Teknolojia ya upimaji Ukimwi kwa njia ya mdomo yaibua mjadala

November 25, 2019 4:07 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Uganda kuzindua matumizi ya teknolojia ya “OralQuick” ya kupima virusi vya Ukimwi.
  • Teknolojia hiyo siyo mpya Tanzania kwani ipo kwenye majaribio.
  • Sheria na upimaji binafsi wa Ukimwi waibua sintofahamu kwa wananchi. 

Dar es Salaam. Tanzania na Uganda zimejipanga na zinaendelea kutumia teknolojia kurahisisha vipimo vya Ukimwi ili kuondoa tishio la ugonjwa huo kuondoa uhai wa watu na nguvu kazi ya Taifa. 

Septemba 27, 2019, Uganda ilizindua matumizi ya teknolojia ya kupima virusi vya Ukimwi kwa njia ya kinywa inayojulikana kama “OralQuick kit”. 

Uzinduzi huo ni utekelezaji wa  adhimio la Uganda la  kuondoa ugonjwa wa Ukimwi kama tishio la jamii ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kifaa hicho kinatumia dakika 20 tu kutoa majibu ambapo mtu anayejipima anahitaji kukipitisha kifaa hicho kwenye fizi za juu na chini na kisha kukiweka kwenye “tube” maalumu na kusubiri kwa dakika 20 ili kupata majibu yake.

Mtaalamu wa afya na Mraghibishi wa masuala ya afya ya uzazi,  Dk Lilian Benjamin amesema kipimo hicho kinapima ute/majimaji ya mdomoni mwa mtu ambapo kinatumia kinga mwili (antibodies) kufanya vipimo na kutoa majibu. 

Kwa mtu anayeishi na virusi vya Ukimwi, unakuwa na “antibodies” ambazo zinazalishwa kwa wingi kupambana na virusi hivyo na kupelekea urahisi wa kifaa hicho kung’amua kama mtu ana virusi hivyo au laa.

Aidha, mtu atakayebainika kuwa na virusi vya Ukimwi kwa kupitia kifaa hicho atabidi aende kwenye kituo cha huduma za upimaji kwa uthibitisho zaidi kwa kufuata muongozo wa matibabu.


Fahamu:

  • “Antibodies” ni protini ambazo zinatengenezwa na seli za “Plasma” ambazo zinatumika na kinga mwili ili kushambulia vimelea vigeni kama virusi na bakteria.
  • “Antibodies” hazisababishi maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Virusi hivyo husambazwa na vimiminika vya mwili kama shahawa, majimaji ya ukeni, maziwa ya mama mwenye virusi na damu.

Hivyo ni kusemwa mtu ambaye anaishi na virusi vya Ukimwi fizi zake zitakuwa na “antibodies” nyingi kuliko kawaida ikiwa ni matokeo ya mwili kukabiliana na virusi hivyo.

Dk Benjamin amesema, kupata majibu kwa kipimo hicho, inampasa aliyekitumi kujipima kuangalia mstari/mistari ambayo itaonekana baada muda unaohitaji kutoa majibu kukamilika. 

Endapo mtu ana maambukizi ya virusi vya Ukimwi, basi kifaa cha OraQuick kitaonyesha mistari miwili myekundu na kama mtu hana, kifaa hicho kitonyesha mstari mmoja tu. 

Kupata majibu kwa kipimo hicho, inampasa aliyekitumia kujipima kuangalia mstari/mistari ambayo itaonekana baada muda unaohitaji kutoa majibu kukamilika. Picha| Mtandao.

Tanzania bado inajipanga kutumia teknolojia hiyo

Wakati Uganda ikizindua teknolojia ya OralQuick, Tanzania bado inaendelea na majaribio ya kipimo hicho ambayo yalianza tangu Aprili 2018.

Majaribio yameshafanyika katika mikoa zaidi ya 15 ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Morogoro na Arusha na hadi sasa, yanaendelea.

Kipimo hicho hakijaruhusiwa bado kutumiwa na watu kwa sababu Sheria ya Ukimwi nchini Tanzania ya mwaka 2008 inakataza  mtu kujipima mwenyewe virusi vya ugonjwa huo kabla ya kupata ushauri na nasaha kutoka kwa mtaalamu wa afya.

Licha ya sheria hiyo kuripotiwa kuwa ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa tangu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa bungeni Septemba 2019 alisema kuwa hata kama sheria ya kujipima mwenyewe ikipitishwa, italazimu mtu ajipime mbele ya mtoa huduma za afya.


Zinazohusiana


Wadau wanasemaje?

Mchoraji wa picha, Martha Ngwanda ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam. amesema kujipima mwenyewe ni vizuri endapo mtu amejiandaa kisaikolojia kwa majibu atakayoyapata. 

Licha ya kuwa kupima virusi vya Ukimwi ni hiari kuna mara kadhaa mtu anaweza kujikuta ameshinikizwa na mpenzi wake, rafiki zake na hata familia kujipima virusi hivyo na kuondoa dhana nzima ya utayari wa kisaikolojia.

Hali hiyo inaweza kusababisha sintofahamu kwa mtu endapo atapata majibu ya kuwa ameathirika.

Mwanafunzi wa masuala ya afya kutoka Chuo cha hospitali ya rufaa ya RMA mkoani Mbeya, Emmanuel Sungwa amesema “ni kweli vifaa hivi vikiruhusiwa vinaweza kufanya mapinduzi kiafya lakini mapinduzi hayo yanaweza yasiwe mazuri.” 

Sungwa amesema watu wengi hawafahamu jinsi ya kutumia vifaa hivyo na kama atutumia isivyo sahihi anaweza kupata majibu ambayo huenda siyo sahihi.

“Vile vifaa vina proces (taratibu) zake. Ukikosea kidogo tu unaweza ukajikuta kinasoma positive (chanya),” amesema Sungwa.

Dk Benjamin ambaye ni mmoja wa wataalamu wa afya ambao wanafanya majaribio ya kipimo hicho,  amesema tangu kuanza kwa majaribio nchini hakuna kesi ya aina yoyote iliyoripotiwa mpaka sasa. 

Mtu anayejipima anahitaji kukipitisha kifaa hicho kwenye fizi za juu na chini na kisha kukiweka kwenye “tube” maalumu na kusubiri kwa dakika 20 ili kupata majibu. Picha| Mtandao.

Hata hivyo, wadau hao wamesema teknolojia ni muhimu katika kutokomeza Ukimwi lakini juhudi zinatakiwa zielekezwe katika kuelimisha jamii wakiwemo vijana kujilinda dhidi ya maambukizi mapya yanayoenezwa zaidi kwa ngono zembe.  

Dk Benjamin amesema, hata wale ambao tayari wana maambukizi, wakiwahi hospitali watapata dawa za ARV ambazo zitawasaidia kuimarisha afya na kupunguza nguvu ya virusi hivyo mwilini.

Hali hiyo inaondoa uwezekano wa mtu anayeishi na Virusi vya Ukimwi kusababisha maambukizi kwenda kwa mwingine.

Enable Notifications OK No thanks