Trump awasili Israel akielekea kwenye mkutano wa amani Misri
- Ajivuna kumaliza vita kati ya Hamas na Israel
Dar es Salaam. Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Israel ambako amekutana na familia za mateka na kuhutubia Bunge la Israel (Knesset) kabla ya kuelekea Sharm el-Sheikh, nchini Misri, kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu vita vya Gaza.
Rais Trump alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na Rais wa nchi hiyo Isaac Herzog muda mfupi baada ya mateka saba waliokuwa wakishikiliwa na Hamas kukabidhiwa kwa jeshi la Israel kupitia shirika la Msalaba Mwekundu.
Hamas imesema mateka wote 20 waliokuwa hai wataachiwa leo kwa kubadilishana na wafungwa zaidi ya 1,900 wa Kipalestina.
Akiwa safarini kwa ndege ya Air Force One, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba vita kati ya Israel na Hamas vimekwisha.”
Baadaye leo, Trump na Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi wataongoza mkutano wa kilele unaolenga kudumisha usitishaji mapigano na kujenga misingi ya amani ya kudumu.

Kwa mujibu wa Ikulu ya Misri, viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria ni Emmanuel Macron wa Ufaransa, Friedrich Merz wa Ujerumani, Keir Starmer wa Uingereza, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amempongeza Trump kwa juhudi zake za kutafuta suluhu za mzozo huo akimuita rafiki mkubwa wa Israel kati ya wote waliowahi kupita Ikulu ya Marekani, White house.
Makubaliano ya kusitisha Vita katika ukanda wa Gaza yanakuja ikiwa ni takriban miaka miwili imepita tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7, 2023, baada ya Hamas kuishambulia Israel na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200 wakiwemo Watanzania wawili na kuchukua mateka 251.
Israel ilijibu shambulio hilo kwa mashambulizi ya angani na ardhini na kusababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 67,000 huku wengine zaidi ya 169,000 wakijeruhiwa.
Latest



