Serikali haitamvumilia kiongozi atakayekiuka maadili ya umma – Majaliwa

December 10, 2018 10:06 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema itaendelea kuenzi misingi ya utawala bora na haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayetanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.
  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mgongano wa maslahi lazima udhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi binafsi nayo.
  • Itaendelea kuunga mkono na kutekeleza mikataba ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa kuzuia na kupambana na rushwa na makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha miaka 70 ya haki za binadamu, Serikali imesema itaendelea kuenzi misingi ya utawala bora na haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayetanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache huku wananchi wengi wakiendelea kuwa fukara, wakati wachache wakijitajirisha isivyo halali ambapo Serikali itaendelea kuziba mianya ya rushwa jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 inayosisitiza kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.

Akizungumza leo (Desemba 10) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma, ametumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wao ikiwa ndio njia pekee itakayoepusha mgongano wa maslahi.

Mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuisababishia hasara Serikali kwa muda mrefu, tatizo ambalo Majaliwa amesema lazima lidhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi au watumishi wa umma wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi binafsi nayo.

“Mathalan katika Halmashauri zetu wapo madiwani au watumishi wanaoshiriki kutoa maamuzi yanayohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa rushwa.”

Amesema mgongano wa maslahi hutokea pale mahitaji binafsi ya kiongozi yanapokinzana na yale ya umma katika utendaji wake wa kazi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora ambayo Taifa letu linaamini na kuifuata tangu lilipoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. 

Ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono na kutekeleza mikataba na makubaliano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu.

“Sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika ibara ya 145 (a), ambapo tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mojawapo ya agenda yetu ilikuwa ni kuendeleza jitihada za kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria katika ngazi zote za uongozi,” amesema Majaliwa na kuongeza kuwa,

“Jambo hili tumelifanya kwa nguvu kubwa na kwa sasa tumeona kuna mabadiliko makubwa sana miongoni mwa watumishi wa umma katika kutoa huduma kwa wananchi kwa nidhamu, bila upendeleo na kuepuka vitendo vya rushwa.”

Ameongeza kuwa kinachofanywa na Serikali ni kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vyote vinavyokiuka maadili na misingi ya utawala bora kadri inavyowezekana na mafanikio ya jitihada hizo yanaonekana, ambapo baadhi ya watumishi wa umma walikuwa miungu watu  na  kusahau kabisa  kwamba  utumishi  wao  ni wa kuwatumikia  Watanzania. 

“Mafanikio ya hatua hizo ni kurejea kwa  nidhamu katika utumishi wa umma, kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa, kuendelea kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo na kuimarika kwa utamaduni wa kufanya kazi halali ili kupata kipato halali hivyo, kufuta maisha yaliyojaa ujanja ujanja,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yanatoa fursa kwa Serikali kujitathmini kama imefanya juhudi za kutosha kuhakikisha maadili yamezingatiwa katika kila eneo katika kupunguza vitendo vya rushwa, kuimarisha uwajibikaji katika kuutumikia umma na misingi ya utawala bora kwa ujumla wake.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi.

Wengine ni manaibu mawaziri, makatibu wakuu wa taasisi zinazosimamia maadili, haki za binadamu, uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wawakilishi wa washirika wa maendeleo.

Siku ya Haki za Binadamu inaadhimishwa leo duniani kote tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzisha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu mwaka 148 kwa kutambua haki za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kupata chakula na malazi.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
21 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
21 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
21 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Nukta TV

FAHAMU KUHUSU SIKOSELI | Part 1: Ugonjwa wa kurithi, unaotesa maelfu ya watoto Tanzania

FAHAMU KUHUSU SIKOSELI | Part 1: Ugonjwa wa kurithi, unaotesa maelfu ya watoto Tanzania

Nukta TV