TCRA yaagizwa kutatua muingiliano wa mawasiliano ya simu mipakani
- Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.
- Amesema muingiliano wa mawasiliano na nchi jirani bado ni changamoto kubwa inayohitaji ufumbuzi.
- Amesema wameanza kuchukua hatua katika mipaka ya Kilimanjaro na Kagera.
Dar es Salaam. Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kushirikiana na mamlaka za mawasiliano za nchi jirani ili kuondoa tatizo la muingiliano wa mawasiliano ya simu katika maeneo ya mipakani.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ametoa agizo hilo Bungeni leo (Juni 24, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngara mkoani Kagera, Alex Gashaza aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la muingiliano wa mawasiliano katika meneo ya mipakani.
Mhandisi Nditiye amekiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika maeneo ya mipakani ambapo mawasiliano yamekuwa yakiingiliana kati ya nchi jirani na Tanzania.
Amesema wamechukua hatua za dharura ikiwamo kuwataka TCRA kushirikiana na nchi jirani kuangalia namna ya kulimaliza tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa baadhi ya wananchi wa mipakani.
“Tumechukua hatua za dharura kwa kuielekeza TCRA washirikiane na mamlaka za mawasiliano za nchi jirani kwa ajili ya kuhakikisha muingiliano huu unapunguzwa au kuondolewa kabisa,” amesema Nditiye.
Zinazohusiana:
- Mwakyembe aingilia kati sakata la TCRA na kampuni za visimbuzi.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
Amebainisha kuwa utaratibu huo umefanyika jijini Arusha Aprili mwaka huu kupitia kikao cha mawasilino cha Afrika Mashariki (East African Communication Organization (EACO)) ambapo wameshaweka mkakati kwa kuanzia na mikoa ya Kilimanjaro na Kagera iliyopakana na nchi za Kenya na Rwanda.
“Maeneo ya Moshi na Kagera, Vodacom wameanza kurekebisha muingiliano ili kuhakikisha kila nchi inapata mawasiliano wanayohusika nayo badala ya kufanya robbing (kuingilia),” amesema Mhandisi Nditiye.
Katika swali lake, Gashaza amesema baadhi ya maeneo katika kata za mipakani zinazopakana na nchi ya Burundi na Rwanda usikivu umekuwa ni hafifu na muingiliano wa mitandao ya nchi jirani umekuwa ukileta changamoto kwa wananchi.