Tanzania kuondoa kodi, ushuru wa vifaa tiba vya Corona

June 11, 2020 3:02 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Michango yote inayotolewa kupambana na Corona haitatozwa kodi.
  • Ushuru wa forodha wa vifaa vya Corona kupunguzwa hadi asilimia 0. 

Dar es Salaaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amependekeza vifaa tiba na michango inayotolewa na wananchi kwa Serikali katika kipindi hiki cha ugonjwa wa virusi vya Corona hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo.

Dk Mpango aliyekuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali leo (Juni 11, 2020) bungeni amesema lengo ni kuwezesha upatikanaji vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa gharama nafuu na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa hivyo na bidhaa nyingine hapa nchini. 

“Napendekeza pia michango iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) isitozwe kodi hadi hapo Serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huu,” amesema Dk  Mpango.

 Aidha, waziri amependekeza kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana COVID19.

Vifaa hivyo ni pamoja barakoa (Masks), kipukusi (sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators), na mavazi maalum ya 85 kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE). 

“Msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “duty remission”. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo,” amesema Dk Mpango. 

Hatua hiyo inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo.

Serikali pia imependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa msamaha kwenye madawa na vifaa muhimu vinavyotumika kupima, kukinga, kutibu na kupambana na mlipuko wa magonjwa kama vile COVID- 19.

Dk Mpango amesema hatua hii inalenga kutoa unafuu wa bidhaa hizo ili kurahisisha mapambano na udhibiti wa magonjwa hayo pindi yanapojitokeza;

Amesema tathmini ya kiuchumi iliyofanyika kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2020 inaonesha kuwa tofauti na nchi nyingi ambazo uchumi wao umeporomoka, kwa upande wa Tanzania athari za COVID-19 kwenye uchumi ni ndogo. 


Soma zaidi:


Fursa zilizojitokeza Kutokana na COVID-19 

Pamoja na athari zilizojitokeza, Dk Mpango amesema zipo pia fursa kadhaa zilizoambatana na janga hili zikijumuisha kuongezeka kwa matumizi ya njia za mtandao katika shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano, miamala ya fedha kwa njia za kielektroniki na matumizi ya tiba asili.

Pia COVID-19 imefungua fursa za kuongeza uzalishaji viwandani na kuuza mazao ya chakula katika masoko ya kikanda; na kupungua kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji viwandani kutokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta. 

“Aidha, janga hili limetupa fundisho la umuhimu wa kutumia mikakati inayoendana na mazingira yetu katika kukabiliana na majanga badala ya kuiga mikakati ya nchi nyingine.

“Vile vile, COVID-19 imetukumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa uzalishaji wa mahitaji ya bidhaa muhimu hapa nchini,” amesema Dk Mpango. 

Enable Notifications OK No thanks