Shughuli zarejea Kariakoo, idadi ya waliofariki yafikia 29
- Kuanzia saa nane leo hii shughuli zote zinaruhusiwa kuendelea.
- Idadi ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo yafikia 29.
Dar es Salaam: Serikali ya Tanzania imetangaza kufunguliwa kwa biashara kwenye baadhi ya mitaa iliyofungwa kupisha zoezi la uokoaji lililokuwa linaendelea katika soko la kimataifa Kariakoo.
Msemaji wa Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba aliyekuwa akizungumza na wanahabari Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Novemba 26,2024 amesema shughuli zote za kibiashara katika eneo hilo zinaruhusiwa kuendelea kuanzia saa nane mchana.
“Mitaa mingine yote, Serikali imeamua kuanzia saa nane leo mchana, Kariakoo yote ukiacha iki kipande nilicho kielezea kazi zingine sasa zinaruhusiwa kwanzia saa nane leo hii shughuli zote zinaruhusiwa kuendelea” amesema Makoba.
Serikali imetoa maagizo hayo ikiwa ni takribani siku 10 tangu kutokea kwa ajali ya kuporomoka kwa jengo hilo Novemba 16 mwaka huu na baadae kufuatia agizo la Serikali kuzuia biashara katika eneo hilo kupisha zoezi la uokoaji lilokuwa likiendelea.
Hata hivyo, marufuku hiyo ya kuendelea kwa shughuli za biashara bado itasalia katika jengo liloloporomoka na majengo mengine mawili ambayo yaliathiriwa wakati wa ajali hiyo.
Pamoja na taarifa hiyo, Makoba amesema wamesitisha zoezi la okoaji huku vifo vikifikia 29 baada ya miili mingine tisa kupatikana wakati zoezi la utoaji kifusi likiendelea.
Makoba ameongezea kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na zoezi la kutambua miili kupitia teknolojia ya vinasaba kwasababu baadhi ya miili kuharibika kiasi cha kutotambulika kiurahisi baada ya kusalia kwenye kifusi kwa muda mrefu.
“Lipo zoezi linaloendelea kutambua miili mingine kwa kutumia teknolojia ya vinasaba na yenyewe tutaoa taarifa tukisha thibitisha ndugu pamoja na miili ya wenzetu” ameeleza Makoba.
Katika hatua nyingine Makoba amesema mmiliki wa jengo liloporomoka tayari ameshakamatwa na kuwataka Watanzania kuwa wavumilivu mpaka pale uchunguzi utakapo kamilika na taarifa zitakapotolewa.