SI KWELI: Mbowe hajateuliwa kugombea Urais kupitia Chaumma

May 21, 2025 6:12 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ameteuliwa kuwa mgombea urais wa mwaka 2025 kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), siyo ya kweli. Habari hiyo imekuwa ikisambazwa katika majukwaa mbalimbali ya mitandaoni kama Facebook, ikidaiwa kuwa uteuzi huo ulifanywa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chaumma tarehe 10 Mei 2025.

Taarifa hiyo inadaiwa kuambatana na barua iliyoandikwa kama “Taarifa kwa Umma” iliyosainiwa na mtu anayejiita Katibu wa Habari wa Chaumma. Pia, baadhi ya majukwaa ya mitandao ya mtandaoni na majina ya vyombo kama Jambo TV na Millda Ayo yamehusishwa katika kusambaza habari hiyo

Ukweli ni huu

Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa taarifa inayodai Freeman Mbowe ameteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Chaumma ni ya kupotosha na haina uhalisia.

Kwanza, muundo na muonekano wa barua iliyosambazwa si wa kawaida. Aina ya mwandiko (fonti) iliyotumika katika barua hiyo haitumiki katika machapisho rasmi ya Chaumma. Zaidi ya hayo, barua hiyo haijachapishwa kwenye tovuti rasmi ya chama hicho wala kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Pili, hakuna ushahidi wowote wa kufanyika kwa kikao cha Kamati Kuu au Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chaumma mnamo tarehe 10 Mei 2025, kama inavyodaiwa katika taarifa hiyo feki. Hakuna kumbukumbu rasmi au taarifa yoyote kutoka kwa chama hicho inayothibitisha tukio hilo.

Pia Chaumma haijatoa taarifa yoyote rasmi inayomhusisha Freeman Mbowe na uteuzi wa kugombea urais, na hadi sasa, hakuna kiongozi wa chama hicho aliyethibitisha madai hayo kupitia vyombo vya habari au mitandao yao rasmi.

Freeman Mbowe bado ni mwanachama halali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na hajatangaza kujiunga na chama kingine au kujitoa rasmi Chadema.

Hata kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za viongozi waandamizi wa Chaumma, pamoja na ukurasa wa idara ya habari ya chama hicho, hawaja chapisha taarifa yoyote kuhusu uteuzi huo. Hili linathibitisha wazi kuwa habari hiyo ni kupotosha umma.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks