Si kweli: Tanzania haijazuia Kiswahili kufundishia shule za sekondari
- Ni baada ya baadhi ya watu kuzusha kuwa Kiswahili kisitumike sekondari.
- Serikali yasema haijatoa tangazo hilo.
Dar es Salaam. Serikali imewataka wananchi kupuuzia taarifa zinazosambaa mtandaoni kuhusu kupiga marufuku lugha ya Kiswahili kufundishia shule za sekondari nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.
Taarifa hiyo inayosambazwa na vyombo vya habari mbalimbali mtandaoni ikiwemo DW Africa na Nairobi News inasema Serikali ya Tanzania imepiga marufuku lugha hiyo kufundishia katika ngazi hiyo ya elimu ili kuwapa uwezo wanafunzi kujieleza vizuri kwa lugha ya Kiingereza jambo ambalo si kweli.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa, Serikali haijapiga marufuku matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari na kwamba taarifa rasmi kuhusu uzushi huo zitatolewa hivi karibuni.
Msigwa katika ukurasa wake wa Twitter ameongeza kuwa hivi sasa Tanzania inaendeleza juhudi zake katika kukuza na kuimarisha Kiswahili ndani na nje ya nchi hivyo marufuku hiyo ni sawa na kurudisha nyuma juhudi hizo.
“Tanzania inatambua wajibu wake wa kukuza matumizi ya Kiswahili duniani kote. Kwa hiyo, isingewezekana kwa Tanzania kupiga marufuku matumizi ya Kiswahili katika shule zetu zozote,” amesema Msigwa.
Nayo Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayoshughulikia na usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi na sekondari nchini imeuwekea ujumbe huo maneno mekundu ’false information’ kwenye ukurasa wao wa Twitter ikimaanisha kuwa habari hiyo haina au ukweli.
Zinazohusiana
-
Hapana: Marekani haibadilishi noti za fedha zake
-
Mate, jasho la mgonjwa aliyepona havisambazi virusi vya Ebola
Tulichobaini
Taarifa hiyo inayosambaa mtandaoni imenukuu taarifa ya Benjamin Oganda anayetajwa kuwa Afisa Elimu Msaidizi katika ofisi ya Rais ambaye kiuhalisia hana mamlaka ya kubadili lugha ya kufundishia kwa ngazi yoyote ya elimu.
Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote rasmi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikithibitisha utekelezwaji wa lugha hiyo ya kujifunzia kwa shule za sekondari.
Kwa mujibu wa Sera ya elimu ya mwaka 2014 Lugha za Kiswahili, Kiingereza, lugha nyingine za kigeni na lugha ya alama zinatumika kufundishia masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.

Latest
