Si kweli: Vaseline na kitunguu maji vinaongeza makalio

August 13, 2024 7:28 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha hilo.
  • Madaktari wabainisha njia zinazoweza kutumika.

Katika baadhi ya tamaduni wanawake wenye makalio makubwa hutafsiriwa kama warembo zaidi, hali hiyo imesababisha kuwepo na msukumo wa baadhi ya wanawake kutaka kuongeza maumbile yao ili kuongeza mvuto.

Msukumo huo umesababisha kuenea kwa taarifa potofu zinazoelezea mbinu za kuongeza makalio ambazo baada ya uchambuzi wa kina zimebainika kuwa si kweli.

Mathalani, hivi karibuni kumekuwa na video mbalimbali katika mitandao ya kijamii kama vile tiktok na WhatsApp inayoeleza kuwa mchanganyiko wa mafuta ya vaseline na kitunguu maji huongeza makalio kwa wanawake, jambo hilo si kweli.

Ukweli ni huu

Vaseline ni aina ya mafuta ya jeli yenye mchanganyiko wa petroli, ambayo hutumika sana kwa madhumuni mbalimbali ya kiafya ikiwemo urembo.

Vaseline ni jina la biashara linalotumika kwa bidhaa hii iliyopo chini ya Kampuni ya Unilever ya Marekani lakini jina la kisayansi ni ‘petroleum jelly’.

Kwa mujibu wa tovuti ya vaseline ambao ndio wazalishaji wa mafuta hayo, vaseline hutumika katika kuimarisha ngozi, kulainisha ngozi kavu, midomo, na kusaidia kuponya ngozi iliyojeruhiwa. 

Kitunguu maji ni aina ya mboga inayojulikana kwa jina la kisayansi Allium cepa na huwa na rangi nyeupe, nyekundu au manjano na mara nyingi hutumika kama kiungo katika mapishi mbalimbali.

Isaac Mittoh, ambaye ni daktari wa tiba asili na mtaalamu wa mimea dawa ameiambia Nukta Fakti kuwa mpaka sasa hakuna ushahidi wowote wa kisayansi unaoonesha kuwa matumizi ya vitu hivyo yanasaidia kuongeza makalio.

“Hakuna scientific evidence( ushahidi wa kisayansi) hata ya kuungaunga inayo weza claim (dai) vaseline au kitunguu maji kuwa na properties(vitu) za kuongeza makalio au hips”, amesema Dk.Mittoh.

Dk. Mittoh amesititiza kuwa mafuta ya vaseline hayajathibitishwa kufanya kazi nyingine yoyote zaidi ya kung’arisha afya ya ngozi huku kwa upande wa kitunguu kikisalia kama chakula.

Kwa upande wake daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Marie Stopes Tanzania iliyopo jijini Dar es Salaam Dk. Berno Mwambe ameiambia Nukta Fakti kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisayansi unaothibitisha kuwa vaseline na kitunguu maji vinaongeza maumbile kwa mwanamke.

Aidha, Dk.Mwambe amebainisha kuwa hakuna njia za kitabibu zinazopendekezwa kwa ajili ya kuongeza maumbile zaidi ya upasuaji.

“Njia za kitabibu ambazo zinatumikaga ni hizi za kufanya surgery(upasuaji)  ingawa pia kila kitu kinafaida zake na hasara zake nadhani pia hata hizo surgery (upasuaji) pia wapo waliopata madhara kwa ajili ya hizo surgery (upasuaji) “, amesema Dk. Mwambe. 

Dk.Mwambe ameongezaa kuwa, maumbile hususan makalio ni suala la vinasaba ambavyo mtu huzaliwa navyo, ingawa kwa wanaotaka kuongeza wanaweza kufanikiwa kwa kufanya aina fulani ya mazoezi kwa muda mrefu au upasuaji.

Nukta Fakti inaiasa jamii kuwa makini na taarifa zinazopatikana kwenye mitandao ya kijamii na kuhakikisha unapata kwanza maelezo ya wataalamu wa jambo husika kabla ya kufanya maamuzi.

Enable Notifications OK No thanks