Trump asitisha safari za Ulaya kwenda Marekani kujikinga na Corona

March 12, 2020 7:13 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Trump amesema hatua hiyo ni kwaajili ya kuepusha maambukizi mapya nchini Marekani. Picha| Sky news.


  • Rais Donald Trump wa Marekani amesitisha safari hizo kwa siku 30 ili kujikinga na virusi hivyo.
  • Asema nchi za Ulaya zimeshindwa kuchukua tahadhari dhidi ya Corona. 
  • Atangaza mikakati ya kukabiliana na virusi hivyo kunusuru mdololo wa uchumi.

Dar es Salaam. Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha safari za raia wa bara la Ulaya wanaoingia nchini Marekani kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuikinga nchi hiyo dhidi ya virusi vya Corona ambavyo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) imevitangaza kuwa janga la dunia. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, imeripotiwa kuwa nchini Marekani kuna visa 1,135 vya watu walioambukizwa virusi hivyo huku vifo vilivyothibitishwa ni 38.

Trump ametoa tangazo hilo  Machi 11, 2020 mara baada ya Italia ambayo ni nchi inayoongoza kwa kuathirika baada ya China kutangaza kufunga maduka yote kasoro maduka ya chakula na yanayouza dawa za binadamu.

“Kuzuia maambukizi mapya kuingia kwenye mipaka yetu, tunaahirisha safari zote kutokea Ulaya,” amesema Trump na kubainisha kuwa zuio hilo linaanza ijumaa ya wiki hii. 

Amesema Ulaya imeshindwa kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo, isipokuwa nchi chache ikiwemo Uingereza.

Zuio hilo limezigusa nchi 26 za Schengen (Ulaya) ambazo zilifuta mipaka ya ndani zikiwemo Ujerumani na Italia na watu ambao wametembelea nchi hizo ndani ya siku 14 huku Uingereza,  Ireland na nchi zingine zilizosalia hazitahusika na marufuku hiyo.


Zinazohusiana


Rais huyo ambaye amesema anafanya hivyo kuwalinda raia wa Marekani, ameshauri Bunge la Wawakilishi nchini humo kupitisha mikakati itakayoweka unafuu kwenye kodi ili kuzuia madhara ya kiuchumi yanayoweza kusababishwa na virusi vya Corona.

Pamoja na hayo, Trump ametangaza mipango ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuhakikisha uchumi wa nchi hiyo hauyumbi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia jana Machi11, watu 4292 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Corona huku watu 118 326 wakithibitika kuathirika na virusi hivyo. 

Taarifa ya WHO inaonyesha kuwa, China inaongoza kwa maambukizi kwa asilimia 68.4 huku vifo nchini humo vikiwa 3162 sawa na 73.67 ya vifo vyote ulimwenguni. 

Enable Notifications OK No thanks