Si kweli: Chadema yatangaza kushiriki Uchaguzi Mkuu
- Machapisho yanayosambaa ni feki, yametengenezwa kwa lengo la kupotosha.
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu waliokutana na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan mtandao wa Facebook zikidai kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025. Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebainisha kuwa habari hiyo si ya kweli.
Taarifa hii ya upotoshaji imesambaa ikionekanama kama chapisho la Taarifa kwa Umma kutoka Chadema likiwa na nembo na sahihi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama hicho, Brebda Rupia likiwa nma kichwa kinachosemeka ‘ Tamko rasmi la Chama cha Demoktasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025’.
Taarifa hiyo potoshi imesambaa ikieleza kuwa chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kutafakari na kufanya majadiliano ndani ya chama.
“Baada ya tathmini ya kina, majadiliano ya ndani ya chama, na kusikiliza maoni ya wanachama wetu kutoka kila kona ya nchi, uongozi wa juu wa chama umetangaza kwa kauli moja kwamba CHADEMA ipo tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Kwa mantiki hiyo, tunapenda kuwajulisha kuwa tumeanza rasmi mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wetu wa nafasi za Udiwani na Ubunge katika majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Tunawahimiza wanachama wote wenye nia ya kugombea kujitokeza kwa wakati, kufuata taratibu za chama, na kushiriki kwa amani na ustaarabu katika mchakato huu wa kidemokrasia” inasomeka taarifa hiyo potoshi.

Taarifa hiyo pia imeendelea kwa kueleza kuwa Chadema itaendelea kusimamia misingi ya haki, uwazi, na uadilifu katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wetu, ikiwa ni sehemu ya dhamira yetu ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini Tanzania.
“Tunatoa wito kwa Watanzania wote wenye kiu ya mabadiliko kuendelea kuunga mkono juhudi za chama chetu katika kuhakikisha tunajenga taifa lenye haki, usawa, na maendeleo kwa wote” imemaliza taarifa hiyo.
Machapisho feki ya vyombo vya habari
Katika hatua nyingine ili kufanikisha adhma ya kufanya taarifa hiyo potoshi ionekane kuwa ya kweli, limesambazwa chapisho feki lenye mfanano na chapa ya Chombo cha Habari cha ‘The Chanzo’ likiwa na Kicha cha Habari kinachosema ‘ Chadema yatangaza rasmi ushiriki wake Uchaguzi Mkuu wa 2025’.

Pia chapisho lenye mfanano na Chombo cha Habari cha ‘Jambo TV’ likiwa na kichwa kinachosomeka ‘hatimaye chadema yathibtisha kushiriki Uchaguzi Mkuu. Na katika machapisho hayo yote mawili, imetumika chapisho la taarifa feki iliyosambaa kama chanzo cha taarifa.
Ukweli ni huu
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebainisha kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote zimesambazwa ili kupotosha.
Nukta Fakti imebaini kuwa aina ya mwandiko (fonts) uliotumika kwenye taarifa inayosambaa si mwandiko unaotumiwa katika taarifa kwa umma rasmi zinazotolewa na Chadema.
Katika hatua nyingine uchunguzi umebainisha kuwa machapisho ya vyombo vya habari ni feki, hayajachapishwa na vyombo hivyo vya habari na hayapo kwenye akaunti rasmi za vyombo hivyo.
Latest