Tanzania mguu sawa Sensa ya Watu na Makazi
- Majaribio kufanyika Agosti 20 na 21 mikoa 18 nchini.
- Wananchi waendelea kuhamasishwa kushiriki zoezi hilo.
- Vijiji, mitaa itakayoshiriki yatajwa.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema kuwa tayari imekamilisha mchakato wa mitaa na vijiji vitakavyoshiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajia kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23 leo Juni 7, 2022 bungeni jijini Dodoma amesema hadi kufikia Aprili 22 mwaka huu vitongoji vyote 64,318 na mitaa 4,670 Tanzania bara imetengwa kwa ajili ya zoezi hilo.
Kwa upande wa Zanzibar jumla ya maeneo 4,313 ya kuhesabia watu kutoka shehia (Kata) 388 yametengwa sawa na asilimia 100 ya lengo.
“Kazi nyingine zilizokamilika ni kuandaa madodoso ya sensa ya watu na makazi, sensa ya majengo, sensa ya anwani ya makazi, miongozo ya fomu za kudhibiti ubora, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji,” amesema waziri huyo.
Zoezi hilo muhimu linalofanyika kila baada ya miaka 10 litatunguliwa na sensa ya majaribio itakayofanyika Agosti 20-21 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Sambamba na hilo Serikali inaendelea na mchakato wa kununua vifaa vya sensa na kuandaa rasimali watu katika maeneo husika.
Soma zaidi:
Aidha, Waziri Nchemba ameendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza wakati wa sensa kwani jambo hilo lina umuhimu kwa maendeleo ya nchi.
Baadhi ya wabunge wamepongeza serikali kwa kuendelea na maandalizi ya sensa lakini wamehoji uwepo changamoto kwa watakaotumika kufanya kazi ya sensa kwani baadhi ya watu wanaochaguliwa kufanya kazi ya sensa hawana weledi ya kiutumishi.
“Tumeona kwenye postikodi, kule kwetu kuna asilimia imetekelezeka kwa utendaji mzuri , kuna asilimia imefeli……mtu hana weledi wa kiutumishi anapewa kazi kwa kuwa ina posho ataomba,” amesema Jerry Slaa,Mbunge wa Ukonga
Aidha Mbunge Slaa amependekeza walimu wapewe kipaumbele katika kazi hiyo kwa sababu wana uzoefu katika utumishi.