Tanzania, Namibia kufufua upya ukurasa wa ushirikiano

May 28, 2019 7:16 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais John Magufuli akipokelewa na mwenyeji wake, rais wa Namibia, Dk Rage Geingob alipowasili nchini humo kwa ajili ya ziara rasmi ya siku mbili. Picha|Mtandao.


  • Rais Magufuli aagiza kamati ya pamoja ya Tanzania na Namibia (Joint Permanent Commission -JPC) kukutana ndani ya miezi miwili. 
  • Kamati hiyo haijakutana tangu mwaka 1999.
  • Akiwa Namibia, Rais Magufuli ameshuhudia kufunguliwa kwa mtaa wenye jina la Baba wa Taifa Julius K. Nyerere. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaagiza mawaziri wa Tanzania kuitisha kikao cha Kamati ya  Pamoja ya  Tanzania na Namibia (Joint Permanent Commission -JPC) ndani ya kipindi cha miezi mwili ili kujadiliana juu ya fursa mbalimbali za ushirikiano wenye manufaa kwa nchi hizo.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana (Mei 27, 2019) wakati wa mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dk Rage Geingob yaliyofanyika katika Ikulu ya Windhoek nchini Namibia ambako yuko katika ziara ya kitaifa ya siku mbili. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya yeye na Rais Geingob kupokea taarifa kuwa kikao cha JPC hakijafanyika tangu mwaka 1999 na kusababisha masuala mengi ikiwemo ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kutopata msukumo wa kutosha. 

“Licha ya uhusiano wa kihistoria na kidugu wa Tanzania na Namibia ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Namibia Sam Nujoma, nchi hizo zimekuwa na kiwango cha chini cha ushirikiano wa kibiashara baina yake.

“Katika  mwaka uliopita biashara iliyofanyika ilikuwa na thamani ya Sh59.556 bilioni tu na kwamba nchini Tanzania kuna kampuni mbili tu za Namibia zinazofanya biashara,” inasomeka taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa. 

Pamoja na kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli amemshukuru mwenyeji wake Rais Geingob kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya Kitaifa nchini Namibia na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika hasa katika  masuala ya kilimo, ufugaji, utalii, usafiri wa anga, biashara, uwekezaji na utamaduni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Magufuli ameserna kwa kutambua uhusiano wa kihistoria na kidugu Tanzania inakamilisha maandalizi ya kufungua Ubalozi wake Jijini Windhoek ili kurahisisha masuala mbalimbali ya uhusiano, hususan katika uchumi ambayo yapo nyuma. 


Zinazohusiana:


Kwa upande wake, Rais Geingob amemshukuru Rais Magufuli kwa kufanya ziara hiyo ambapo amesema Namibia inatambua na kuenzi mchango mkubwa wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere na Watanzania katika juhudi za ukombozi wa Namibia. 

Amefafanua kuwa wakati wa kupigania uhuru wa Namibia, wapigania uhuru wa nchi hiyo walipata nafasi ya kuweka kambi yao huko Kongwa mkoani Dodoma.

Licha ya kuweka makazi yao kwa ajili ya harakati hizo, amesema walisaidiwa kupata rnafunzo ya kijeshi na waliishi vizuri na wananchi wa eneo hilo jambo ambalo hawatasahau. 

Rais Geingob amesisitiza umuhimu wa kutekeleza makubaliano yatakayowekwa katika kikao cha JPC na kwamba Namibia ipo tayari kutekeleza kwa maslahi ya Wanamibia na Watanzania. 

Akiwa nchini humo, Rais Magufuli ameshuhudia kufunguliwa rasmi kwa mtaa uliobadilishwa jina kupewa jina la Julius K Nyerere ili kuenzi mchango wake katika ukombozi wa Namibia. 

Enable Notifications OK No thanks