Tuboreshe sheria kuwalinda wazee Tanzania

February 3, 2023 8:54 am · Abdushakur
Share
Tweet
Copy Link
  • Wazee washauri wapewe elimu na msaada wa kisheria.
  • Wasema bado wanakabiliwa na changamoto nyingi. 

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo jijini Mwanza wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuongeza uelewa wa sheria zinazohusu wazee ili kuboresha maslahi ya kundi hilo nchini.

Baadhi ya wazee hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuhisiwa ni wachawi na hivyo kwa nyakati fulani kukabiliwa na vitisho, kuzalilishwa na kuuwawa.

Baadhi ya wazee jijini hapa, wameiambia Nukta Habari kuwa hukumbwa na changamoto za kisheria lakini baadhi yao hukosa namna sahihi ya kuzitatua.”Natambua tuna haki ya kulindwa ila bado usalama wetu haujaimarika, mtoto wa kuzaa  anakuita mchawi hujui sehemu ya kupeleka kesi hiyo na hata ukiipeleka haisikilizwi,” amesema Eferdina Peter.

Efradina (70) anasema kutolewa kwa elimu ya kutambua sheria kutaongeza ujasiri wa wazee kupigania haki zao wanapoona zimekiukwa. 

Mzee Dk Tungi Charles, Afisa mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni mtaalamu wa udhibiti ubora wa chakula ameshauri Serikali kuboresha sheria zinazolinda wastaafu katika taasisi zote ili kuwaandalia mazingira mazuri wanapotoka kwenye utumishi.

“Serikali iweke mkazo kwenye utekelezaji wa sera na sheria zake kwa wazee,  mifumo ya huduma za kijamii na tiba kwa wastaafu ni mibovu, thamani ya wastaafu inazidi kupungua kadri miaka inavyozidi kwenda,” amesema Dk Charles. 

Edward Magembe miongoni mwa wazee maarufu wa Mtaa wa Silivini, Kata ya Luchelele wilayani Nyamagana ameiomba Serikali kupitia na kutunga  upya sheria zote zinazo walenga wazee na kusimamia utekelezaji wake.

Mzee Magembe amesema kuwa hilo litaongeza hamasa kwao kuzidi kujifunza sheria  ili kujua maeneo muhimu yanayowalenga. 

Wazee hao wamedai kuwa endapo elimu ya utambuzi wa sheria isipokuwa endelevu, wataathirika zaidi na kushindwa kupata haki zao za msingi mbali na kutekeleza wajibu wao kisheria.


Soma zaidi:


 

Wazee wana haki

Wakili  Amri Linus  kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) jijini Mwanza, amesema kuwa wazee wana haki ya kupata msaada wa kisheria bila malipo. 

Wakili Linus ameeleza kuwa baadhi ya wazee hawana uwezo wa kusimamia kesi zao na wengine hawafiki mahakamani kutokana na sababu mbalimbali.

Amesema TLS inapigania haki za wazee kupitia msaada wa kisheria bure ili kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili.

“Wazee kufika mahakamani  ni changamoto na wakifika hawapati kipaumbele lakini hilo linawekwa sawa kupitia haki ya msaada wa kisheria bure…” amesema Wakili Linus.

Wakili Linus ameshauri Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kutilia mkazo elimu ya utambuzi wa sheria mbali na kusubiri matukio ya kisheria.

Diwani wa kata ya Buhongwa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Joseph Kabadi amesema kuwa wameendelea kuendesha semina elekezi kutoa elimu ya sheria kwa wazee ili wazidi kufahamu haki na wajibu wao kisheria.

Diwani Kabadi amewataka wananchi kuachana na dhana potofu ya kumhusisha mzee na uchawi kwani ni kosa kisheria.

 “Sheria za nchi hazitambui uchawi na sisi hatupaswi kuutambua uchawi, wakina mama wakongwe mara nyingi huingizwa kwenye tuhuma hiyo, lakini hata mtoto anaweza kuwa mchawi,” amesema Diwani Kabadi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...