‘Silicon Zanzibar’ yapata msukumo mpya uwekezaji kituo cha ubunifu
Mji wa Fumba ukionekana kwa juu,eneo ambalo zinajengwa ofisi za teknolojia ikiwemo ya Wasoko. Picha | Wasoko.
- Ni Mpango wa kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha teknolojia barani Afrika.
- Wadau wazindua kituo cha ubunifu cha Wasoko kitakachowekeza Sh34 bilioni ndani ya miaka 10.
- Kitaibua suluhu mbalimbali za kibiashara na ajira visiwani humo.
Dar es salaam. Huenda hali ya maisha ya wananchi wa Zanzibar hasa vijana ikaimarika zaidi siku zijazo, baada ya wabunifu kuja na mpango wa kukuza ubunifu na kutafuta suluhu za kiteknolojia kutatua changamoto za kijamii visiwani humo.
Kampuni ya biashara mtandao ya Wasoko imezindua rasmi kituo cha kwanza cha uvumbuzi na ubunifu wa teknolojia visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kituo hicho kinachoitwa Wasoko kipo Kusini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja katika mji wa Fumba, na kitajielekeza kuibua suluhu za kiteknolojia katika uendeshaji wa biashara mtandao barani Afrika.
Kituo hicho kitawakutanisha pamoja, wahandisi wa teknolojia ,watafiti na wabunifu zaidi ya 500 kutoka pembe tofauti za dunia ili kupendekeza suluhu kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi wa kisiwa hicho.
Pamoja na kuimarisha utendaji kazi wa Wasoko kituo hicho kitajikita katika kuboresha huduma za wateja ikiwemo ufikishaji wa bidhaa, kuongeza machaguo ya huduma za kifedha pamoja na kukusanya data muhimu za kibiashara.
Wasoko inatarajia kuwekeza Dola za Marekani milioni 15 sawa na Sh34 bilioni katika kipindi cha miaka 10 na kuzalisha fursa za ajira kwa wakazi wa visiwani humo.
Umesoma hii?:
Wasoko inakuwa kampuni ya kwanza kutekeleza mpango wa serikali ya Zanzibar wa kuvutia kampuni za teknolojia kuwekeza visiwani humo wa ‘Silicon Zanzibar’ kwa ajili ya kufanya mageuzi ya teknolojia.
Daniel Yu Mkurugenzi na mwanzilishi wa Wasoko aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho cha uvumbuzi Agosti 30, 2022 amesema wamepata sehemu sahihi itakayowakutanisha wabunifu bora kutoka sehemu mbalimbali duniani watakao vumbua na kuendeleza huduma za kiteknolojia.
Yu amesema ni muhimu kuwa na vituo vya teknolojia Afrika kwa ajili ya mageuzi ya bara hilo.
“Kupitia ushirikiano wetu tunajiskia fahari kufanya kazi pamoja na Serikali ambayo imewekeza nguvu katika mradi huu, tunafurahi pia kuwa watu wa kwanza kutekeleza mpango wa ‘Silicon Zanzibar’,” amesema Yu.
Fursa zaidi
Kituo Cha ubunifu Cha Wasoko kitakuwa sehemu ya mpango wa sasa wa uendelezaji wa Mji wa Fumba ambapo nyumba za kisasa na ofisi za kibiashara zinajengwa kando ya ufukwe wa bahari ya Hindi uliopo umbali wa takribani dakika 15 kutoka ulipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Eneo hilo ambalo litakuwa kitovu cha mradi wa Silicon Zanzibar, kitarahisisha utoaji wa viza za kazi kwa wafanyakazi wenye ujuzi wa teknolojia barani Afrika na kwingineko ili kuchochea uwekezaji katika sekta ya teknolojia na utalii.
Waziri wa Uwekezaji na Maendeleo ya Uchumi Zanzibar, Mudric Soranga amesema wanaandaa mazingira mazuri kwa kampuni zote za teknolojia ulimwenguni kuwekeza visiwani Zanzibar pamoja na kushiriki katika kutengeneza sera na maboresho yatatakayoifanya Zanzibar kuongoza katika medani ya teknolojia barani Afrika.
Latest
