St. Francis Girls yavunja rekodi nje, ndani
- Karibia nusu ya watahiniwa wake katika matokeo ya mwaka 2018 wamepata daraja la kwanza la juu la alama saba.
- Shule hiyo na Marian Boys ya mkoa wa Pwani hazijawahi kutoka 10 bora kwa miaka saba mfululizo.
- St Francis imetoa changamoto kwa shule nyingine kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kuongeza ubora wa ufaulu.
Dar es Salaam. Ni miaka saba sasa wamebaki katika ubora ule ule bila kushuka. Ni wanafunzi wa shule ya St. Francis Girls ya jijini Mbeya waliodhihirisha ubora wao katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mtihani la Tanzania (Necta) jijini Dodoma jana (Januari 24, 2019), St Francis imefanikiwa kuingia katika orosha ya shule 10 bora baada ya kuwa ya kwanza kitaifa.
Shule nyingine zilizofanikiwa kuingia 10 bora ni Kemebos ya mkoani Kagera, Marian Boys (Pwani), Ahmes (Pwani) na Canossa (Dar es Salaam). Shule nyingine ni Maua Seminary (Kilimanjaro), Precious Blood (Arusha), Marian Girls (Pwani), Bright Future Girls (Dar es Salaam) na Bethel Sabs Girls (Iringa).
St. Francis Girls imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wote 91 waliofanya mtihani huo kwa daraja la kwanza ikivunja rekodi ya mwaka 2017. Katika mtihani wa mwaka juzi, wanafunzi 92 walifanya mtihani lakini kati ya hao 91 walipata daraja la kwanza na mmoja tu alishika mkia kwa kuambulia daraja la pili.
Hata hivyo, katika matokeo yaliyotangwa jana kati ya watahiniwa 91 waliofanya mtihani huo, 41 wamepata daraja la kwanza la alama saba ikiwa na maana wanafunzi wote walipata alama A kwa masomo saba ya awali ambayo hutumika na Necta kutengeneza madaraja.
Kwa ufaulu huo, karibia nusu ya watahiniwa hao wamepata daraja hilo ambalo ni la juu zaidi katika mpangilio wa ufaulu.
Mafanikio ya shule hiyo siyo ya kubahatisha, imekuwa ikitikisa kwa muda mrefu katika sekta ya elimu nchini.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta kwa miaka saba iliyopita yaani tangu mwaka 2012 hadi 2018 umebaini kuwa katika kipindi hicho takriban wanafunzi 627 wamehitimu kidato cha nne katika shule hiyo lakini ni wawili tu waliowahi kupata daraja la tatu.
Zinazohusiana:
- Wadau wa elimu watoa neno udangajifu matokeo kidato cha nne 2018
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?
Miaka mingine kama mwaka 2012 hakukuwa na daraja la kwanza lenye alama saba, mtahiniwa aliyefanya vizuri zaidi alipata daraja la kwanza lenye alama nane. Mwaka uliofuatia wa 2013 ufaulu ukaongezeka ambapo alijitokeza mtahiniwa mmoja tu aliyepata daraja la kwanza lenye alama saba.
Mwaka 2016 watahiniwa sita wakaibuka tena na kupata daraja la kwanza lenye alama saba, lakini mwaka 2018 umevunja rekodi kwa kuwa na watahiniwa wengi waliopata alama za juu zaidi. Kwa uchambuzi huo, St Francis hapana shaka St Francis imevunja rekodi yake yenyewe na nje kwa maana ya ngazi ya kitaifa.
Majengo ya shule ya St. Francis ya jijini Mbeya ambayo inakimbiza katika mitihani ya kidato cha nne kila mwaka. Picha| Mtandao.
Upekee mwingine ni kuwa shule hiyo na shule ya Marian Boys ndiyo shule pekee ambazo hazijawahi kutoka katika orodha ya 10 bora kitaifa katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Marian Boys wameendelea kutoa ushindani kwa St. Francis Girls ambapo mwaka 2012, watahiniwa 90 waliofanya mtihani wa kidato cha nne, 75 walipata daraja la kwanza huku wanafunzi 14 wakipata daraja la pili na wanafunzi mmoja akipata daraja la tatu.
Hali hiyo ilijitokeza tena mwaka unafuata mwaka 2013 ambapo kati ya wanafunzi 90 waliofanya mtihani wanafunzi 81 walipata daraja la kwanza, nane walipata daraja la pili huko mmoja akiambulia daraja la tatu la alama 25.
Upekee mwingine wa shule hiyo ni kuwa tangu mwaka 2014 hadi mwaka 2018 haijawahi kupata mwanafunzi wenye daraja la tatu. Wanafunzi wote walikuwa wakipeta katika daraja la kwanza na la pili. Pia nusu ya wanafunzi walioingia 10 bora katika matokeo ya haya (2018) wanatoka katika shule hiyo.
Shule hizi zinaweza kuwa mfano mzuri wa kuigwa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa shule nchini zilizofanikiwa kuwekeza katika miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji, jambo linalowapa wanafunzi fursa ya kupata maarifa na ujuzi kuwawezesha kujibu mtihani vizuri.
Mwishoni mwa Desemba mwaka jana, uongozi wa shule hiyo walinukuliwa na Clouds Media kuwa baadhi ya mbinu zinazosaidia wanafunzi kufauli vizuri ni kuwafundisha kujitambua, kumcha Mungu, bidii kwenye masomo, kuwa na ndoto na nidhamu bora.
Hata hivyo, St. Francis itaendelea kuvunja rekodi mwaka 2019? Lini shule za umma zitaipiku St Francis katika nafasi hiyo na kuibuka nafasi za juu zaidi katika orodha za shule bora nchini?
Latest