Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
- Simu hizo zitatumia mfumo wa ujumbe mfupi kupokea na kutuma taarifa za uchunguzi binafsi.
- Itasaidia kujua hali ya afya na kumkumbusha mgonjwa kwenda katika kituo cha afya kupata matibabu.
Dar es Salaam. Umechoka kwenda mara kwa mara katika kituo cha afya kufuata vipimo vya afya yako? Teknolojia ya matibabu imeboreshwa, kwa kutumia simu ya mkononi unaweza kupata vipimo vya kifua kikuu (TB) ukiwa popote nchini.
Hatua hiyo inakuja baada ya Serikali kuzindua huduma binafsi za uchunguzi wa TB ambapo kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi mgonjwa au mtu yeyote anayehitaji taarifa sahihi na vipimo atazipata kwenye kiganja chake bila kwenda katika kituo cha Afya.
Akizundua huduma hiyo leo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile amesema wizara yake inalenga kuwafikia watu wengi kwa kutumia teknolojia rahisi ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya magonjwa yanayoweza kuizuilika kwa kutumia taarifa sahihi.
“Tunaangalia idadi ya watu waliosajiliwa, ujumbe uliotumwa kwa walengwa, idadi ya wagonjwa wa TB waliogunduliwa na ufuatiliaji wa wagonjwa kwa wakati muafaka. Matumaini yangu taarifa zitakazokusanywa zitakuwa muhimu kwa mtu binafsi na programu,” amesema Dk Ndungulile.
Amesema kupitia ujumbe wa uchunguzi binafsi, mtumiaji anaweza kuingia kwenye mtandao na kujibu maswali kuhusu dalili za ugonjwa wa TB na kupata maelekezo muhimu ya kitabibu.
Iwapo mhusika atagundulika kuwa na dalili za ugonjwa huo, ujumbe utamwelekeza kwenda kwenye kituo cha afya kilicho karibu na ataendelea kukumbushwa mpaka atakapokubali kwamba ametembelea kituo cha afya.
“Mpaka sasa watoa huduma kutoka mikoa sita wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo,” amesema Dk Faustine.
.Zinahusiana:
- Apple yaingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Huduma hiyo imeanza kutolewa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na kampuni ya simu ya Airtel Tanzania ambao ndiyo wawezeshaji wa mfumo huo wa ujumbe mfupi ambapo changamoto iliyobaki ni kuwatambua wagonjwa wapya wa TB na kuhakikisha wanafika katika vituo vya afya kupata matibabu.
Meneja Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando amesema wanazidi kujitanua katika utoaji wa huduma za kijamii hasa katika sekta ya afya ambapo walianza na kampeni ya “Wazazi Nipendeni” ambayo ilitumia meseji 31 milioni na kufanikiwa kuwafikia zaidi ya akina mama 5 milioni ambao wamepata matibabu ya uzazi.
“Sisi kama watoa huduma tunazidi kujiimarisha ili kuhakikisha tunasaidia jamii katika masuala ya afya,” amesema Mmbando.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO) TB inashika nafasi ya 9 kwa kusababisha vifo duniani kote na ni ugonjwa wa kuambikiza unaoongoza ukifuatiwa na Virusi Vya UKIMWI.