Serikali ‘kuwatema’ mawakala ununuzi wa magari ya umma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, amewataka watumishi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini- GPSA, kufanya kazi kwa weledi, alipofanya ziara ya kikazi katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, kubaini changamoto za utekelezaji wa bajeti yake ya mwaka 2018/19 na njia za kuzitatua. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.
- Imesema itaanza kununua magari yake moja kwa moja toka kiwandani.
- Imedai hatua hiyo itapunguza gharama ununuzi na kuokoa pesa za walipa kodi.
Dar es Salaam. Serikali imesema itaanza kununua magari yake moja kwa moja toka viwandani na itaachana na utaratibu uliopo sasa wa kutumia mawakala ili kupunguza gharama za uagizaji magari hayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Khatibu Kazungu aliyekua akizungumza leo (Agosti 7, 2019) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), jijini Dar es Salaam, amesema amesema ununuzi wa magari ya Serikali unatumia gharama kubwa kutokana na kuwatumia mawakala wa ununuzi.
Amesema bei za Mawakala wa Ununuzi ziko juu na zinabadilika mara kwa mara, hivyo kuna haja ya kwenda moja kwa moja kiwandani ili kuokoa fedha za walipakodi zinazopotea.
Aidha, Serikali inaangalia namna itakavyoboresha miundombinu ya GPSA hasa kwa kuwekeza katika visima vya mafuta ili kuwa na mafuta ya kutosha hivyo kusaidia kuongeza ufanisi katika kuhudumia magari ya Serikali.
Soma zaidi: Magari ya kukodi yaongeza gharama uendeshaji balozi
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa GPSA, Dk Geraldine Rasheli, amemshukuru Dk Kazungu, kwa kutembelea taasisi yake na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa ili kupunguza malalamiko katika utoaji huduma na kuongeza tija kwa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Kazungu, anaendelea na ziara ya kikazi katika taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, kuangalia changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na njia za kuzitatua kwa bajeti ya mwaka 2019/20.
Latest



