Rais Samia aonya siasa kilimo cha pamba Simiyu

June 17, 2025 7:18 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka wakulima wa zao hilo kusikiliza maelekezo ya Serikali peke yake.
  • Bashe asema pamba Simiyu inatumika kisiasa na sio kama zao la kuleta maendeleo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Simiyu kujiepusha na siasa zilizopo katika kilimo cha pamba mkoani humo na badala yake kusikiliza maelekezo na mwongozo wa Serikali katika uzalishaji wa zao hilo

Rais Samia aliyekuwa kihutubia wananchi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu amewaambia wakazi wa mkoa huo kuwa Serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa ajili ya kuchochea uzalishaji wa zao hilo linalotumika katika uzalishaji wa nguo na vifaa vya matibabu.

 “Ndugu zangu katika kilimo na uzalishaji wa pamba kuna siasa kubwa, niwaombe sana tusikilizeni serilikali tunavyowaambia,” amesisitiuza Rais Samia.

Kauli ya Rais Samia inakuja muda mchache tu mara baada ya Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina kutaka mabadiliko katika mfumo wa ununuzi wa pamba kutoka wa mnunuzi mmoja uliopo hivi sasa na kuwa wa ushindani ukiwahusianisha mnunuzi zaidi ya mmoja.

Bashe amesema wanasiasa wa mkoa huo wamekuwa wakitumia zao la pamba kisiasa jambo lililoathiri soko la zao hilo katika misimu iliyopita. Picha | Ikulu.

Mpina aliongeza kuwa uwepo wa mnunuzi zaidi ya mmoja utasaidia kuwa na bei shindani ya zao hilo na hivyo wakulima kuuza kwa bei ya faida.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alipangua hoja ya Mpina na kubainisha kuwa ni Serikali ndiyo inayoamua bei ya pamba bila kujali idadi ya wanunuzi waliopo.

Bashe amesema wanasiasa wa mkoa huo wamekuwa wakitumia zao la pamba kisiasa jambo lililoathiri soko la zao hilo katika misimu iliyopita ambapo sasa Serikali inafanya juhudi ya kunyanyua zao hilo kwa kufanya afua mbalimbali ikiwemo kutoa pembejeo na huduma za kulimiwa mashamba kwa ruzuku.

“Endeleeni kukusanya pamba, bei inaamua Serikali na tunapanga sisi bei,” amesisitiza Bashe.

Kwa mujibu wa Ripoti ya hali ya Uchumi wa Nchi 2024, wastani wa bei ya pamba nchini kwa mwaka 2024 ilikuwa Sh1,350 kwa kilo ,ikiongezeka kwa asilimia 17.4  kutoka Sh1,150 mwaka 2023.

Aidha, uzalishaji wa pamba mwaka 2024 uliongezeka kwa asilimia 61.9 kutoka tani 282,510, ukilinganishwa na tani 174,486 mwaka 2023.

Thamani ya mauzo nje ya nchi ya zao hilo mwaka 2024 ilikuwa Dola za Marekani milioni 69.3 sawa na Sh180.91 bilioni, ikilinganishwa na milioni 101.9 sawa na Sh266.01 bilioni mwaka 2023 sawa na upungufu wa asilimia 32.

Serikali imesema upungufu huo wa umetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya pamba katika soko la ndani sambamba na kupungua kwa bei ya pamba katika soko la dunia kwa asilimia 9.9.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks