TikTok yajisogeza kwa watumiaji wa televisheni janja
- Inakuwa App ya kwanza ya mtandao wa kijamii kuwa na app ya kujitegemea kwenye televisheni.
- Hatua hiyo huenda ni kuongeza wigo wa watumiaji wa TikTok na kuwapa watumiaji uwanda mpana wa matumizi.
Dar es Salaam. Mtandao wa kijamii wa TikTok ambao unaruhusu mtu kupakia maudhui ya video za hadi dakika tatu umezindua programu tumishi (app) ambayo itaanza kutumika kwenye televisheni janja za kampuni ya LG hivi karibuni.
Mtandao huo unafanya hivyo ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuwapatia watumiaji wake mawanda mapana ya kuchagua wapi watumie TikTok.
Kabla ya LG, TikTok ilikuwa imeshaanza kuonekana kwenye televisheni za kampuni ya Android, Samsung na Fire za Amazon.
TikTok ambayo imekuwa jukwaa la elimu na burudani inakuwa mtandao wa kijamii wa kwanza kuwa na app ya moja kwa moja kwenye televisheni.
Kabla ya hapo mtu alitakiwa kupakua app mbalimbali ikiwemo Smart Hub kwenye televisheni yake na kuiunganisha na simu janja ili aweze kuifikia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na Instagram.
Hata hivyo, baada ya app hii kuanza kutumika, TikTok itakuwa inajitegemea kama zilivyo apps za YouTube, Netflix na Prime Video kwenye televisheni janja.
Itaungana na App zingine ikiwemo Netflix na Amazon Prime. Picha| The Drum.
Hiyo itasongeza burudani kwa watumiaji wa mtandao huo kwenye skrini kubwa zaidi mbali na skrini ya simu janja au tableti kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la The Verge, televisheni za LG ambazo zitafikiwa na TikTok ni matoleo ya kuanzia mwaka 2019 hadi sasa.
“Matoleo ya awali yatafikiwa miezi michache ijayo” imeandika The Verge.
Hata hivyo, App ya Tiktok imetengenezwa kutumika kwenye simu (portrait mode) hivyo upana wa televisheni unaweza usiwe na muonekano mzuri kwa mtumiaji.
Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana katika nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Huenda na Tanzania ikafika mdogo mdogo.
Latest
