Tanzania, Poland kuendeleza ushirikiano maeneo ya kimkakati
- Ni pamoja na elimu, kilimo, biashara,viwanda, uwekezaji na utalii.
- Tanzania kuanza safari za ndege hadi Poland kukuza utalii.
Dar es Salaam. Tanzania na Poland zimeandika historia mpya katika kuendeleza ushirikiano kwenye maeneo ya kimkati ikiwemo biashara na utalii ili kuchochea ukuaji wa uchumi baina ya mataifa hayo.
Rais Samia Suluhu aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Februari 9, 2024, mara baada ya kumpokea Rais wa Poland Andrzej Duda aliyepo nchini kwa ziara ya kitaifa, amesema hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa nchi hiyo kutembelea Tanzania licha ya uhusiano uliodumu tangu mwaka 1962.
“Hii ni ziara ya kihistoria…ni kwa mara ya kwanza Rais wa Poland anafanya ziara ya kitaifa hapa nchini Tanzania…
…Ziara hii ni kielelezo cha urafiki na ushirikiano baina ya nchi zetu mbili uliodumu tangu mwaka 1962,” amesema Rais Samia Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa maeneo ya kimkakati yaliyotajwa na Rais Samia ni pamoja na elimu,kilimo, biashara,viwanda, uwekezaji na utalii, madini, gesi asilia, uchumi wa buluu, pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Kwa mujibu wa Tovuti ya Report Linker, Poland ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika eneo la tehama ikihika nafasi ya 18 kati ya nchi zote duniani.

Rais wa Poland Andrzej Duda akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam.Picha|Ikulu Mawasiliano
Tovuti hiyo inabainisha kuwa mwaka 2021 nchi hiyo iiingiza Sh 27.1 trilioni kutokana na kuuza Tehama katika nchi nyingine fedha ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi Sh133.2 trillioni mwaka 2026.
Huenda ushirikiano baina ya Poland na Tanzania ukaongeza nguvu katika jitihada za Serikali kukuza Tehama ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia duniani.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Poland kupitia wakala wa mikopo ya usafirishaji imetoa bima kwa benki za biashara zitakazosaidia kuendeleza awamu ya tatu na ya nne ya ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.
Kiongozi huyo amesema ufadhili huo utawezesha kukamilika kwa wakati kwa reli hiyo katika vipande vya Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Lusaka.
Soma zaidi:Rais Samia amteua Badru kuongoza PSSSF, HESLB ikipata bosi mpya
Utalii biashara na uwekezaji kuimarika
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa mahusiano ya mataifa hayo katika sekta ya utalii yataendelea kuimarishwa zaidi ili kuvutia wataliikutoka nchini humo ambapo takwimu za mwaka 2023 zinabainisha kuwa nchi hiyo imeshika nafasi ya saba katika orodha ya mataifa yanayoingiza watalii nchini.
Ili kurahisisha shughuli za utalii baina ya nchi hizo, Rais Samia amewaambia wanahabari kuwa amewasilisha ombi la kuanzishwa kwa safari za ndege za Tanzania zitakazoenda moja kwa moja mpaka Poland.
“Tumewaelekeza wataalamu wetu kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za moja kwa kutoka Tanzania na tumeweka ombi letu kwa msisitizo mkubwa kwa wenzetu wa poland,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Rais wa Poland Andrzej Duda, amesema amefurahishwa na ziara yake nchini Tanzania na kwamba anatumaini kwamba itaimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
“Kazi tunayoifanya leo katika kuimarisha mahusiano kati ya poland na Tanzania italeta matunda katikanchi zetu zote mbili,” amesema Rais Duda.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland umeimarishwa kwa kiasi kikubwa baada ya kubadilishwa kwa Sera ya Mambo ya Nje nchini Poland ili kulenga zaidi bara la Afrika tangu mwaka 2013.
Mabadiliko hayo yalilenga kuanzishwa na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Latest