Si kweli: Mtu ajirusha ghorofa ya nne hoteli ya bondeni Magomeni Tanzania
- Ni Mombasa nchini Kenya.
- Uchunguzi wa Nukta Fakti umebaini chanzo si fumanizi kama ilivyoelezwa awali.
Dar es Salaam. Kwa siku mbili mfululizo kumekuwa na video fupi inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kama Whatsapp na X ikionesha mwanaume akijirusha kutoka ghorofani katika hoteli inayodaiwa kuwa ipo Magomeni Tanzania, jambo hilo si kweli.
Mathalani video hiyo, inayosambaa ikiwa na maneno “Jamaa kafumaniwa Bondeni Hotel, kaona mambo yasiwe mengi kaamua kujirusha ghorofani” imeshatazamwa na zaidi ya watu 103, 700 kutoka sehemu mbalimbali ambao huenda wameamini tukio hilo limetokea Dar es Salaam.
Ukweli ni huu
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini, ni kweli mtu huyo alijirusha kutoka ghorofa ya nne katika hoteli ya Suhufi Palace Hotel in Bondeni iliyopo Mombasa nchini Kenya na sio Magomeni Tanzania.
Kwa msaada Geolocation tumebaini eneo hilo lipo Mombasa katika Barabara ya Abdel Nasser na chini ya jengo hilo kuna benki.
Aidha, usajili wa namba za magari yaliyo chini ya ghorofa hilo yana onyesha ni ya Kenya na sio Tanzania kwa kuwa zinaanzia na herufi K inayotumika nchini humo, wakati zile za Tanzania huanza na herufi T.
Hata hivyo, vyombo mbali mbali vya habari nchini Kenya vimeripoti tukio hilo lililotokea Mombasa, vikimtaja mtu aliyejirusha ghorofani kuwa ni Abdulrazak Kassim mwenye miaka 23 siku ya jumatatu asubuhi ambapo chanzo cha kujirusha kwake kinaendelea kutafutwa na si fumanizi kama ilivyoelezwa awali.