwa huduma hiyo mpya ndani ya Tigo Pesa itasaidia wale wasiojua kiwango halisi cha kutolea kupunguza hatari ya kutuma fedha nyingi zaidi kiasi cha kumnufaisha mpokeaji.

Majaribio ya kurusha fedha kwa Tigo Pesa kwa kutuma chaguo la “tuma na ya kutolea” na lile kawaida yanaonyesha kuwa kabla ya kutuma fedha kwenye chaguo hilo jipya la ya kutolea unaonyeshwa na kiwango cha kutolea jambo ambalo huwezi kulipata kwenye menu iliyozoeleka.

“Unakaribia kutuma Sh2, 000 na ya kutolea Sh400 kwenda kwa xxxxx (namba ya Vodacom) xxxx (jina la mpokeaji). Ada ni Sh50. Tafadhali ingiza namba ya siri kuthibitisha,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa Tigo Pesa kabla ya kutuma fedha kwenda mtandao mwingine kupitia menu ya “tuma na ya kutolea”.

Hata hivyo, ada za kawaida za kutuma fedha zimebaki kama zilivyokuwa awali huku kutuma fedha ndani ya mtandao huo wa Tigo zikibaki zilezile iwe umema kwa chaguo la “tuma na kutolea” ama kawaida.

Tangazo: 



Katika kiwango hicho cha Sh2,000 kilichotumika kwenye majaribio, ada ya Sh30 ilitozwa kwenda kwa mtumiaji wa Tigo Pesa kupitia “tuma na ya kutolea”, kiwango ambacho ni sawa kabisa na kile ambacho kilibainishwa kwenye menu ya kawaida ya kutuma fedha ila cha chini kidogo ikilinganishwa na Sh50 kwenda mitandao mingine.

Iwapo utafananisha na menu ya zamani, kuna ubunifu katika “tuma na ya kutolea” kwa kuwa inampunguzia mteja muda na usumbufu wa kuanza kutafuta taarifa za gharama za kutoa na kufanya hesabu kiwango gani anachotakiwa kuwa nacho ili kukamilisha muamala.

Hata hivyo, ahueni iliyopo ni kwa wale ambao wamekuwa wakituma fedha nyingi za kutolea ama kidogo kiasi cha kumfanya mpokeaji apate kiwango kidogo na kile kilichotarajiwa.

Enable Notifications OK No thanks