St. Francis yavunja rekodi yake yenyewe kidato cha nne 2019
- Wanafunzi 57 kati ya 91 wamepata daraja la kwanza la alama 7 kutoka wanafunzi 41 mwaka juzi.
- Waifunika shule ya kwanza kitaifa ya Kemobos kwa kuwa kiwango hicho cha daraja la kwanza.
Dar es Salaam. Ukiwa ni mwaka wa nane mfululizo, Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis imeweza kubaki katika ubora ule ule ambao shule zingine zaidi ya 3,000 Tanzania zimeshindwa kufikia baada ya kung’ang’ania katika shule 10 bora huku ikivunja rekodi yake yenyewe ya kuwa na wanafunzi wengi waliopata daraja la kwanza la alama saba.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) ya mwaka 2019 jana (Januari 9, 2020) Jijini Dar es Salaam, wanafunzi wote waliofanya mtihani katika shule hiyo wamepata daraja la kwanza huku takriban theluthi au wawili kati ya watatu wakipata alama saba ambazo ni za juu zaidi.
Uchambuzi wa matokeo hayo uliofanywa na www.nukta.co.tz unabainisha kuwa St. Francis kama wanavyoitwa kwa kimombo wamevunja historia yao wenyewe baada ya wanafunzi 57 kati ya 91 kupata alama saba ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 16 zaidi ya waliopata kiwango hicho mwaka 2018.
Mwaka 2018, shule hiyo pia ilikuwa na idadi ya wanafunzi 91 sawa kabisa na walioketi kufanya mtihani huo mwaka jana. Ufaulu wa kiwango hicho cha alama saba ndiyo wa juu zaidi kufikiwa na shule za sekondari mwaka 2019.
Hata shule ya kwanza kitaifa katika mtihani huo mwaka jana ya Kemebos ina jumla ya wanafunzi 35 waliopata daraja la kwanza la alama saba kati ya wanafunzi 70 waliofanya mtihani huo. Wanafunzi wote wa Kemebos kama ilivyo St Francis wamapata daraja la kwanza.
Shule hiyo pia imetoa wanafunzi sita walioingia katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa na Mwanafunzi wa kwanza kitaifa. Picha|Mtandao
Uchambuzi zaidi wa matokeo ya St Francis unaonyesha kuwa wanafunzi 13 wa shule hiyo wamepata daraja la kwanza la alama nane huku wa mwisho katika shule hiyo akiwa na daraja la kwanza la alama 17.
Shule hiyo ya Wasichana ya Mtakatifu Francis sio tu kwamba imefaulushi wanafunzi wote katika daraja la kwanza lakini hata katika somo moja moja imefanya vizuri zaidi kuliko shule yoyote kitaifa.
Katika masomo 10 ambayo wanafunzi walifanya mtihani masomo 7 wameshika nafasi ya kwanza katika masomo ya Kemia, Phizikia, Biolojia,Kiingereza ,Kiswahili, Bible Knowldge na Jiografia huku masomo ya Uraia (Civis) ikishika nafasi ya pili ,somo la historia nafasi saba na hesabu na fasi ya nne kitaifa.
Lakini ufaulu huo wa haukuja kwa kubahatisha kwani katika mitihani wa taifa wa kidato cha pili mwaka 2017 darasa hili wanafunzi wote 92 waliofanya mtihani walipata daraja la kwanza huku wanafunzi 91 wakipata daraja la kwanza alama ya 7 na mmoja daraja la kwanza alama ya 11.
Zinazohusiana
- Necta yatangaza matokeo kidato cha pili, nne 2019
- Matokeo kidato cha nne haya hapa
- Shule 10 bora zilizotikisa matokeo kidato cha nne 2019
Siri ya ushindi wa St. Francis
Akiongea na Nukta (www.nukta.co.tz), Mkuu wa shule ya St. Francis Girls, Mtawa Veena Vas amesema wanafunzi wake kabla ya kufanya mtihani waliahidi ushindi na wameipatia ushindi shule hiyo.
Vas amesema siyo kusoma pekee ndiyo kumeipatia shule hiyo ushindi bali nidhamu pamoja na kujituma bila mipaka ndiko kumewapatia wasichana wote wa shule hiyo ufaulu wa daraja la kwanza.
“Ufaulu kwa daraja la A shuleni kwetu ni alama 81 na hata mitihani ambayo tunayowapatia wanafunzi ni migumu. Wanapokuja kwenye ufaulu wa Necta ambao daraja la A linaanzia alam 75 inakuwa ni rahisi kwao” amesema Vas.
Pia Vas ameongeza kuwa wanafunzi wa shule hiyo wanasoma kwa makundi ili wasaidiane na kuwawezesha wote kufanya vizuri katika masomo yao.
“Wanafunzi hawajafanya haya peke yao. Waalimu wamefanya kazi kubwa lakini pia na wazazi wametoa ushirikiano mkubwa. Wamekuwa wepesi wakiitwa shuleni kwa makosa ya kinidhamu,” amesema Vas.