Siri iliyofichika watoto mapacha kuhusishwa na “mikosi” Kanda ya Ziwa-1

November 20, 2020 8:19 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya watu katika kabila la wasukuma wanaamini watoto mapacha wanashikilia hatma ya familia.
  • Wasipofanyiwa tambiko kuondoa mikosi, familia haiwezi kufanikiwa.
  • Pia mapacha ambao hawajafanyiwa tambiko kuwaondolewa mikosi, hukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupungua kwa ufanisi wa tendo la ndoa. 

Mwanza. Kundi kubwa la watu limekusanyika katika moja ya kaya zilizopo katika Kijiji cha Mwamajila, umbali wa saa saba hivi kwa basi kutoka jijini Mwanza. 

Vigelegele na shangwe vinarindima. Wanaume na wanawake wanaimba hapa. Hii ni siku ya kwanza ya sherehe ya kuwakaribisha Masomi Shibiriti na mkewe, Tabu Shibiriti kwenye jamii ya ‘Wakango”. 

Wakango ni chama cha watu waliozaa watoto mapacha ambao baadhi ya watu wa kabila la Wasukuma wanaamini kitendo hicho ni “laana” na “mikosi” kwenye familia. 

Wanandoa hawa walizaa mapacha miaka 37 iliyopita lakini kutokana na imani yao ya Kikristo walishindwa kufanya mila na desturi zinazoaminika kuwa zinaoondoa mikosi yote kwa kuwa na watoto hao.  

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa mila hiyo hufanywa na baadhi ya Wasukuma tu huku wengine hawaamini kuwa kuzaa mapacha ni laana. 

Najumuika na wanakijiji hawa na kuwa moja ya wageni waalikwa wanaoipongeza familia hii ya Shibiriti baada ya kufanyiwa tambiko ili kuondoa “mikosi” iliyokuwa inawakabili. 

Katika maongezi yetu ya awali, Shibiriti mwenye umri wa miaka 70 anasema katika miaka yote hiyo hali ya kiuchumi ya familia yake haikua nzuri, mikosi iliwaandama na hata walipolima ardhi haikuzaa matunda.

“Ng’ombe na mbuzi zizini hazikua na msaada kwao maana mifugo mingi ilikufa pasi na ugonjwa kufahamika,” anasema Mzee Shibiri, mkazi wa kijiji cha Mwamajila kata ya Mwagi, wilayani Kwimba katika Mkoa wa Mwanza.Baba huyo wa watoto nane wakiwemo mapacha aliowazaa mwaka 1983, ni miongoni mwa watu wanaofanyiwa sherehe za tambiko kijijini hapa.

Sherehe hizi hufanyika kwa siku tatu mfululizo zikiambatana na ngoma, nyimbo mbalimbali na chakula cha kila aina.  

Kwa kuwa usukumani kilimo na ufugaji vimetawala, ng’ombe, mbuzi na kondoo wa kutosha huangushwa kwa ajili ya kalamu hiyo. 

Wazazi na wanachama wa jamii ya Wakango huvalia mavazi nadhifu ambayo ni shuka, shanga na kofia kwa wanaume kwa ajili ya sherehe hizi. 

Wale wanaokaribishwa baada ya matambiko huvaa mavazi tofauti kutokana na siku ya tambiko.

Watoto mapacha ambao wazazi wao wanafanyiwa tambiko wakiwa wamefunikwa shuka wakati tambiko hilo likiendelea katika familia ya mzee Shibiriti katika Kijiji cha Mwamajila, Wilaya ya Kwimba, jijini Mwanza. Picha|Mariam John.

Siku ya kwanza, Wakango wapya huvaa nguo za kawaida lakini jioni hutakiwa kuvaa nguo zinazoacha wazi sehemu ya juu ya mwili (kuanzia kiunoni hadi kichwani) na kwenda porini ili kuonyeshwa dawa za kuwalinda watapokamilisha shughuli ya tambiko na kurejea nyumbani.  

Katika siku ya pili nayo huwa na mambo yake, viti hupangwa katikati ya uwanja wa nyumba, karibu na liliposimikwa tawi la mti lililoegeshewa majembe mapya ambapo shughuli ya tambiko inafanyika, Mtemi wa jamii Wakango, Emmanuel Mkwaga aliiambia Nukta.  

Katika siku hiyo asubuhi na mapema, Shibiriti na mkewe wanatolewa nje ya nyumba ndani na kuanza kuzunguka eneo hilo huku mwanaume akiwa amebeba mkuki na mwanamke mwiko na watoto mapacha wakiwa wamefunikwa mashuka wasionekane utosi na hata unyayo.

Wakiongozwa na Nsumba Ntale, mapacha wakiwa gubigubi wanaongozwa kuzunguka eneo hilo huku Wakango na majirani  wakiendelea kuimba na kucheza ngoma na baadaye mapacha hurejeshwa tena ndani wakiwaacha wazazi wao wakiketishwa kwa tambiko la ugali. 

Nsumba Ntale ni kijana mkuu wa mila. 

Mganga aliyeteuliwa na Mtemi anashiriki kuwachanja chale sehemu mbalimbali za miili yao na kupakwa dawa kisha vyungu  vitatu hupitishwa mbele yao ambapo wazazi pamoja na washiriki  hula chakula hicho. 

Siku ya tatu ambayo haina mambo mengi, nilishuhudia wazazi wa mapacha ambao waliofanyiwa tambiko wakichukua fagio na kuamrishwa kufagia uwanja mzima, baadaye takataka hizo hukusanywa sehemu moja na kuongezewa kuni zingine, moto mkubwa huwashwa. 

Baada ya moto kukolea sana wazazi hutakiwa kuuruka lengo ni kukamilisha matambiko yote yaliyofanyika eneo hilo.

Zoezi hili lilifanyika saa 4:00 asubuhi,  ambapo mchana Wakango walivalia mavazi yao mekundu na kuingia ukumbini kwa kucheza na kuimba ili kumkaribisha rasmi Mzee Shibiriti na familia yake. 

Baada ya zoezi hilo, ratiba hutangazwa kama kuna sehemu nyingine wataenda kumkaribisha mkango mpya na kutawanyika kurudi katika nyumba zao. 


Soma zaidi: 


Kwa nini tambiko kwa watoto mapacha?

Ili kujibu swali hili nakutanishwa na wazee maarufu kijijini hapo akiwemo Mtemi wa jamii Wakango, Emmanuel Mkwaga. 

“Watoto mapacha huzaliwa na mikosi na mzazi asipochukua jukumu la kuwatibu yaani kufanya tambiko husababisha mali na mifugo kupotea na wakati mwingine magonjwa na vifo vya gafla hutokea kwa wanafamilia ,” anasema Mtemi Mkwaga.

Mtemi huyo anadai kuwa mapacha ambao hawajafanyiwa tambiko kuwaondolewa mikosi, hukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupungua kwa ufanisi wa tendo la ndoa.

“Kama ni pacha wa kiume akienda kuoa alikuwa hawezi kushiriki tendo la ndoa kwa kuwa maumbile yake yanakuwa legelege, hata pacha mwanamke anapoolewa, mwanaume akitaka kushiriki naye tendo la ndoa hataweza maana maumbile yake hulegea kabla ya tendo,” anasema Mtemi huyo. 

Mtemi Mkwaga anasema wanaamini jambo lingine linaloweza kuwapata watoto hao, ni nyota zao kuathiri mwenendo na ustawi wa shughuli za kiuchumi kwa familia hususani ufugaji na kilimo. 

Hali hiyo, anasema, hutokea pia kwa mtoto anayezaliwa akiwa ametanguliza makalio ambaye usukumani hujulikana kama Kashinje.

Wakango wakigawana karanga na pipi kwenye sherehe za tambiko zilizofanyika katika kijiji cha Mwamajila wilayani Kwimba, ugawanywaji wa karanga hizo ni moja ya shukrani ambazo familia inayofanyiwa tambiko huitoa ili iweze kubarikiwa. Picha|Mariam John.

Kwa mujibu wa Mtemi Mkwaga anasema Kashinje  huwa na nyota kali, jambo linaloilazimu jamii kuwachukulia kama watu wa kipekee wakiwaheshimu na kuwasujudu.

“Wanamsujudia kwa sababu ndiye amebeba hatma ya familia hiyo kimafanikio. Mfano kama siku hiyo akisema anataka kula nyama ya kuku, mbuzi ama kondoo basi muda huo huo mfugo huo utakufa,” anasema Mkwaga.

Mzee Kulwa Mabirika, niliyekutana naye katika sherehe hizo, anasema Kashinje hudekezwa mno na hufanyiwa kila jambo analotaka lengo ikiwa kumfurahisha kwa kila jambo na si kumuudhi kwa sababu ameshikilia hatma ya familia na jamii kwa ujumla. 

Mikosi mingine inayoweza kutokea kama tambiko halijafanyika, kwa mujibu wa jamii ya Wakango ni mke ama mume wa pacha kufariki au kushindwa kufanya maendeleo na badala yake kubakia masikini.

Mtemi huyo pamoja na mambo mengine ananifahamisha namna matambiko hayo hufanyika japo ananikanya hatoniambia vyote maana tambiko linakuwa na mambo mengi ya siri nzito.

Usikose sehemu ya pili ambayo tutaangazia kwa undani matambiko yanavyofanyika kulingana na aina za mapacha na iwapo kuna ukweli kuwa mapacha ni “mikosi”.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV