Siri iliyofichika watoto mapacha kuhusishwa na “mikosi” Kanda ya Ziwa-2

November 20, 2020 8:17 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Matambiko na gharama zake hutegemeana na aina ya mapacha waliozaliwa. 
  • Baadhi ya watu wanaofanya matambiko hayo, wanaamini kuwa ni njia sahihi kufanikiwa katika maisha.

Mwanza. Tunaendelea na simulizi yetu ya matambiko kwa mapacha na leo tunaangazia aina za mapacha na matambiko wanayopaswa kufanyiwa ili kuwaondolea kinachodaiwa kuwa ni mikosi kwa familia zao. 

Ukiachilia mbali mapacha wawili maarufu kwa jina la Kulwa na Doto, lakini pia wapo mapacha watatu ama wanne wanaozaliwa kwa siku moja.

Lakini katika kabila la Wasukuma, yupo ‘pacha mmoja’ ambaye ndiye anatajwa kuwa “hatari zaidi” kwenye familia ambaye huitwa Kashinje kama nilivyokueleza hapo awali.

Mtoto huyu Kashinje huzaliwa akiwa ametanguliza miguu ama makalio, yeye huaminika kuwa ujio wake ni “laana” kwenye familia, nadharia ambayo wataalamu wa afya na viongozi wa dini wanapingana nayo. 

Kwa mujibu wa Mtemi Mkwaga, Kashinje ndiye mkuu wa mapacha na hata matambiko yake huwa ni tofauti na matambiko ya watoto wawili mapacha.

“Watoto hawa huzaliwa wakiwa na joto (Wasebu) na ndiyo sababu ya wao kuleta athari kwenye familia na ndio maana tunawafanyia mila hizo ili kupunguza baadhi ya matatizo.  

“Na mtoto huyu anatakiwa kuanza kufanyiwa tambiko siku tu anapozaliwa ili kudhibiti hiyo mizimu inayoweza kuiandama familia kwani wazazi wasipotekeleza hilo matokeo yake huwa ni mabaya sana,” anasema Mtemi huyo katika maongezi yetu wakati sherehe ya Wakango ikiendelea. 

Mtemi huyo ambaye anaheshimika kwenye jamii, anasema hata hospitalini, huwa wanawaambia wakunga na wauguzi kumuangalia kwa makini Kashinje wanapozaliwa ili  anapotoka wodini waweze kumfanyia tambiko na mila. 

Hata hivyo, Mtemi Mkwaga ananidokeza  kuwa matambiko yao hufanyika kwa “kumuomba mwenyezi Mungu na si vinginevyo”.

Mzee Masomi Shibiriti na mkewe, Tabu Shibiriti wanavalishwa shanga ikiwa ni ishara ya kukaribishwa kwenye chama cha Wakango. Shanga hizo huvalishwa muda mfupi baada ya kufanyiwa tambiko lingine la kuogeshwa dawa mapema asubuhi. Picha|Mariam John. 

Shibiriti asimulia mikasa iliyomkuta

Baada ya maongezi yangu na Mtemi Mkwaga, narudi tena kwa Mzee Shibiriti ambaye ananieleza kwa kina mambo anadai alikutana nayo miaka 37 baada ya kupata watoto mapacha.

“Uzao wangu ulikuwa wa kawaida, lakini uzao wa nne nilijaaliwa kupata mapacha na ndipo historia ya maisha yangu ilipobadilika, kwa kuwa nilikuwa na mali nyingi zikaanza kupukutika na sikujua ziliishaje.

“Wengi walinishauri kwenda kwenye nyumba za ibada, nilisali pale miaka mingi lakini hali ilizidi kudidimia,” anasema Mzee Shibiriti ambaye shughuli za tambikoilikuwa ikifanyika nyumbani kwake.

Kabla hajafanikiwa kupata uzao huo, anaeleza kuwa alikuwa na ng’ombe zaidi ya 50 na alifanikiwa kupata mazao mengi ya chakula kwenye shughuli zake za kilimo lakini alipopata mapacha mambo yalibadilika. 

“Ujio wa mapacha hawa ulibadili historia ya maisha yangu, wazee wa mila za kisukuma walinishauri kufanya tambiko lakini sikuweza kutokana na kutofautiana kiimani na ndugu wengine.

“Lakini kadiri hali ilivyozidi kuwa mbaya nikaamua kukubaliana nao na hatimaye leo nafanya tambiko la kuondoa mikosi,”  anasema  Shibiriti katika sherehe hizo.

Mzee huyo anasema uamuzi wa kufanyiwa tambiko na kuingia kwenye jamii ya Wakango ni kuhakikisha familia yake inakuwa na amani lakini pia watoto wake waweze kupata maendeleo.

“Kwa sasa watoto wamedumaa kimaendeleo kila wanachogusa hakifanikiwi, hivyo familia tumeshauriana tukaona ni vema tuangalie upande wa pili huenda ndiko tulikokwama,” anasema mzee huyo ambaye anaonekana mwenye furaha.


Soma zaidi:


Kuithibitisha kauli ya Shibiriti nakutana na Mkango mwingine, Elizabeth Masanyiwa yeye ni mama wa watoto 12, kati ya hao nane ni mapacha. 

Mama huyo alizaa mapacha mara nne na watoto wanne wasiokuwa mapacha.

Alijiunga na jamii ya Wakango mwaka 2001 baada ya kufanikiwa kuzaa pacha aliyetanguliza makalio yaani Kashinje ambaye anadai kuwa “alileta tabu nyingi kwenye familia.

“Nilikuwa na mifugo nikaanza kuona inakufa tu bila sababu, watoto niliotangulia kujifungua wakawa wanakufa na mpaka kufanya tambiko tayari nilikuwa nimezika watoto watatu,” anasema Masanyiwa.

Masanyiwa anabainisha kuwa baada ya kufanikiwa kujiunga na chama hicho, matatizo yote yaliisha na sasa yuko huru.

Shamra shamra zinaendelea kwenye sherehe hiyo ambayo inaongeza wanachama wapya wa Wakango, bado napata kiu ya kuongeza na washiriki mbalimbali ili kufahamu kwa undani imani waliyonayo Wakango. 

Mkango mwingine niliyefanikiwa kuzungumza naye ni Deus Masheku baba wa mtoto mmoja pacha ambaye Kulwa alitangulia mbele za haki, yeye anasema alimlea mwanae vizuri na alipofikisha umri wa kuoa, hakufanikiwa kupata mtoto na ndoto za kupata wajukuu zikafifia. 

Lakini alipomfanyia tambiko, Masheku anasema mtoto wake amefanikiwa kupata watoto wawili baada ya kukaa kwenye ndoa kwa miaka miwili bila kupata mtoto.

Baadhi ya waalikwa waliohudhuria sherehe za tambiko wakichinja vitoweo vyao ambapo pamoja na mambo mengine baadhi ya vitoweo kama mguu mmoja wa mbuzi, kondoo au ng’ombe, kichwa, bandama, nusu ubavu, na viungo vingine vya tumboni huchukuliwa na wakango, na zoezi hili hufanyika kwa waalikwa wote waliofika eneo la tukio. Picha|Mariam John.

Watoto wa Shibiriti wakubali yaishe

Simulizi ya mzee Shibiriti ikaniongezea hamasa na shauku ya kutaka kufahamu zaidi kutoka kwa watoto wake mapacha na kwa haraka haraka nampata pacha wake mmoja wakati akitoka nje usiku kwenda maliwatoni. 

Kiutaratibu, wakati wote wa shughuli ya tambiko katika siku ya kwanza, mapacha hawa hawaruhusiwi kutoka nje, hivyo hata kuonana naye ilikua ni kwa usiri mno. 

Dotto Masomi (37) yeye pamoja na ndugu yake Kulwa wanaunga mkono maamuzi ya wazazi wao kufanyiwa tambiko kwa sababu wanaamini kukosa kwao mafanikio ni “kwa sababu wana laana”.“Kulala njaa kwetu ilikuwa kawaida, tumesoma kwa shida na hata mwaka ukiwa mzuri namna gani sisi kwetu ilikuwa afadhali ya jana,”anasema Dotto

Dotto anakumbuka mwaka 2018 ambapo alifanikiwa kupata zaidi  ya Sh6 milioni zilizotokana na mauzo ya zao la pamba, lakini hadi mwaka unaisha hakuna kitu cha maana alichoweza kukifanya kwenye pesa hizo.

Katika kuzunguka kwa waganga wa kienyeji alielezwa kuwa sababu kubwa ni wazazi wao hajawaweza kufanya tambiko kuondoa laana iliyopo ndani ya familia yao.

“Nilipotathmini hali yangu na hali ya baba ambaye alituelekeza niliona huenda majibu ya watalaamu yana ukweli ndani yake. Niliwashirikisha wazazi nao wakakubali kufanya tambiko na ndiyo maana tuko hapa kwa ajili ya shughuli hiyo,” anasema Dotto huku akiwa amefunika uso wake.

Licha ya kufanikiwa kuwa na familia na watoto sita, Dotto anasema changamoto za kimapato bado zinamwandama ambapo anaamini tambiko hilo litamfungulia ukurasa mpya wa maisha.

Matumaini ya mapacha hao baada ya tambiko hilo ni kupata mafanikio waliyoyakosa katika kipindi chote cha mahangaiko yao ya maisha. 

Endelea kufuatilia simulizi hii ambapo sehemu inayofuata tutaangazia gharama za kufanikisha matambiko ya “kuondoa laana kwa mapacha na jinsi ambavyo watu wanashindwa kutimiza masharti ya mila hiyo”. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW