Serikali yazindua vipindi maalum kuhamasisha malezi, maadili mema

December 19, 2023 1:03 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vipindi hivyo vitafahamika kama ‘mamakuzi’ na ‘kijadili’
  • Vitasaidia kupambana na changamoto za mmomonyoko wa maadili na makuzi kwa watoto na vijana.
  • kusambazwa nchi nzima kwa miezi miwili mfululizo.

Dar es Salaam.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vipindi maalum vitakavyohamasisha malezi mema, makuzi ya watoto na maadili jambo ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kushamiri nchini Tanzania.

Waziri Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya ustawi wa jamii na miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa jamii jijini Dar es Salaam leo Disemba 18 , 2023 ametoa wito kwa wizara husika kusimamia vipindi hivyo ili viwafikie watanzania wengi.

“Nitoe wito vipindi vilivyokamilika visimamiwe kikamilifu ili kurushwa katika vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini na viweze kuwafikia watanzania,” amesema Majaliwa.


Soma zaidi:Namna ya kupunguza gharama za manunuzi ya vyakula, vinywaji msimu wa sikukuu


Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye,kutakuwa na vipindi 22 vitakavyosambazwa kwa miezi miwili mfululizo katika vyombo vya habari zaidi ya 150 nchi nzima ikiwemo redio.

“Takwimu zinaonyesha asilimia 70 ya Watanzania wanasikiliza redio…ukweli ni kwamba kuna idadi kubwa ya watanzania wanaosikiliza redio peke yake kwa muda mrefu ndio maana tukasema vipindi hivyo vilenge hiyo asilimia 70 ya Watanzania,”  amesema Nape.

Huenda vipindi hivyo vikawa muarobaini wa mmonyoko wa maadili unaoendelea Tanzania na duniani kwa ujumla jambo lililomuibua Rais Samia mara kadhaa kukemea, na kutoa rai kwa wazazi, walezi viongozi wa dini kudhibiti mmonyoko huo.

Miongoni mwa matukio yanayotajwa kuchochewa na mmomonyoko wa maadili ni pamoja na vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vikifanywa na makundi ya watoto kama panya road, ongezeko la matukio ya uvunjifu wa sheria, pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Machi 8, 2023 Rais Samia aliwataka wahudhuriaji wa kongamano la siku ya wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililofanyika mkoani Kilimanjaro kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili unaoendelea katika jamii.

“Kuna mengine ya kuletewa tukatae yale ya kuletewa, sisi kama taifa tukatae yale yakuletewa, kwa sababu yakija hayamuumizi mmoja, leo yamemuumiza jirani kesho yataingia kwako” alisistiza Rais Samia.

Mgawanyiko wa vipindi vya malezi na makuzi

Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Makundi Maalum Dorothy Gwajima amebainisha kuwa viipindi hivyo vitagawanyika mara mbili, ambapo kutakuwa na vipindi vya malezi na makuzi vitakavyofahamika kama ‘Mamakuzi’ na kijana na maadili kitaitwa ‘Kijadili’ vyenye mada 10.

“Vitafanyika (vipindi) kwa njia ya mahojiano na majadiliano kati ya mtangazaji na wataalamu mbalimbali wa malezi, makuzi na maadili kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya jamii na Makundi Maalum…

…Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wataalamu wa afya ya akili na saikolojia, wazazi, walezi na vijana,” amefafanua Gwajima.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...