Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha tiba utalii Afrika
- Zaidi ya wagonjwa 900,000 wametibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, jambo lililopunguza gharama za matibabu nje ya nchi kwa asilimia 99.
Dar es Salaam. Tanzania imeweka mikakati ya kuimarisha sekta ya afya ili kuwa kitovu cha tiba utalii barani Afrika, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yaliyofanyika leo Agosti 15,2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema tiba utalii ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele kwenye maono ya Taifa.
“Tumeshaandaa mwongozo utakaotuongoza kufanikisha tiba utalii kwa weledi,” amesema Dk. Shekalaghe, akibainisha kuwa mpango huo utahusisha hospitali za Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi, idara ya uhamiaji na Bodi ya Utalii Tanzania.
Tiba utalii (Medical Tourism) ni kitendo cha mhitaji wa tiba ya afya kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa kuvuka mipaka kwa sababu ya kufuata teknolojia ya matibabu,huduma za kibingwa, unafuu wa gharama za matibabu na muda mfupi wa kutibiwa.
Huduma hii ilianza kufanyika nchini Tanzania miaka 25 iliyopita ikiwawezesha mamia ya raia wa kigeni pamoja na wenyeji kupata matibabu ya maradhi mbalimbali.

Waziri wa Afya Jenista Mhagama alyekuwa akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26 Bungeni jijini Dodoma Juni 2 mwaka huu alisema Serikali imetenga Sh123.9 Bilioni kwa ajili ya utalii huo.
Mhagama alibainisha kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika hospitali ya Taifa, Hospitali maalum, hospitali za rufaa za kanda na hospitali za rufaa za mikoa pamoja na kuanzisha na kuimarisha huduma mpya kulingana na mahitaji ya sasa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Tiba Utalii Taifa, Abdumalik Mollel, amesema kuwa sekta ya afya nchini imepiga hatua kubwa, ikijivunia madaktari wenye ujuzi wa juu na huduma za kisasa zinazokidhi viwango vya kimataifa.
“Miaka ya nyuma wananchi walikuwa wakisafiri kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu, lakini sasa hali imebadilika. Tanzania imejipambanua kama kitovu cha tiba utalii na wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali wanakuja hapa kwa huduma bora,” amesema Mollel.
Kwa mujibu wa Mollel kwa sasa Tanzania inavutia watalii wa afya kutoka maeneo mbalimbali nje ya nchi badala ya kupeleka wagonjwa wao katika mataifa mengine hatua inayotajwa kuchangia ukuaji wake kwa asilimia kati ya nne na 15.
Latest