Serikali yafuta mapori tengefu 12, hifadhi saba

September 24, 2019 6:29 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mapori hayo yaliyofutwa yana ukubwa wa ekari 707,659.94  huku hifadhi saba zilizofutwa zina ukubwa wa ekari 46,715.
  • Yatagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi.
  • Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa.

Dar es Salaam. Serikali imeridhia kufuta hifadhi saba na mapori tengefu 12 ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi.

Mapori hayo yaliyofutwa yana ukubwa wa ekari 707,659.94  huku hifadhi saba zilizofutwa zina ukubwa wa ekari 46,715.

Uamuzi huo umefikiwa jana (Septemba 23, 2019) kweye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  mara baada ya kikao hicho, inaeleza kuwa Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi walichambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri.

“Mawaziri walichambua na kubaini kuwa vijiji vyenye migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa awali, baraza limeamua kwamba vijiji 920 vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” amesema Majaliwa.

Orodha ya maeneo ya vijiji, mapori ya wanyama, misitu na mashamba yaliyofutwa itatangwa baadaye.

“Vijiji 55 vilivyobaki vinaendelea kufanyiwa tathmini ya kina maeneo yaliyobaki ndani ya hifadhi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa ajili ya uamuzi. Uchambuzi na taarifa itatolewa,” amesema Waziri Mkuu.  


Zinazohusiana:


Wakati huo huo, Majaliwa amesema Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.

Baraza la Mawaziri limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer zone (eneo kinga) kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za wanyama ziachiwe vijiji husika na wananchi wasiondolewe kwenye maeneo hayo.

Pia Ofisi ya Makamu wa Rais imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na bahari.

Maamuzi mengine ni kuzitaka Wizara na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa kuweka alama za kudumu zinazoonekana; na kwamba wananchi hawaruhusiwi kuvamia maeneo mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote kuanzia jana.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri waliochambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri, Septemba 23, 2019. Kutoka kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi,  Selemani Jafo; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene; Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina; na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Januari mwaka huu, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Mawaziri nane  wa sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.

Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja na: Kutoviondoa vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi; kubainisha maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za ufugaji na kilimo na kuhakiki na kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

Mengine ni kumega baadhi ya hifadhi za Taifa, mapori tengefu na misitu, kuwagawia wafugaji na wakulima; kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi; upitia upya Sheria ya Vyanzo vya Maji inayozungumzia uhifadhi ndani ya mita 60.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW