Siri za ushindi mwanafunzi bora kidato cha nne mwaka 2019
- Ni Joan Ritte aliyetangazwa na Necta kuwa mwanafunzi bora kitaifa kidato cha nne mwaka 2019
- Tangu akiwa elimu ya msingi yeye ni kupasua tu.
- Baba yake asema mwanaye “amemrudishia fadhila za kumlea”.
- Malengo yake ni kuwa mhandisi ujenzi akihitimu elimu ya juu.
- Amesema ufaulu wake ni salamu kwa wasichana kuwa wakiamua wanaweza
Dar es Saaam. Unaweza kudhani binti huyo alipanda “School bus” akiwa shule ya msingi yaani kuwa alisoma shule binafsi zenye sifa kede kede za ufaulu na huduma za kisasa. Kama wewe ni miongoni waliodhani hivyo, badilisha mtazamo.
Joan Ritte, binti ambaye ndiye habari ya mjini nchini Tanzania kwa sasa baada ya kuibuka kuwa mwanafunzi bora wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2019, alisoma shule ya kawaida ya msingi ya umma maarufu “kidumu na mfagio” huko mkoani Kilimanjaro.
“Mimi nimesoma shule za kawaida kabisa,” Ritte ameiambia Nukta Habari (nukta.co.tz) huku akitabasamu na kuongeza;
“Nimesoma Shule ya Msingi Muungano.”
Joan ametangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Dk Charles Msonde kuwa ndiye mwanafunzi bora kitaifa kwa mwaka 2019 baada ya kuwashinda wenzie zaidi ya 400,000 waliofanya mtihani huo mwishoni mwa mwaka jana.
Binti huyo, aliyesoma Shule ya Sekondari ya St Francis, amefaulu kwa daraja la kwanza kwa kupata alama A ama “banda” kama vijana wanavyoita katika masomo yote. St Francis imekuwa ya pili kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana nyuma ya Kemebos ya Kagera.
Ufaulu huo wa Joan si wa bahati mbaya. Katika mtihani wa darasa la saba, Joan alifaulu kwa alama A pia licha ya kusoma shule ya umma.
Hapana shaka binti huyu ni nondo yaani yupo vizuri kichwani. Uchunguzi wa matokeo yake ya kidato cha pili unaonesha kuwa alipata daraja la kwanza kwa masomo yote 10 aliyoyafanya.
Joan amesema kumtegemea Mungu na kuwa na nidhamu ni kitu kilicho chochea mafanikio yake. Picha| Joan Ritte.
Namna alivyovipiga bao vichwa 340,913 vilivyofaulu mtihani wa kidato cha nne 2019
Joan amesema safari yake haikuwa rahisi. Hata alipokuwa kwenye mstari wa kukaguliwa kuingia kwenye chumba cha mtihani alioufanya, hakuwaza kama ataongoza kitaifa kwenye matokeo hayo.
Mawazo yake yaligubikwa na kubadilika kwa mfumo wa mtihani. Licha ya walimu wa Shule ya St. Francis kujitahidi kuwaweka wanafunzi kwenye hali ya utulivu, bado alijiuliza maswali yaliyokosa majibu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo yake, kumtegemea Mungu, juhudi na kuisikiliza walimu ndicho kilichomsaidia.
“Unaweza ukiamua. Mkono wa Mungu ukiwa ndani yako unaweza kufanya lolote. Mwaka huu tumepitia kipindi kigumu cha kubadilishwa kwa mfumo wa mtihani. Jinsi maswali yalivyokuja ni tofauti na ambavyo tumezoea maswali kwenye mitihani yetu awali,” amesema binti huyo kwa sauti ya kujiamini.
Watanzania wategemee nini kutoka kwa Joan?
Kichwa cha Joan siyo cha mchezo mchezo kwani amesema kati ya masomo yote, analipenda somo la fizikia. Licha ya kwamba Kemia, Hesabu na Baiolojia yalikuwa kwenye masomo yake pendwa, binti huyu amesema alikuwa na wasiwasi kama angeweza kulifauru Fizikia kwa alama ya A.
Hata hivyo, kufaulu somo hili na mengineyo kunazidi kumpeleka kwenye ndoto yake ya kuwa mhandisi wa majengo yaani ”Civil Engeneer” kwa kimombo. Uhandisi majengo ndiyo fani anayotaka kuifanya akihitimu masomo yake ya elimu ya juu.
“Kazi ya uhandisi itanifanya kuwa mfano wa kuigwa kwani nitawaonyesha wasichana kuwa inawezekana kusoma hata masomo ambayo yanadhaniwa kuwa ni wanaume pekee,” amesema Joan.
Licha ya kwamba wasichana wengi huogopa masomo haya, Joan ambaye anatazamia kusoma tahasusi ya masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM) akiingia hatua ya kidato cha tano na sita, amesema kwake siyo tatizo kwa kuwa anaamini hiyo ndiyo njia ya kuwa mfano kwa wasichana wa Tanzania.
Our very own Joan… #T1♥️
Jinsi simu ziko busy kwa Ritte’s 🙌 … God thank you. pic.twitter.com/ms7uIUPOqx— RitteRingSling&Wrap (@janecritte) January 9, 2020
Joan ameusifu uongozi wa shule hiyo iliyopo mkoani Mbeya kwa kuwafundisha masomo na nidhamu.
“Uongozi wa shule umetupokea kwa madhaifu na mapungufu yetu. Matokeo yetu ya kidato cha pili 2017 hayakuwa mazuri. Tulitamani wote kuwa na daraja la kwanza lakini haikuwezekana,” amesema huku akionekana kutoridhishwa na walichofanya wakiwa kidato cha pili.
Joan amesema japo hafahamu maisha yake ya mbele na nini amepangiwa na Mungu, atasoma zaidi ili kubaki kuwa mfano wa kuigwa.
“Ufaulu huu umenionyesha kuwa ninaweza na kwamba kila mtu anaweza. Napenda matokeo yangu haya yatumike kama chachu hasa kwa wasichana ambao wanaogopa kwa kujiona duni mbele ya wavulana,” amesema Joan.
Binti huyo anayeishi Kilimanjaro, ameshauri Serikali, walimu na wadau wa elimu kutilia mkazo malezi kwa watoto na angefurahi kama yangeazia nyumbani kwenye ngazi ya familia.
Amesema wanafunzi wengi wanashindwa kufikia malengo na ufaulu mzuri kwa sababu wengi wao huishia kuingia kwenye makundi yasiyofaa kutokana na harakati zaukuaji.
“Endapo baba na mama nyumbani watashirikiana na walimu shuleni, watoto watafaulu bila mashaka,” amesema Joan huku akishukuru jitihada za wazazi wake pamoja na walimu na jamiii ya Shule ya St. Francis.
Baba mzazi wa binti huyo William Ritte amesema Joan siyo wa kwanza kutikisa Taifa kwenye familia hiyo kwani mwaka 2014, dada yake na Joan, Catherine Ritte alishika nafasi ya tisa kitaifa kwa wasichana.
Zinazohusiana
- Necta yatangaza matokeo kidato cha pili, nne 2019
- Matokeo kidato cha nne haya hapa
- Shule 10 bora zilizotikisa matokeo kidato cha nne 2019
Huenda unahisi Joan anakesha na madaftari kila wapo nyumbani lakini Ritte amesema ni ajabu kwa kuwa binti huyo anafanya kazi zote awapo nyumbani.
“Akiwa nyumbani anafanya kazi zote za nyumbani. Anapika, anafanya usafi na anafanya usafi wa mazingira,” amesema Ritte huku akiongeza kwa kusema “Joan amenirudishia fadhila kwa yote ambayo nimemfanyia tangu nimeanza kumlea,”
Ushauri wa Ritte kwa wazazi wenzake ni kwamba, wajitahidi kuwasikiliza watoto wao hasa kwenye masuala ya kimasomo. Na wasisite kuwapongeza pale wanapofanya vizuri.
Uongozi wa shule unafurahia mafanikio ya wanafunzi wake akiwemo Joan.
Mkuu wa Shule ya St. Francis Girls, Mtawa Veena Vas amesema kwamba Joan na wenzie wa shule hiyo husoma sana na bado walimu pamoja na wafanyakazi wa shule hiyo wanatilia mkazo nidhamu na kujituma.
“Hatupendi Ufaulu wa daraja B shuleni kwetu. Daima tunapenda kuwafundisha wanafunzi wetu kuwa bora darasani na hata maishani,” amesema Mtawa Vas.