SI KWELI: Freeman Mbowe afukuzwa Chadema
Dar es Salaam. Taarifa za kupotosha zinazosamba kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kama Facebook, Instagram, na YouTube, ikidai kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefukuzwa uanachama na uongozi wa chama hicho.
Baadhi ya machapisho hayo yameonekana yakiwa na vichwa vya habari kama:
“Mbowe Afukuzwa Chadema”, bila kuambatanishwa na ushahidi wowote au chanzo halali kutoka ndani ya chama.
Mfano, katika moja ya machapisho yanayosambaa kupitia mtandao wa Facebook, kuna barua iliyowekwa ambayo inadaiwa kutolewa na Chadema. Sehemu ya maneno ya awali katika barua hiyo inadai

“Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza rasmi kumfutia uanachama Bwana Freeman Mbowe.”
Ukweli ni huu
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa hakuna taarifa yoyote rasmi kutoka CHADEMA inayothibitisha kufukuzwa kwa Freeman Mbowe kutoka chama hicho.
Aidha, Nukta Fakti imepitia mitandao rasmi ya chama hicho, ikiwemo tovuti na kurasa zake za kijamii, na hakuna chapisho lolote la barua au taarifa kwa umma inayohusiana na madai hayo. Barua iliyosambazwa kwenye mtandao wa Facebook pia imebainika kuwa ni ya kughushi, kwa sababu.
Haipo kwenye kurasa rasmi za Chadema. Haitumii muundo na mwandiko wa barua rasmi za chama hicho. Imesambazwa na akaunti zisizo na uhusiano wowote rasmi na chama.
Zaidi ya hayo, baadhi ya machapisho ya video na picha yanayodaiwa kutoka kwa vyombo vya habari kama ITV hayapo kwenye kurasa rasmi za taasisi hizo, jambo linalothibitisha kuwa taarifa hizo ni za uongo na zenye lengo la kupotosha umma.
Latest



