Tiba shufaa inavyookoa gharama za matibabu kwa wagonjwa nchini

September 18, 2018 8:01 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni utaratibu wa matibabu unaoboresha ubora wa maisha ya mgonjwa na kuipunguzia familia gharama za kuuguza.
  • Wizara ya Afya yaanza kutoa kozi za tiba hiyo ili kuongeza wataalam katika sekta ya Afya.
  • Wadau washauri bima za afya kuchamkia fursa hiyo ili kuwafikia wagonjwa wengi zaidi.

Dar es Salaam. Ongezeko la magonjwa sugu kama saratani, kiharusi, figo na UKIMWI huambatana na gharama kubwa za matibabu ambazo mgonjwa anatakiwa kulipa ili kumrejesha katika hali ya kawaida.  

Hata hivyo, siyo wagonjwa wote wana uwezo wa kwenda hospitali kutokana na ngumu ya kiuchumi au hali ya kuumwa muda mrefu na kulazimika kukaa nyumbani akisubiri kifo. Hapo ndipo inaibuka tiba shufaa kuokoa jahazi lisizame.  

Tiba Shufaa ni tiba ni mahususi kwa watu wenye magonjwa sugu ambao wameumwa kwa muda mrefu bila kupata uponyaji. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO huduma za tiba shufaa ni utaratibu wa matibabu unaoboresha ubora wa maisha ya mgonjwa na familia iliyo katika matatizo yatokanayo na kuuguliwa kwa kuzuia na kupunguza matatizo katika maana ya kutambua mapema dalili za tatizo na namna ya kuhakiki tatizo na kutuliza maumivu na matatizo mengine ya kimwili, kijamii, kiakili na kiroho kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu.

Kutokana na umuhimu wa tiba hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanzisha mafunzo ya tiba shufaa (Palliative Care Services) kwa watumishi wa Sekta ya Afya ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wakati kwa wagonjwa wanaohitaji. na kusaidia kupunguza gharama za matibabu kwa kuwafikia wale waliopo katika mazingira duni.

Kupitia tiba hiyo, mtoa huduma anapaswa kumtembelea mgonjwa nyumbani kwa ajili ya matibabu ya mara kwa mara huku akisaidia kuwapa ushauri wanaomuuguza mgonjwa huyo.

“Tiba shufaa ina faida hasa kiuchumi, ikiwafikia watu nyumbani gharama zinakuwa ndogo” anasema Mkuu wa programu ya Tiba Shufaa inayotolewa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT) Dk. Zebadia Mmbando.

Wadau wa Tiba Shufaa huwa na utaratibu wa kuwatembelea wagonjwa majumbani kwao kupata kujua maendeleo ya wagonjwa hao.Picha|www.wn.de

Hata hivyo ukiondoa gharama za kutumia mgonjwa kwenda hospitali kufuata matibabu hata Serikali wanaweza kupata nafuu ya kuhudumia wagonjwa wanaopokuwa wengi hospitalini hasa wale wanaohitaji matibabu ya muda mrefu.   

Lakini bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya tiba shufaa kwasababu ya kutokuwa na hospitali au vituo vya afya vingi vinavyotoa huduma hiyo nchini.

“Madaktari wengi hawana elimu au uwezo wa kutoa tiba shufaa na ndiyo maana unaona serikali wametoa mtaala kwa ajili ya wauguzi kujifunza,” anasema Dk Mmbando.


Inayohusiana: 


Matibabu ya shufaa ambayo hufanyika zaidi nyumbani, bima ya afya haijaunganisha huduma hiyo kwenye mikakati yake jambo linaloweza kuwaongezea gharama za kuipata.   

“Nashauri bima ziwafikie hadi wagonjwa nyumbani na dawa za kupunguza maumivu makali (morphine) zipatikane maduka yote kupunguza gharama za kuzifuata hospitali,” anashauri Dk Mmbando. 

Hadi mwaka 2016, hospitali takribani 35 zikiwemo za rufaa za kanda za Bugando, KCMC na Mbeya, hospitali za mikoa pamoja na hospitali za dini zinatoa huduma hizo.

Hata hivyo bado hospitali za umma zinahitajika kuongeza vitengo vya tiba shufaa kurahisisha maisha ya mgonjwa na kupunguza gharama za matibabu na kuwapa ahueni kwa wanauguza na wagonjwa wenyewe.

Enable Notifications OK No thanks