Si kweli: Maria Sarungi amshinikiza Heche kusaini kanuni za maadili za Uchaguzi
- Machapisho yanayosambaa hayajachapishwa na vyombo vya habari vya Mwananchi, Jambo Tv na The Chanzo na hayapo kwenye akaunti rasmi ya vyombo hivyo vya habari.
- Boni Yai hajachapisha madai hayo kwenye akaunti yake rasmi ya Mtandao wa X.
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu waliokutana na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan mtandao wa Facebook zikidai kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai amemtuhumu mwanaharakati Maria Sarungi kumshinikiza Makamu Mwenyekiti wa chama hicho John Heche kusaini kanuni za maadili za Uchaguzi. Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa habari hiyo si ya kweli.
Taarifa hii ya upotoshaji inayosambazwa kama chapisho kutoka akaunti rasmi ya mtandao wa X (zamani Twitter) ya Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai linalosomeka “Maria Sarungi ndiye aliyewasiliana na Makamu Heche na kusisitiza tusisaini kanuni za maadili za Uchaguzi. Hakukuwa na utaratibu wa kiofisi uliofuatwa, leo tunasema ukweli haki za wanachama wa CHADEMA zimeporwa na wachache wasiothamini misingi ya demokrasia”.

Katika hatua nyingine machapisho ya kughushi yenye mfanano na chapa za vyombo mbalimbali vya habari vinavyoaminika nchini ikiwemo Mwananchi, Jambo TV na The Chanzo yalionekana yakisambaa mtandaoni yakiripoti taarifa hiyo potoshi kwa vichwa mbalimbali vya habari.
Ukweli ni huu
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebainisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli, kwani machapisho yote yenye mfanano wa vyombo vya habari vya Mwananchi, Jambo Tv na The Chanzo hayakuchapishwa kwenye akaunti rasmi za vyombo hivyo.
Aidha aina ya miandiko (fonts) zilizotumika sio zinazotumiaka katika machapisho rasmi ya vyombo tajwa vya habari.
Pia, chapisho linalosambaa kama chapisho kutoka akaunti rasmi ya Mtandao wa X wa Boni yai, si chapisho halali kwani halijachapishwa kwenye akaunti ya mtandao wa X ya Boni Yai, na aina ya mwandiko unaoonekana kwenye chapisho hilo si mwandiko rasmi unaotumika katika machapisho ya mtandao wa huo.
Latest



