Sheria mpya ununuzi wa umma inatakavyosaidia kukabiliana na ubadhilifu serikalini

September 8, 2023 6:25 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Inatarajiwa kukabili ubadhilifu kwa kuweka masharti bora ya usimamizi wa ununuzi wa umma
  • Sheria ya Ununuzi wa Umma namba 7 ya mwaka 2011 yafutwa

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma na Ugavi ambayo inalenga kusaidia kukabiliana na ubadhilifu kwa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.

Muswada huu unalenga kufuta Sheria ya Ununuzi wa Umma namba 7 ya mwaka 2011, ambayo ilikuwa inakosolewa kwa kuwa na mapungufu mengi na kutoa nafasi kwa ubadhirifu, ufisadi na upotevu wa rasilimali za umma ambayo pia yalibainishwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022. 

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, ukiukwaji wa taratibu za ununuzi, ubadhirifu na rushwa katika baadhi ya miradi ya taasisi za Serikali na kupendekeza kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma na Ugavi ibadilishwe ili kuondoa mianya ya ufisadi.

Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha kwa mara ya pili hoja ya Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma 2023 na marekebisho yake, amesema Sheria hiyo ina lengo la kuweka masharti bora ya usimamizi wa ununuzi wa umma, ugavi na uondoshaji wa mali kwa njia ya zabuni.

“Kwa ujumla sheria inayopendekezwa inakusudia kutatua changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa masharti na utaratibu wa ununuzi, ugavi pamoja na uondoshaji wa mali kwa njia ya zabuni,” amesema Dk Mwigulu.

Kwa mujibu wa Dk. Mwigulu changamoto hizo ni pamoja na sheria kutokutofautisha masharti ya ununuzi kati ya taasisi za umma zinazojiendesha kibiashara na nyingine, kutokujumuisha masuala ya ugavi, kutokuwa na sehemu mahususi inayohusu masuala ya usimamizi wa mikataba ya ununuzi, na kutoa mwanya wa kutotumia mifumo ya kielektroniki.

Pia kutobainisha masharti ya bei kikomo, kutokuwa na masharti kuhusu ukomo wa thamani ya mradi, kukosekana kwa taarifa za ukaguzi wa kazi zinazofanyika kipindi cha uangalizi wa ubora wa kazi, sharti la kudhibiti viwango vya weledi na uzoefu wa kiutekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa utaratibu wa ‘force account’.

Mapungufu mengine ni kutokuwa na viwango vya ukomo vya uidhinishaji wa zabuni na kuweka muda wa urefu wa hatua za utekelezaji wa ununuzi.

Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba akiwakilisha Muswada wa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma 2023 bungeni jijini Dodoma| picha na Wizara ya Fedha

Sambamba na hayo sheria mpya inategemewa kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa ununuzi wa umma na ugavi kwa sababu ya kuongezwa nguvu kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma na Ugavi (PPRA), ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kudhibiti shughuli zote za ununuzi wa umma na ugavi nchini. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo aliyekuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo amesema kamati imependekeza kuboresha kifungu cha ibara ya 11 juu ya majukumu ya PPRA kufanya ukaguzi.

“Ibara hii haikua imetoa fursa kwa afisa masuhuli kufanya uchunguzi au ukaguzi maalum kuhusu swala lolote katika ununuzi…marekebisho yanaenda kuipa PPRA mamlaka ya kufanya uchunguzi, kuhakikisha kuwa masuala ya ununuzi yanafuata sheria zilizoainishwa na taratibu zake zitakazotungwa,” amesema Sillo.

PPRA itakuwa na mamlaka ya kufanya uchunguzi, ukaguzi, tathmini ya ufuatiliaji wa ununuzi wa umma na ugavi, na kutoa taarifa, ushauri na mapendekezo kwa mamlaka husika hususan kwa waziri mwenye dhamana.


Zinazohusiana


Sheria mpya pia inatoa mwongozo wa taratibu za ununuzi wa umma na ugavi ikiwemo kutangaza zabuni, kupokea maombi, kufanya tathmini, kutoa mikataba, kusimamia utekelezaji na kutatua migogoro kwa njia ya ushindani wa wazi isipokuwa pale ambapo hali maalum zinahalalisha kutumia njia nyingine.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei, aliyekuwa akichangia hoja hiyo amesema anaamini baada ya sheria hii kupita itakwenda kuleta uhakika wa kupatikana kwa thamani halisi ya fedha ambazo ni asilimia 70 ya bajeti inayoidhinishwa kwa matumizi ya Serikali ili kutekeleza miradi na shughuli za ununuzi kwa tija kuwanufaisha zaidi wananchi.

Pia Dk Kimei mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika sekta ya benki na fedha ameishauri Serikali kuunda sera husika ili kujua ni kitu gani Bunge litahitajika kuhalalisha kuwa sheria kabla ya kutengenezwa kwa muswada.

Mbunge wa Handeni Mjini Kwagilwa Nhamanilo amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inapaswa kuimarishwa kwa kuwa ina sehemu kubwa kufanikisha masuala ya mikataba ya manunuzi.

“Ndio maana nasisitiza kuiboresha na kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama tunataka sheria hii tunayoitunga ikafanye kazi kwa usahihi na hizi asilimia 70 za mapato yetu yote tunayopeleka kwenye manunuzi zikasimamiwe vizuri lazima ofisi hii tuiwezeshe kibajeti iwe na wataalam wa kutosha,” amesema Nhamanilo

Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa amesisitiza Serikali kutambua ujuzi na uwezo wa mafundi hususan walioko maeneo ya vijijini na kuwapa mafunzo na ujuzi zaidi ili waweze kutekeleza miradi ya kutumia rasilimali za ndani ikiwa ni hatua ya kupeleka ajira kwa wananchi.

Sheria hii ni sehenu ya juhudi za Serikali za kupambana na rushwa, kuimarisha utawala bora na kuongeza uwajibikaji katika utumishi wa umma hivyo inatarajiwa kuongeza ufanisi, uendelevu na uwiano katika matumizi ya fedha za umma na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Enable Notifications OK No thanks