Tofauti na ngono, haya ndiyo unayoweza kufanya kulinda penzi lako

February 7, 2020 12:45 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Usilalamike “nimetumiwa” jiulize mbali na ngono, ni mchango gani umetoa kwenye mahusiano yako.
  • Tafuta kitu mnachokipenda kwa pamoja na kifanyeni mara kwa mara kama muda upo.
  • Siyo mbaya ukianza kumtambulisha mwenzio hata kwa dada na kaka yako kama kweli una malengo naye.

Dar es Salaam. Malalamiko juu ya kuumizwa kimapenzi huenda ni kati ya jumbe unazozipata kila siku katika posti za mitandao ya kijamii.

Kulidhihirisha hilo, fungua ukurasa wako wa “status” kwenye mtandao wako wa whatsApp kisha angalia “status” za wadau wako na kisha vuta pumzi kuanza safari ya makala hii fupi.

Wakati baadhi ya vijana wakiumizwa na wapenzi wao na kuishia kusema “ameniacha baada ya kupata alichokitaka” huenda kama mtu ambaye haupo kwenye mahusiano unajiuliza ni nini kile watu hutafuta kwenye mahusiano. Ngono au ni kipi hasa? 

Nimezungumza na barobaro wawili watatu na walimbwende wachache na barobaro wameniambia kuwa, kile anachohitaji mtu kwenye mahusiano inategemeana na umri wa mtu na zaidi, aina yake.

“Kuna hatua mtu atataka mwenza kwa ajili ya kukidhi matakwa ya mwili na kuna wakati mtu atahitaji mwenza wa kutulizana naye kimaisha. Sasa mtu upo kidato cha tano unawaza kuoana na mwenza uliye naye, kweli…,” amesema kijana mmoja kati ya niliozungumza nao ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Jambo hilo linatupeleka kwenye swali la hatua ambayo wewe upo. Je, upo kwenye hatua ya utambuzi au kutulizana? Jibu unalo.

Ninapotea kwenye lengo la makala hii. Wacha nirudi kwenye mstari.

Kama wewe ni upo kwenye mahusiano ambayo mbali na ngono unaona hayana faida, haya ni mambo ambayo unaweza kujaribu kuanzia sasa ili uendelee kulifaidi penzi lako bila kujali hatua ambayo upo kwani kila sekunde kwa sasa ina hesabika.

Tumia muda na mwenzi wako

Huenda ukazidi kujihoji ni kwanini haumfikirii mpenzi wako lakini huenda ni kwa sababu haujapata kitu cha kukuwezesha kufanya hayo. 

Tumia muda wako unaoweza kuupata kwa kukaa naye huku mkibadilishana mawazo ya hapa na pale ili kuzidi kufahamiana.

Piga stori na mwenzio, penda kujua kuhusu yeye. Picha| |Dreamstime.

Wekeni malengo “jengefu”

Waswahili wanasema, “kipofu hawezi kumuongoza kipofu mwenzie”. Hivyo basi, kama kuna jambo ambalo wote hamlifahamu siyo mabaya mkatumia fursa ya mahusiano yenu kujifunza.

Mfano, mnaweza kujiwekea malengo ya kuhifadhi fedha kila mtu na fedha zake, mnaweza kushindana kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kompyuta na programu zake.

Msikae kizembe zembe. Mpenzi wako ni rafiki yako hivyo mahusiano yenu yanahitaji kuwa na manufaa.

Mtambulishe basi hata kwa dada yako

Endapo wewe upo kwenye kundi la wanaojitambua, hili halikuhusu. 

Kuna wakati mwingine wasichana huanza kufikiri kuwa hauko “serious” na yeye kwasababu umemficha.

Mbali na kwamba ukimpost unablock familia yako, jambo ambalo anaweza akawa anafahamu kama anatumia simu yako, haujawahi hata kumtambulisha siyo kwa rafiki tu bali hata ndugu zako.

Lakini kama wewe unahitaji kutulia, usiache ndege wako apeperuke kwa sababu amepata mwingine anayehisi ana malengo nayeye.

Mara moja moja mpe hata simu basi aongee na mama yako au hata dada. Inatosha.

Penda kufanya naye vitu tofauti tofauti. itawajengeaukaribu. Picha| Blackhealth.

Chunguza kujua kitu gani mnapenda wote, kifanyeni

Huenda “Bae” wako ni mpenzi wa mpira au hata mieleka. Hilo linaweza lisiwe fungu lako lakini siyo mbaya ukimpa sapoti.

Mara moja moja vaa hata jezi ya upinzani ilimradi tu apate cha kuongea lakini kama ukila mitama tafadhali nisihusike.

Natania tu… ninachomaanisha ni kwamba, kama mpenzi wako anapenda mpira, na wewe unapenda mpira ni muhimu muanze kuhudhuria mechi pamoja, au hata kwenda kwenye mabanda ya kuangalizia mechi pamoja. Itawajengea ukaribu.


Zinazohusiana


Funguka

Kati ya vitu vinavyovunja mahusiano, hili ni mojawapo.Wapo wadau huko nje hawaongei na wenza wao. Endapo mwenzi wako amekukwaza, ni bora umwite na muyazungumze na kuyamaliza.

Kama unapitia mambo fulani fulani pia funguka mwambie mwenzako. Kama anaweza kukusaidia ni heri lakini kama akishindwa, pia sio kesi.Tuishie hapa kwa leo. Asante kwa kusoma hadi mwisho, tukutane wiki ijayo.

Enable Notifications OK No thanks