Si kweli: Vidonge vya Paracetamol P 500 vina virusi vya Machupo

July 30, 2024 4:50 am · Bacley Madyane
Share
Tweet
Copy Link
  • TMDA yakanusha uwezekano wa virusi kukaa kwenye dawa.
  • Yawataka wananchi kujenga utaratibu wa kupata taarifa kwenye vyanzo sahihi kabla ya kusambaza.

Dar es salaam. Huenda umekutana na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayowataka watu kuchukua tahadhari na kutotumia vidonge vya Paracetamol P 500 kwa kuwa vina virusi vya Machupo, taarifa hiyo si ya kweli.

Ujumbe huo ulioanza kusambaa katika mitandao ya WhatsApp, pamoja na Facebook kuanzia Julai 26,2024 umeambatanishwa na picha inayoonesha mtu aliyetapakaa na vidonda mwilini ikiwa na maneno yanayosomeka;

“ONYO LA HARAKA! Kuwa mwangalifu usichukue paracetamol ambayo inakuja imeandikwa P 500. Ni paracetamol mpya nyeupe sana na inayong’aa, madaktari wanashauri kuwa ina virusi vya “Machupo”.

Ukweli huu hapa

Nukta Fakti imefanya uchunguzi ili kujiridhisha na kuthibitisha madai hayo na kugundua yafuatayo;

Ukweli ni kwamba ujumbe huo umekuwa ukisambaa katika makundi sogozi ya WhatsApp, na sio mpya kama wengi wanavyodhani kwa kuwa umeshatokea katika nchi mbalimbali barani Afrika, ikiwemo hapa Tanzania, pamoja na Afrika Kusini.

Aidha, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) ilitoa taarifa kwa umma tarehe 21 Agosti 2019 ikikanusha taarifa hiyo ya upotoshaji. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa hakuna virusi vyovyote vinavyoitwa Machupo, na hakuna uwezekano wa virusi kuishi kwenye vidonge vya paracetamol.

Pia, bidhaa ya P-500® (Paracetamol) iliyotengenezwa na Apex Laboratories Private Limited, India, haijasajiliwa nchini Tanzania, na TMDA haijawahi kutoa kibali cha uingizaji wa bidhaa hiyo.

Hata hivyo, Julai 27, 2024 TMDA ilitoa tena ufafanuzi mwingine kutilia mkazo taarifa iliyotoa mwaka 2019 ambapo imesisitiza dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa.

“TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda afya ya jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi,” imebainisha taarifa ya TMDA.

Hata hivyo, TMDA imewakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye jamii.

Enable Notifications OK No thanks